POLISI WA UJERUMANI WAMKOSA KABUGA 2007,MWENDESHA MASHITAKA NORWAY ATAKA MTUHUMIWA AFUNGWE MIAKA 21 JELA
Jarida moja la kila wiki la Ufaransa limechapisha habari kwamba
polisi nchini Ujerumani walimkosa kumtia mbaroni mwaka 2007, mtuhumiwa
wa mauaji ya kimbari ya Rwanda anayesakwa vikali, Felician Kabuga huku
Mwendesha mashitaka nchini Norway ameiomba mahakama impatie kifungo cha
miaka 21 jela mfanyabiashra mmoja wa Rwanda kwa kushiriki kwake katika
mauaji ya kimbari mwaka 1994.
NORWAY
Ataka mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari afungwe miaka 21: Jumatatu wiki
hii, mwendesha mashitaka nchini Norway ameiomba mahakama impatie kifungo
cha miaka 21 jela mfanyabiashara mmoja wa Rwanda,Sadi Bugingo, iwapo
atatiwa hatiani kwa mashitaka ya kula njama za kuua watu 2,000 nchini
mwake mwaa 1994.Pamoja na mambo mengine anashitakiwa kwa kudaiwa
kushiriki katika mikutano ambayo mauaji hayo yalipangwa na hatimaye
kutekelezwa.Mwendesha mashitaka iliiambia mahakama kwamba hakuna sababu
zilizotolewa kuomba punguzo la adhabu iliyopendekezwa.
UFARANSA
Polisi wakosa kumtia mbaroni Kabuga: Jarida moja la Ufaransa Jumanne
wiki hii limeripoti kuwa polisi nchini Ujerumani mwaka 2007 walimkosa
kumtia mbaroni mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari anayetafutwa vikali,
Felicien Kabuga.Kwa mujibu wa jarida hilo la kila wiki la Ufaransa,
Jeune Afrique, Kabuga, anayedawa kuwa mfadhili wa mauaji ya kimbari ya
Rwanda ya mwaka 1994, aliingia nchini Ujerumani kwa kutumia hati bandia
ya kusafiria ya Tanzania.Imeripotiwa kwamba mshitakiwa huyo alikwenda
nchini Ujerumani wakati huo kwa ajili ya kupata matibabu ya maradhi ya
kupumua yaliyokuwa yanamsumbua.
Mahakama Ufaransa yanadai jalada la kesi ya Waziri wa Rwanda lina
utata: Mwendesha mashitaka katika Mahakama ya Rufaa mjini Paris,
Ufaransa amedai Jumatano kwamba kumbukumbu za waziri wa zamani wa
Rwanda, anayetakiwa nchini mwake, Hyacinthe Rafiki Nsengiyumva limekosa
ufafanuzi na kukiuka taratibu zinazotakiwa na mahakama. Pamoja na mambo
mengine taratibu zilizokiukwa ni pamoja na Mwendesha mashitaka mmoja
kutia saini hati ya mashitaka na hati ya kukamatwa kwa mshitakiwa huyo.
Lakini akijibu hoja hiyo, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Rwanda, Martin
Ngoga, amelezea kuwa maoni kama hayo ni kiburi cha hali ya juu.
Nsengiyumva alitiwa mbaroni mjini Paris,mwaka 2011, kufuatia hati ya
Rwanda iliyomtaka mshitakiwa huyo iliyotolewa 2008.
RWANDA
Jallow akabidhi Rwanda jalada la Munyarugarama: Mwendesha Mashitaka
wa Taasisi itakayorithi kazi za Mahakama mbili za Kimataifa, Hassan
Bubacar Jallow, Jumatano alikabidhi jalada la mshitakiwa ambaye bado
hajatiwa mbaroni, Kanali Pheneas Munyarugarama kwa Mwendesha Mashitaka
Mkuu wa Rwanda, Martin Ngoga. Sherehe hizo za makabidhiano zilifanyika
mjini Kigali.Munyarugarama ambaye alikuwa Kamanda wa kambi ya jeshi ya
Gako, katika mkoa wa Kigali Vijijini, anashitakiwa kwa mashitaka ya
mauaji ya kimbari, kula njama za kufanya mauaji hayo, uchochezi na
uhalifu dhidi ya binadamu.
WIKI IJAYO
Kesi ya Bemba kuendelea kuunguruma wiki ijayo: Kesi ya utetezi
inayomkabili kiongozi wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC), Jean Pierre Bemba anayeshitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na
uhalifu wa kivita itaendelea kusikilizwa Jumatatu ijayo, Desemba
3,mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC). Uhalifu huo
unadaiwa kufanywa kati ya mwaka 2002 na 2003 katika Jamhuri ya Afrika ya
Kati.
0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia