Ticker

6/recent/ticker-posts

CHADEMA YALAANI DIWANI KUSWEKWA RUMANDE

 Katibu wa CHADEMA jimbo la Arumeru Mashariki Elisa Stephen Mungure (Kulia)
akiteta jambo na Diwani wa Kata ya Embaseny Gadieli Mwanda (kushoto) nje ya
Mahakama ya Mwanzo ya Enaboishu jana  mara baada ya kuwekwa rumande kwa saa
48 na mkuu wa wilaya ya Arumeru ambapo jana alifikishwa mahakamani na
kupewa dhamana

Na Woinde Shizza,Arusha


Chama cha Demokrasia na Maendeleo Wilaya ya Arumeru Mashariki kimelaani
vikali kitendo cha Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Alexender Mnyiti kumuweka
rumande Diwani wa Kata ya Embaseny Gadieli Mwanda  kwa saa 48 na kudai kuwa
kitendo hicho ni matumizi mabaya ya madaraka.



Katibu wa CHADEMA  Wilaya ya Arumeru Elisa Stephen Mungure  amesema kuwa
kitendo hicho ni udhalilishaji dhidi ya viongozi wa upinzani ambao wamekua
wakikamatwa mara kwa mara na kuwekwa rumande .



Mungure alisema kuwa mbinu hiyo imekua ikitumika kwa hila ili  kudhoofisha
na kuua upinzani hivyo chama chake kimejipanga kukabiliana na hila hizo za
kisiasa.



“Diwani wa Kata ya Embaseny alitakiwa kuripoti katika kituo cha polisi cha
Usariver septemba 20 mwaka huu ndipo alipokutana na Amri ya Mkuu wa Wilaya
ya kuwekwa ndani kwa masaa 48 bila kuhojiwa  ,jana alifikishwa mahakama ya
Mwanzo ya Enaboishu  na kutuhumiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu
kupitia mradi wa Kuku Kukua ambao Diwani huyo siyo muhusika ,tunamshukuru
Mungu amepata Dhamana”  Alisema Mungure



Akizungumza baada ya kupata Dhamana katika mahakama hiyo Diwani huyo Gadiel
Mwanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema jimbo la Arumeru Mashariki
alisema kuwa Mkuu wa Wilaya alifanya ziara katika kata yake na kuzungumza
na Wananchi ,baadhi ya watu ambao wanadaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM
walimshutumu kuwa anahusika na mradi huo alipotaka kujitetea alinyimwa
nafasi hiyo na kuamriwa kufika kituo cha polisi asubuhi na mapema ndipo
alipokutwa na masaibu hayo.



Mwanda alisema kuwa misigano ya kisiasa inayotekea inalenga kuzorotesha
juhudi za maendeleo ambazo amekua akizifanya kwa kushirikiana na wananchi
jambo ambalo litawaathiri wananchi wengi hivyo amewataka wananchi kuendelea
na juhudi hizo ikiwemo ujenzi wa zahanati ya kisasa.



Kwa upande wao wananchi wa kata hiyo Ester Swai na Agnes Elia wamesema kuwa
kukamatwa kwa viongozi kila mara kunazua hali ya taharuki miongoni mwa
wananchi hivyo wamezitaka mamlaka husika kutimiza majukumu yao kwa
kuzingatia misingi ya haki na usawa.

Post a Comment

0 Comments