Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAOMBWA KUTENGA FEDHA KILA MWAKA KWA AJILI YA UKARABATI WA SHULE KONGWE YA ILBORU


 
Na Woinde  Shizza,Arusha
SERIKALI imeombwa kuendelea kutenga fedha za ukarabati kila mwaka kwa shule
kongwe ya wanafunzi wenye vipaji maalum ya Ilboru   ili walau kuzirudisha
katika hali yake nzuri na kuzijengea mazingira mazuri ya kujifunzia na
kufundishia, ili zionekane tofauti na shule zingine hatimaye ziwafanye
wanafunzi  wajitume zaidi katika masomo.

Hayo yalisemwa  jana na mkuu wa shule kongwe  ya Ilboru  sekondari  Julius
Shulla alipokuwa akizungumza na wadau wa elimu  na walezi katika mahafali
ya 24 ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo.

Alisema kuwa shule hiyo kongwe na ambayo imekuwa ikitoa wataalamu mbali
mbali imekuwa ina uhitaji wa kukarabatiwa na hivyo ili kuondokana na hali
hiyo serikali inapaswa kutenga fedha kila mwaka ili kuweza kuirejesha shule
hiyo katika mazingira mazuri yatakayowavutia wanafunzi.

Alileleza kuwa shule hiyo inakabiliwa  na changamoto ya uchakavu mkubwa wa
madarasa na nyumba za watumishi hali ambayo inasababisha mara nyingi
wanafunzi kukosa mahala pazuri pa kujifunzia hivyo kuwakatisha tama
kimasomo.

“tunaiomba na kuishauri serikali yetu sikivu iendelee kutenga fedha za
ukarabati kila mwaka kwa shule hizi kongwe ili kuzirudisha katika mazingira
yake mazuri ikizingatiwa hii ni shule ya wanafunzi wenye vipaji maalum
kiakili hali hii itawafnya wanafunzi wajitume zaidi katika masomo kwa kuwa
na mazingi mazuri ya kujifunzia”aliongeza Shulla.

Aidha Shulla alitaja changamoto  zingine zinazoikabili shule hiyo kongwe
kuwa ni pamoja na upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi ambapo
hali hiyo inatokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi
ikilinganishwa na idadi ya walimu.

Alifafanua kuwa tatizo hilo husababisha shule hiyo kutafuta walimu wa muda
wa masomo ya Fizikia,kemia ,na hisabati ambao malipo yao ni makubwa sana
kwa mwezi ambapo shule haina uwezo wa kumudu gharama hizo kila mwezi.

Aliwataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata katika kutatua matatizo
yao na matatizo ya jamii yote kwa kufuata sheria na taratibu za nchi huku
wakijiepusha na uzembe ,ulevi,uvutaji bangi na matumiz ya madawa ya kulevya
kwani hivyo vyote havina tija katika maendeleo.

Post a Comment

0 Comments