Na Woinde Shizza– Arusha
Katika hatua kubwa ya kuimarisha miundombinu ya jiji la Arusha, hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya miradi mikubwa ya maendeleo imefanyika jijini Arusha ambapo imehusisha ujenzi wa soko kuu la Kilombero, soko la Morombo, bustani ya mapumziko ya Themi (Tembo Garden), na kituo kikuu cha mabasi cha Bondeni (Bondeni City).
Miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango wa TACTIC, unaofadhiliwa na Serikali Kuu kupitia mkopo kutoka Benki ya Dunia wenye thamani ya dola za Marekani milioni 410 (bila VAT).
Akizungumza katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Victor Seff, alisema mradi huo unalenga kuboresha miundombinu ya miji 45 nchini na ambapo ita saidia halmashauri katika ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma bora.
“Lengo la TACTIC ni kuziwezesha halmashauri za miji na majiji kukabiliana na kasi ya ukuaji wa miji, pamoja na kujenga uwezo wa ndani wa kiutawala na kifedha,” alisema Seff.
Alisema mkataba wa ujenzi huo umesainiwa na mkandarasi Mohammedi Builders Ltd, ambapo gharama ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa Arusha pekee ni shilingi bilioni 30.6 (bila VAT), na inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 15 kuanzia Mei 15, 2025 hadi Agosti 8, 2026.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Arusha alisema ujenzi wa standi hiyo ni ndoto iliyocheleweshwa tangu makubaliano ya awali mwaka 2019 kutokana na migogoro ya uongozi, lakini sasa mwanga umeonekana ambapo alimshukuru Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo licha ya changamoto zilizokuwepo.
Naye Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, alieleza kuwa serikali haitavumilia wizi au uzembe katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Serikali makini haiwezi kuacha hata shilingi moja ipotee Nitamchukulia hatua kwa yeyote atakayekwamisha maendeleo ya wananchi,” alisisitiza Makonda.
Kwa upande wake Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, akiongea katika hafla hiyo, alisema wanapojenga misingi hii, wanajenga misingi ya maendeleo ya vizazi vya sasa na vijavyo na kubainisha kuwa hii ni safari mpya ya utu wa Mtanzania.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mshikamano ndani ya chama na mkoa wa Arusha, huku akiwataka wakandarasi kuanza kazi mara moja au wajiandae kuchukuliwa hatua.
Waziri Mchengerwa pia alizihimiza halmashauri kuhakikisha miradi hiyo inajiendesha na kuzalisha mapato, huku wananchi wakihimizwa kuitunza miundombinu hiyo kwa ajili ya vya sasa na vizazi vijavyo.
Aidha ameuelekeza uongozi wa Mkoa na Jiji la Arusha kuhakikisha miradi hiyo inakamilika mara moja na endapo kutakuwa na mkwamo wowote wachukue hatua kali
0 تعليقات
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia