SERIKALI YAPAMBANA NA VITENDO DHIDI YA MFUMUKO WA BEI YA BIDHAA

Waziri
wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na
vyombo vya habari jijini Dodoma Agosti 15, kuhusu tathmini ya mwenendo
wa bei ya bidhaa bidhaa muhimu nchini na hatua mbalimbali
zilizochukuliwa na serikali kupunguza mfumuko wa bei.Baadhi ya wanahabari wakiwa katika mkutano huo.
Baadhi
ya maafisa wa serikali na wanahabari wakifuatilia kichozungumzwa na
waziri katika mkutano huo.PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA
Mdau, nakuomba uendelee kusoma taarifa kamili hapo chini iliyotolewa na Waziri Dkt Kijaji...
TAARIFA KWA UMMA
_________________________________________________
TATHMINI YA MWENENDO WA BEI YA BIDHAA MUHIMU NCHINI
15/08/2021, DODOMA
1. UTANGULIZI
Ndugu Waandishi wa Habari;
Wizara
ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inashirikiana na Tume ya Ushindani
(FCC) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kutekeleza jukumu la kufuatilia
na kufanya tathmini ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini. Lengo
la tathmini hiyo ni kumlinda mlaji kwa kuhakikisha anapata bidhaa bora
kwa bei stahiki na kuzuia upandishwaji holela wa bei za bidhaa
mbalimbali; pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote
atakayebainika kupandisha bei za bidhaa kiholela bila kuzingatia gharama
halisi za uzalishaji au uingizaji nchini wa bidhaa husika.
Matokeo
ya tathmini zilizofanyika hivi karibuni yalionesha kuwa kuna uhimilivu
mkubwa wa bei (price stability) kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini,
ambazo zilionesha ongezeko dogo la bei ikilinganishwa na bidhaa
zinazoagizwa kutoka nje ya nchi ambazo zilionesha ongezeko kubwa zaidi
la bei.
Ndugu Waandishi wa Habari;
Serikali ya Awamu
ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imefanya jitihada kubwa za kuweka mazingira rafiki
ya ufanyaji biashara nchini, kwa kuchukua hatua mbalimbali katika
kudhibiti ongezeko la bei za bidhaa ikiwa ni pamoja na udhibiti wa
upandishwaji holela wa bei. Kutokana na jitihada hizo, bei za bidhaa
kwenye soko la ndani zimeendelea kuwa na utulivu huku bei za baadhi ya
bidhaa hususan zinazotegemea malighafi kutoka nje ya nchi zikiongezeka
kutokana na kupanda kwa bei za malighafi katika soko la dunia na gharama
kubwa za usafirishaji. Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na
kuimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa mbalimbali ili kupunguza
utegemezi wa kuagiza mahitaji muhimu kama vile vyakula kutoka nje ya
nchi. Aidha, bei za baadhi ya bidhaa zimepanda kutokana na kupanda kwa
bei ya nishati hasa mafuta ya petroli kwenye soko la dunia.
Ndugu Waandishi wa Habari;
Serikali
inaendelea kuchukua hatua mbali mbali kwa lengo la kuwapunguzia
Wananchi athari zitokanazo na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu. Hatua
hizo ni pamoja na kuwapunguzia gharama za uzalishaji au uagizaji na
usambazaji wa bidhaa ili kuleta uhimilivu wa bei (price stability)
kwenye soko. Hatua zilizochukuliwa na Serikali zimelenga kupunguza
athari za mtikisiko wa uchumi duniani uliosababishwa na janga la
UVIKO-19 na vita kati ya nchi za Urusi na Ukraine.
Baadhi ya
hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Bajeti Kuu ya Serikali ya
mwaka wa fedha 2022/2023 na Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 ni pamoja na
hizi zifuatazo:
i) Serikali imeondoa (zero rate)
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wazalishaji wa ndani wa mafuta ya
kupikia yaliyosafishwa (double refined edible oil) kwa kipindi cha mwaka
mmoja kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa hiyo
nchini na hivyo kuleta unafuu wa bei za mafuta ya kupikia kwa mlaji wa
mwisho. Hatua hii imeanza kuonesha mafanikio kwani mwenendo wa bei ya
mafuta ya kupikia unaonesha bei hizo zimeanza kushuka. Serikali pia
inaendelea na jitihada za kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta ya
kupikia nchini hasa alizeti na chikichi kwa lengo la kujitosheleza kwa
mahitaji yetu na kuuza ziada nchi jirani.
ii)
Serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wazalishaji wa
mbolea kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuwapunguzia wakulima gharama za
uzalishaji na hivyo kuleta unafuu wa bei za mazao muhimu ya chakula.
iii)
Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 pia imempa Waziri wa Fedha
mamlaka ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa Wawekezaji
Mahiri hususan watakao wekeza kwenye ujenzi wa viwanda kwa ajili ya
kupunguza utegemezi wa nchi wa kuagiza bidhaa muhimu kutoka nje. Hatua
hii ni ya kuweka uwiano kati ya Sheria ya VAT na Sheria ya Uwekezaji ili
kuweka mazingira yanayotabirika kwa Wawekezaji, kuvutia uwekezaji,
kuongeza uzalishaji wa ndani na hivyo kuleta uhimilivu wa bei.
iv)
Serikali imeanza kutoza ushuru wa asilimia 30 au Dola za
Marekani 150 kwa Tani kwenye usafirishaji wa bidhaa za shaba na chuma
chakavu nje ya nchi kwa lengo la kuwalinda wazalishaji wa ndani wa
bidhaa za chuma, kwa kuwahakikishia upatikanaji wa malighafi za kutosha
na hivyo kuleta unafuu wa bei za bidhaa za chuma hasa nondo kwenye soko
la ndani.
v) Serikali imepunguza ushuru kwa malori
yanayosafirisha bidhaa (transit charges) kutoka Dola za Marekani 16 kwa
kila kilomita 100 hadi Dola za Marekani 10 kwa kila kilomita 100 ili
kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa nchini na hivyo kuleta
unafuu wa bei za bidhaa hizo.
vi) Serikali imepunguza
kiwango cha ushuru wa forodha kutoka asilimia 35 hadi asilimia 10 kwa
waagizaji wa ngano ili kuwapunguzia gharama wazalishaji wa ndani wa unga
wa ngano na hivyo kuleta unafuu wa bei ya unga wa ngano kwenye soko la
ndani.
vii) Serikali pia imeondoa ushuru wa forodha
kwa kutoza kiwango cha asilimia sifuri (0%) badala ya asilimia 10 kwenye
malighafi za utengenezaji wa sabuni (RBD Palm Stearin) kwa lengo la
kuhamasisha na kupunguza gharama za wazalishaji wa ndani wa sabuni ili
kudhibiti ongezeko la bei ya sabuni.
viii) Serikali
imeongeza kiwango cha juu cha ushuru wa forodha kwa bidhaa mbalimbali
zinazozalishwa na viwanda vya ndani kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35
ili kuwalinda wazalishaji wa ndani na kuongeza biashara miongoni mwa
nchi za EAC. Hatua hiyo itawanufaisha wasindikaji wa ndani wa bidhaa za
samaki, nyama, maziwa na mazao ya kilimo ikiwa ni pamoja na kahawa,
chai, mboga na matunda, mafuta ya kupikia, saruji, chumvi, sabuni,
vifungashio, bidhaa za ngozi na samani za mbao kwa lengo la kuleta
unafuu wa bei za bidhaa hizo.
2. MWENENDO WA BEI ZA BIDHAA
i) MAFUTA YA KUPIKIA
Serikali
inatekeleza Mkakati wa kuongeza uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula
ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wakulima kutumia mbegu bora za alizeti na
chikichi (mawese) ili kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kupikia
yatokanayo na mazao hayo. Ongezeko la bei ya mafuta duniani lina athari
hasi kwetu Watanzania, kwani mahitaji ya mafuta ndani ya Taifa letu kwa
mwaka ni tani 650,000 (MT) huku uwezo wetu wa kuzalisha mafuta ni tani
270,000 (MT), ambayo ni sawa na asilimia 41.5 tu ya mahitaji yetu kwa
mwaka. Hivyo ongezeko lolote la bei ya mafuta ya kula kwenye soko la
Dunia lina athari hasi za moja kwa moja kwenye bei ya bidhaa hiyo kwenye
soko letu la ndani.
Wastani wa bei ya mafuta kwa mwezi Julai,
2022 ilikuwa Shilingi 5,000 kwa mafuta yaliyosafishwa mara moja na
Shilingi 9,000 kwa mafuta yaliyosafishwa mara mbili (double-refined).
Kwa mwezi Agosti, 2022 bei zimeshuka kidogo ambapo mafuta hayo yanauzwa
kwa wastani wa bei ya Shilingi 4,500 na Shilingi 8,000 kwa mafuta
yaliyosafishwa mara mbili (double-refined).
ii) SABUNI
Bei
za sabuni za kufulia za mche zimeongezeka katika kipindi cha mwezi
Agosti kutokana na kuongezeka kwa bei ya malighafi za kutengeneze sabuni
zinazoagizwa kutoka nchi za Indonesia na Malaysia. Bei zimepanda kutoka
wastani wa Dola za Marekani 500 hadi 600 kwa tani hadi Dola za Marekani
1,800 kwa tani, hasa baada ya nchi ya Indonesia kuweka zuio la
kusafirisha nje malighafi hizo. Kutokana na ongezeko hilo la bei ya
malighafi bei kwa mche ni kati ya Shilingi 3,000 na 4,500.
Vilevile,
sabuni ya kufulia ya unga inauzwa kwa shilingi 1000 hadi 4500/- kwa
kilo moja (Doffi, Niceone, Killsoft) wakati Omo ikipatikana kwa Shilingi
8000 hadi 8200/- kwa kilo moja.
iii) NGANO
Serikali
inatekeleza Mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la ngano nchini ili
kukabiliana na upungufu wa tani 800,000 tunazoagiza kila mwaka huku
kiasi kikubwa kikitoka katika nchi za Urusi na Ukraine. Mahitaji ya
ngano nchini ni tani 1,000,000 kwa mwaka huku uzalishaji wa ndani ukiwa
chini ya tani 200,000 kwa mwaka. Kwa mwezi Julai, bei ya kilo moja ya
ngano hapa nchini ni wastani wa Shilingi 2,000 na kwa mikoa ya pembezoni
hadi Shilingi 4,000 kwa kilo moja. Aidha, bei hii haikubadilika kwa
mwezi Agosti.
iv) VIFAA VYA UJENZI
a) Saruji
Kwa
sasa nchi yetu ina jumla ya Viwanda 17 vya Saruji vyenye uwezo wa
kukidhi mahitaji ya saruji hapa nchini. Wastani wa bei ya saruji kwa
mwezi Julai ilikuwa kati ya Shilingi 14,500 na 16,500 kwa mfuko wa Kilo
50 wa Saruji ya 32.5R na Shilingi.17,200 hadi 23,000 kwa saruji ya
42.5N. Wastani wa bei ya saruji kwa mwezi Agosti ni Shilingi 14,500 kwa
Saruji ya 32.5R na Shilingi. 17,000 kwa saruji ya 42.5N
b) Nondo
Nchi
yetu ina jumla ya Viwanda kumi na sita (16) vyenye uwezo wa kuzalisha
tani 1,082,788 za nondo kwa ukubwa wa 16mm, 12mm, 10mm na 8mm. Hata
hivyo, kwa sasa uzalishaji wa nondo ni tani 750,000.
Wastani wa
bei ya nondo za 16mm ni kati ya Shilingi 45,000 na 52,000 kwa mwezi
Julai; na Shilingi 41,000 hadi 55,000 kwa mwezi Agosti kutokana na
umbali kutoka viwandani na ongezeko la gharama ya usafirishaji na bei ya
dizeli. Wastani wa bei ya nondo za 12mm ni kati ya Shilingi 24,500 na
30,000 kwa mwezi Julai na Shilingi 24,000 hadi 30,000 kwa mwezi Agosti,
2022.
Wastani wa bei ya nondo za 10mm ilikuwa kati ya Shilingi
19,000 na 23,000 kwa mwezi Julai na Shilingi 18,000 hadi 23,000 kwa
mwezi Agosti; 2022. Wastani wa bei ya nondo za 8mm ilikuwa Shilingi
14,500 hadi 19,500 kwa mwezi Julai na Shilingi 10,000 hadi 18,000 kwa
mwezi Agosti, 2022.
c) Bati
Mwezi Julai, 2022 bati za
gauge 28 iliuzwa kwa wastani wa Shilingi 30,000 hadi 45,000 na mwezi
Agosti inauzwa kati ya Shilingi 30,000 hadi 45,000. Wastani wa bei ya
bati za gauge 30 kwa mwezi Julai ziliuzwa kati ya Shilingi 22,000 hadi
28,500 na mwezi Agosti zinauzwa kati ya Shilingi 22,000 hadi 28,000.
Wastani wa bei kwa bati za gauge 32 kwa mwezi Julai ilikuwa kati ya
Shilingi 19,000 na 26,000 na mwezi Agosti ni kati ya Shilingi 18,500 na
26,000.
v) SUKARI
Mahitaji ya Sukari
nchini kwa mwaka 2021/22 ni wastani wa tani 655,000 ambapo kati ya hizo,
tani 490, 000 ni kwa matumizi ya kawaida na tani 165,000 ni kwa
matumizi ya viwandani. Uzalishaji wa sukari kwa viwanda vya ndani
unakadiriwa kuwa kiasi cha tani 394,606 ambayo ni sawa na asilimia 80.5
ya mahitaji ya sukari nchini kwa matumizi ya kawaida. Aidha, nchi yetu
ina jumla ya
viwanda 5 vya kuzalisha sukari. Kila mwaka
tunalazimika kuagiza sukari kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuziba pengo
la uzalishaji (Sugar gap)..
