Ticker

6/recent/ticker-posts

WAJAWAZITO WAJIFUNGUA KWA TOCHI ZA SIMU

Image result for picha wajawazito
picha na maktaba






Na Woinde Shizza,Arusha

Wajawazito katika zahanati ya kijiji cha Selela kata ya Selela wilaya ya
Monduli mkoani Arusha wamelazimika kujifungua kwa kutumia tochi za simu
pamoja na taa ya chemli kutokana na kukosekana kwa huduma ya umeme kwa
takribani mwezi mmoja na wiki mbili.



Kinamama wa kijiji hicho tumaini shirima na mwasiti hemedy  wameeleza kuwa
wamekua wakiwapeleka wajawazito kwenye zahanati hiyo kwa ajili ya
kujifungua na kushuhudia wauguzi wakitumia tochi za simu kutoa huduma kwa
wajawazito jambo ambalo linawafedhesha hivyo wameiomba serikali isaidie
upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme ili waweze kupata huduma  bora.



“Tunapata shida hata tunapowapeleka Wajawazito zahanati hakuna umeme
wauguzi wanatumia tochi za simu ,juzi tulimpeleka mwenzetu akajifungue
tuliona hilo likijitokeza kwa sababu umeme hakuna”



Mganga wa zahanati hiyo Michael Msalu alisema kuwa nyakati za usiku
wanalazimika kutumia tochi jambo ambalo linaweza kuathiri afya ya mama
mjamzito na mtoto ,vile vile wameshindwa kufanya baadhi ya vipimo maabara
kutokana na kukosa huduma ya umeme .]



Msalu anaeleza kuwa si jambo zuri kiafya kushika simu huku unamhudumia mama
mjamzito unaweza kusababisha maambukizi kwani huduma hiyo inahitaji
uangalifu mkubwa ili kulinda afya ya mama na mtoto pamoja na mtoa huduma.



Diwani wa kata ya Selela Cathbet Meena amesema kuwa licha ya zahanati hiyo
shughuli za kiuchumi na kijamii zimesimama katika kata hiyo ikiwemo
biashara,mashine za kusaga nafaka kwa muda wa mwezi mmoja na wiki mbili
baada ya transfoma iliyowekwa na Tanesco kupata hitilafu baada ya
kuwasiliana na mamlaka hiyo imekua ikitupiana mpira kati ya   Rea katika
maboresho hayo.



Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mkoa wa Arusha  Tanesco ambaye ni Mhandisi
Mkuu Donasian Shamba amekiri kuwepo kwa tatizo hilo ambalo linasababishwa
na masuala ya kitaalamu yanayopelelekea transfoma kuungua mara kwa mara
hivyo wametuma timu ya wataalamu na mapema wiki hii watarekebisha tatizo
hilo ili wananchi wapate huduma.



wakazi wa selela wamelazimika kusimamisha shughuli zao za uchumi
zinazotegemea nishati ya umeme hivyo wanaiomba serikali ichukue hatua ili
waweze kurudi katika shughuli za uzalishaji zinazowaingizia kipato.

Post a Comment

0 Comments