Ticker

6/recent/ticker-posts

LOWASA ATANGAZA NEEMA KWA POLISI

 

MGOMBEA urais wa CHADEMA na UKAWA, Edward Lowassa, jana amefanya mikutano minne ya kampeni jijini Dar es Salaam na kuvitaja vipaumbele 11 ambavyo atavitekeleza ndani ya siku 100 baada ya kuchaguliwa.

Amesema asipotimiza vipaumbele hivyo ndani ya siku 100, ruksa wananchi kumuuliza.

Vipaumbele hivyo ni kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linaondokana na foleni, pili kufuta michango yote shuleni, tatu elimu bure kuanzia chekechea hadi Chuo Kikuu, nne kuunda mfumo bora wa kulipa na kukusanya kodi ambao utaliwezesha Taifa kuongeza mapato yake, tano kukuza michezo na sanaa.

Kipaumbele cha sita ni kuunda tume ambayo itashughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji, saba kuunda tume ya kushughulikia masilahi ya wafanyakazi, nane kupunguza kodi katika mishahara ya wafanyakazi, tisa kuboresha masilahi ya wanajeshi na askari polisi. 

Lowassa alisema kipaumbele cha kumi, atahakikisha anaboresha huduma za afya kwa akinamama na kuondoa kero wanazopata waendesha bodaboda na mama lishe, kumi na moja kutengeneza mkakati wa kuondoa tatizo la maji nchini. 

"Hivi ndivyo vipaumbele vyangu, nikiingia Ikulu baada ya siku 100, nitawaeleza Watanzania kama nimevifanya au la...nimezunguka maeneo mengi na kuona jinsi Watanzania walivyo na kiu ya mabadiliko; hivyo mwaka huu CCM ni vigumu kurudi madarakani," alisema.

Frederick Sumaye
Waziri Mkuu mstaafu aliyehama CCM na kuhamia upinzani, Frederick Sumaye, alisema Watanzania watajiangamiza wenyewe mwaka huu kama Oktoba 25, mwaka huu, watairudisha CCM madarakani. 

Alisema huu ni mwaka wao wa kufurahia mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa kuiingiza UKAWA madarakani ili kupata maendeleo na mabadiliko ya kweli.  

"CCM wamevunja mikataba na wananchi ambao wameendelea kuwa na maisha magumu...iliahidi maisha bora kwa kila Mtanzania, kutoa ajira lakini hadi sasa hawajatekeleza," alisema Sumaye.

Alimshangaa Jaji mstaafu Joseph Warioba aliposema upinzani hawawezi kuweka historia ya kuiondoa CCM madarakani akimtaka aelewe kuwa, tangu nchi ipate uhuru wananchi wanaishi kwa shida ambapo hiyo ni historia tosha hivyo lazima CCM iondoke madarakani.

John Mnyika
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, John Mnyika, alisema wataendelea kuisumbua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili iweze kutenda haki katika Uchaguzi Mkuu ujao.

"Baada ya UKAWA kutoa taarifa za kinachoendelea ndani ya NEC, Jaji Lubuva anasema tunawabana, lazima tuendelee kuwabana tukiwatumia wataalamu wetu kwenye mfumo wa kuhesabia kura na ndani ya sikunne tunataka awe ametupa majibu," alisema.

Mama Regina Lowassa
Katika hatua nyingine, Mama Regina Lowassa, amewataka wanawake nchini kuyahamasisha makundi mbalimbali ya watu yajitokeze kupigakura ili Taifa liweze kupata viongozi ambao watajali masilahi ya Watanzania.

Mama Lowassa aliyasema hayo Dar es Salaam jana kwenye Kongamano la Wanawake wa Wilaya ya Kinondoni na kuongeza kuwa, kama UKAWA watashinda katika uchaguzi huo, wataunda Katiba mpya itakayozingatiamaoni ya wananchi, kuondoa sheria kandamizi kwa wanawake.

Mwakilishi wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA), Penina Enock, alisema baraza hilo limefanikiwa kuwaweka wanawake pamoja kutoka vyama vyote vinavyounda UKAWA.

Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema Oktoba 25, mwaka huu, wanaume wote walinde kura kwa kukaa mita 100 kutoka kwenye vituo vya kupigia kura na wanawake warudi nyumbani kuwapikia chakula.

James Mbatia
Naye Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, James Mbatia, alisema Tanzania bila CCM inawezekana hivyo kushika dola ni maridhiano na kukitaka Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), kutoa ufafanuzi jinsi watavyokabidhiana madaraka kama uchaguzi utakuwa huru na haki.

Tundu Lissu
Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu, alisema UKAWA watashinda  kihalali wakitumia nguvu ya umma, hivyo CCM itoe ratiba ya kukabidhimadaraka.

Mikutano hiyo minne jana ilifanyika katika Wilaya tatu za jiji ambazo ni Temeke, Kinondoni na Ilala ambapo kwa Upande wa Temeke, mkutano umefanyika katika Viwanja vya Mwembe Yanga na Ilala (Uwanja wa Shule ya Msingi Liwiti-Jimbo la Segerea).

Katika wilaya ya Kinondoni mikutano ilifanyika Tip Top (Sinza) na Tanganyika Packers (Kawe).

Post a Comment

0 Comments