Katika kipindi cha mwezi Julai na
Agosti 2022, bei ya rejareja kwenye maeneo mengi nchini ni kati ya
Shilingi 2,400 na 3,000 kwa kilo. Maeneo machache hasa ya pembezoni ni
shilingi 3,000 kwa kilo kutokana na ongezeko la gharama za usafirishaji.
vi) BIDHAA ZA VYAKULA
a) Maharage
Maharage
katika masoko yetu yanapatikana kwa wastani wa bei ya Shilingi 1,800
hadi 2,600 kwa kilo. Bei hiyo ni ongezeko la kutoka Shilingi 1,650 hadi
2,600 kwa kilo mwezi Julai, 2022.
b) Mchele
Wastani wa
bei ya mchele kwa kilo ni kati ya Shilingi 1,700 na 3,000 katika maeneo
mbalimbali nchini kwa mwezi Agosti. Bei hii ni ongezeko la asilimia saba
kutoka wastani wa Shilingi 1,600 hadi 2,800 kwa kilo mwezi Julai, 2022.
c) Mahindi na Unga wa Mahindi
Bei
ya zao la mahindi kwa kilo moja haikuonesha mabadiliko yoyote kati ya
mwezi Julai na Agosti, 2022, ambapo zao hilo linauzwa kwa Shilingi 700
hadi 1,500 kwa kilo. Unga wa Mahindi unapatikana kwa Shilingi 1,400 hadi
1,700 kwa kilo mwezi Agosti, kutoka bei ya mwezi Julai ya Shilingi
1,100 hadi 1,700.
d) Ulezi
Wastani wa bei ya
ulezi ni Shilingi 1,200 hadi 3,000 kwa kilo kwa mwezi Agosti na hakuna
mabadiliko ya bei kutoka mwezi Julai, 2022.
e) Uwele
Wastani
wa bei ya uwele ni Shilingi 1,200 hadi 3,000 kwa kilo mwezi Agosti
2022; na hakuna mabadiliko ya bei za mwezi Julai, 2022..
g) Viazi Mviringo
Wastani
wa bei ya viazi mviringo ilikuwa Shilingi 800 hadi 1,500 kwa kilo mwezi
Julai, 2022; na Shilingi 900 hadi 1,400 kwa mwezi Agosti, 2022..
Wizara
ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inaendelea kuchukua hatua za kumlinda
mlaji dhidi ya upandishaji holela wa bei ikiwa ni pamoja na kukutana na
wadau wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa mbalimbali. Vikao vya
wadau kwa ajili ya udhibiti wa bei za bidhaa vilivyoandaliwa na Wizara
na kuhudhuriwa na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na Shirikisho la Wenye
Viwanda Tanzania (CTI); ni pamoja na kikao na wazalishaji wa Saruji
tarehe 31 Januari, 2022 Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa NDC;
wazalishaji wa Nondo tarehe 1 Februari, 2022; na wasambazaji
(distributors) wa vifaa vya ujenzi kilichofanyika tarehe 3 Februari,
2022 Jijini Dododma.
3. FURSA ZA MASOKO YA BIDHAA ZINAZOZALISHWA NCHINI
Serikali
inaendelea na jitihada mbalimbali za kutafuta masoko ndani na nje ya
nchi kwa ajili ya mazao na bidhaa zinazozalishwa nchini. Wizara ya
Uwekezaji, Viwanda na Biashara inaunga mkono jitihada za Mheshimiwa
Samia Suluhu Hassan za kuifungua nchi, kuvutia uwekezaji na utalii kwa
kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini. Matokeo ya jitihada
hizo yameanza kuonekana ambapo kwa mwezi Agosti, 2022, fursa mbalimbali
zimepatikana katika masoko ya Kimataifa kwa mazao yanayozalishwa nchini
kama inavyoonekana kwenye Jedwali hapa chini:
Na.
Bidhaa
Kiasi Kinachohitajika (Tani)
Wanunuzi Walipo
1
Mtama Mweupe
205
Kenya
2
Mashudu ya Soya
200
Uganda
3
Maharage ya Njano
1,000
Kenya
4
Fiwi
1,000
Kenya
5
Maharage ya Soya
1,660
Kenya
6
Kunde
30,000
Uganda
7
Ulezi
3,000
Kenya
8
Mahindi
1,000
Kenya
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) itawaunganisha wazalishaji wa mazao hayo na wanunuzi kupitia barua pepe: enquiries@tantrade.go.tz /info@tantrade.go.tz Aidha, taratibu za kusafirisha bidhaa hizo nje ya nchi zimeainishwa kwenye tovuti ya trade@tanzania.go.tz.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Napenda
kuhitimisha taarifa yangu, kwa kuuhakikishia umma wa Watanzania kwamba
Serikali itaendelea kufuatilia, kufanya tathmini na kusimamia ushindani
wa haki katika soko, kwani ni wajibu wa Serikali kumlinda mlaji.
Dkt. Ashatu K. Kijaji (Mb.)
WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA
15 AGOSTI, 2022
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia