Ticker

6/recent/ticker-posts

MKUU WA WILAYA YA HAI ATOA AGIZO KUWEKA MIKAKATI YA KUFAULUSHA


Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga ameziagiza kamati za shule za sekondari pamoja na kamati za maendeleo za kata kuweka mikakati itakayowezesha shule zilizoko katika maeneo yao kuchukuwa wanafunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza.

Makunga ametoa agizo hilo wakati akiendesha harambee ya kuchangia ukamilishaji wa darasa la shule ya sekondari ya Lerai iliyoko katika wilaya hiyo kwa ajili ya maandalizi ya kuchukuwa wanafuni waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza

Makunga ameeleza kuwa kutokana na ufaulu mzuri wa wanafunzi katika wilaya,idadi ya wanafunzi wote waliofaulu wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na hivyo wilaya inahitaji madarasa kumi na mawili.

Alisema kuwa amelazimika kuhitisha haraka zaidi harambe ya shule ya sekondari ya Lerai kutokana na halmashauri ya wilaya ya Hai kuwapanga wanafunzi wote 67 kutoka kijiji hicho jamii ya wafugaji wa Kimasai  katika shule ya sekondari ya Boma ambayo ipo umbali wa kilometa saba.

Alisema kuwa shule hiyo tayari ina chumba cha darasa darasa kinachotumiwa kama ofisi ya walimu huku ikiwa na jengo linalohitaji  kiasi cha shilingi milioni nane na laki saba ili kukamilika na baadaye kutumiwa kama ofisi ya walimu.

Shule ya sekondari ya Lerai iliyoanzishwa mwaka 2011 ina wanafunzi 98 wa kidato cha kwanza na cha pili na hivyo kuchukuliwa kwa wanafunzi hao 67 kutafanya shule kuwa na wanafunzi 165.

Aliwaeleza wananchi wa kijiji hicho kwamba ni vyema kuhakikisha watoto wanasoma katika mazingira rafiki badala ya kutembea umbali mkubwa huku walipigwa na jua na huku njiani wakikutana na watu wa tabia tofauti.

"Nawashukuru kwa kujitokeza kwa wingi na kutoa michango ya ari na  moyo ili kuhakikisha watoto wetu wanasoma hapa hapa katika shule iliyopo jirani badala ya kwenda Boma,"alisema Makunga.

Amezitaka kamati za maendeleo za kata kukutana haraka iwezekanavyo na kamati za shule ili kuweka mkakati wa kuchukiwa wanafuni wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza

Aidha Makunga amemtaka mkurugeni mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hai,Melkizedeck Humbe kuhakikisha anasimamia kwa ukaribu michango yote ya fedha iliyotolewa na wananchi kwa ajili ya kukamilisha madarasa

Katika harambee hiyo jumla ya shilingi milioni tano zilichangwa na jamii hiyo ya wafugaji wa kijiji cha Lerai ambao walifikia maamuzi ya ujenzi kuanza mara moja.

Aidha Makunga alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wananchi wote wa Hai na wadau katika elimu kwa kuwezesha wilaya hiyo kufanya  vizuri katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.

Alisema kuwa wilaya ya Hai kati ya halmashauri saba za mkoa wa Kilimanjaro, imeweza kushika nafasi ya pili kwa kuwa na wastani wa ufaulu wa asilimia 86 ikiwa nyuma ya halmashauri ya manispaa ya Moshi.

Alisema kuwa kwa  mkoa mzima jumla ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ni 40,162 ambapo kati ya hao wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani ni 32,905.

Alisema Kwa upande wa wilaya ya Hai katika mtihani huo wa  darasa la saba waliofanya   watoto 4,826 ambapo kati ya hao waliofaulu na kuchaguliguliwa kidato cha kwanza ni  4,128 sawa na asilimia 85.5.

Alisema kuwa wanafunzi 19 wamefanikiwa kuchaguliwa kujiunga na shule za bweni za ufaulu mzuri zaidi,ufundi na bweni kawaida

Shule hizo kwa upande wa wasichana ni Kilakala,Msalato,Moshi Technical,Iringa,Mgugu na Korogwe na kwa upande wa wavulana ni Ilboru,Tabora,Moshi Technical,Ifunda Technical,Tanga Technical,Iyunga,Mpwapwa,Malangali, Moshi na Songea.

Wilaya ya Hai ina  jumla ya shule za sekondari ambazo ni za serikali 29.

Post a Comment

0 Comments