HIZI NDIZO NCHI ZA AFRIKA ZINAZORUHUSU NDOA ZA UTOTONI
Takriban wasichana na wanawake milioni 650 walio hai leo waliolewa kabla ya kutimiza miaka 18
‘Ndoa ya utotoni’ ni muungano rasmi au usio rasmi ambao angalau mmoja kati ya wanandoa ni chini ya umri wa miaka 18.
Takriban wasichana na wanawake milioni 650 walio hai leo waliolewa kabla ya kutimiza miaka 18. Zaidi ya milioni 50 kati yao wanaishi Mashariki na Kusini mwa Afrika. Kwa mujibu wa shirika linaloshughulikia haki za watoto unicef Takriban theluthi moja (asilimia 32) ya wasichana wa eneo hilo waliolewa kabla ya umri wa miaka 18.
Mashirika na watetezi wa watoto wamekua wakihusisha sheria, tamaduni na matakwa ya dini kwa baadhi ya jamii za Afrika, kuwa ni chanzo kikubwa cha ndoa za utotoni.
Mapendekezo ya jumuiya ya kimataifa ya umri wa kuoa na kuolewa ni miaka 18 na kuendelea. Lakini mbali na mapendekezo hayo bado baadhi ya nchi sheria zake zina ruhusa ndo za chini ya miaka 18, hususani kwa watoto wa kike.
pamoja na mapendekezo hayo lakini baadhi ya nchi barani Africa zina sheria zenye mwanya wa kusababisha ndoa za utotoni hususani kwa watoto wa kike.
Tanzania miaka -15, 14 kukiwa na sababu muhimu
Sheria ya ndoa ya Tanzania, inatoa mwanya kwa mtoto wa kike kuolewa kuanzia miaka 15 na kuendelea , huku kwa miaka 14 lakini si chini ya hapo ruhusa maalum inhaitajika kutoka na mazingira ya mtoto mwenyewe ikiwemo suala la ujauzito
Lakini sheria hiyo imepingwa na wanaharakati mara kadhaa, na mahakama nchini humo iliamuru kubadilishwa na umri wa kuolewa kwa watoto wa kike uanzie miaka 18 na kuendelea kama ilivyo kwa watoto wa kiume.
Lakini tangu kutolewa kwa maamuzi ya mahakama miaka zaidi ya mitatu imepita bila mabadiliko hayo kutekelezwa.
Matatizo yaliyopo katika Sheria hii ni pamoja na kukianzana na sheria ya mtoto ambayo inamtafsiri mtoto kama mtu yoyote alieko chini ya umri wa miaka 18.
Hata hivyo hivi karibuni rais wa nchi hiyo Samia Suluhu alisema kuwa wanashughulikia mabadiliko ya sheria hiyo kandamizi kwa mtoto wa kike.
Mahakama iliamuru Tanzania kufanya marekebisho ya umri wa kuolewa kwa mtoto wa kike
Cameroon 15, chini ya 15 kukiwa na ulazima
Nchini Cameroon kanuni ya Kiraia (Kifungu cha 144) inaruhusu ndoa kwa wasichana kutoka umri wa miaka 15, na hata chini ya miaka 15 kukiwa na hali ya ulazima wa (Kifungu cha 145)
Sambamba na hilo, rasimu ya toleo lililorekebishwa la Kanuni ya Kiraia inashikilia masharti kadhaa (Kifungu cha 294 – 303) ambayo yanasalia kuwa mazuri kwa ndoa za utotoni, kwani yanaruhusu ndoa kwa ridhaa ya wazazi; hivyo, hata marekebisho ya Kanuni ya Kiraia haionekani kuwa na mwelekeo wa kuzuia ndoa za utotoni.
Gabon- miaka 15
Chini ya Kanuni ya Kiraia ya 1995 umri wa chini wa kisheria wa kuolewa kwa wasichana nchini Gabon ni miaka 15, na miaka 18 kwa wavulana. Hata hivyo Kifungu cha 203 cha Sheria ya Kiraia kinaeleza kwamba Rais wa Jamhuri au Rais wa Mahakama ya Juu anaweza kuidhinisha ndoa zilizo chini ya umri wa chini kabisa "ikiwa kuna sababu za msingi’’.
Sudan - kuanzia miaka 10
Sheria ya Hali ya Kibinafsi ya Waislamu, ambayo iliratibiwa mwaka wa 1991 chini ya utawala wa Kiislam-Kijeshi wa Omar al-Bashir (1989-2019) inasema kwamba wasichana wenye umri wa miaka 10 wanaweza kuolewa.
Kando na kuweka umri wa ndoa katika balehe, ambayo iko katika muktadha wa kisheria wa Sudan unaofasiriwa kuwa miaka 10, inazuia uasherati.
Licha ya shinikizo la kimataifa na la ndani la kufanya miaka 18 kuwa umri wa chini zaidi wa kuolewa, Sheria ya Kibinafsi ya Kiislamu imesalia bila kubadilika hata katika kipindi cha mpito cha muda mfupi chini ya uongozi wa Abdallah Hamdok.
Ingawa Sudan imeidhinisha Mkataba wa Haki za Mtoto, imeshindwa kuzingatia pendekezo lake la kuweka miaka 18 kama umri wa chini wa kuolewa.
Uhalalishaji wa ndoa za utotoni ndani ya mfumo wa Sharia umefanya kuwa changamoto kwa mashirika ya haki za wanawake kutetea dhidi yake.
Kwa mujibu wa shirika la Girls Not Brides asilimia 34 ya wasichana nchini Sudan huolewa kabla ya umri wa miaka 18 na 12% huolewa kabla ya kutimiza miaka 15.
Ndoa za utotoni zimeenea zaidi Darfur Kusini na Mashariki (ambapo 56% ya wanawake wenye umri wa miaka 20-49 waliolewa kabla ya umri wa miaka 18), Darfur ya Kati (55%), Blue Nile (50%) na Gadarif (49%).
Mali- miaka 16
Sheria ya Familia ya nchini Mali (“Kanuni za Familia”) inaweka umri wa chini wa kuolewa kuwa miaka 18 kwa wanaume na 16 kwa wanawake, na inaruhusu watoto kuolewa kuanzia umri wa miaka 15 kwa idhini ya mama au baba kwa mtoto wa kiume, lakini kupitia ridhaa ya baba tu kwa mtoto wa kike.
Kwa mujibu wa Unicef Viwango vya ndoa za utotoni viko juu zaidi katika eneo la Afrika Magharibi na Kati, ambapo karibu wasichana 4 kati ya 10 waliolewa kabla ya umri wa miaka 18.
Lakini kutokana na jitihada za mashirika ya kutetea haki za watoto, nchi nyingi zimekubali umri wa kuoa na kuolewa usiwe nchini ya miaka 18.
Lakini mtihani mkubwa unabaki kwenye mila na desturi, tamaduni, dini na mazoea ya jamii juu ya ndoa za mapema.
Kukosa elimu ya madhara ya ndoa za utotoni pia ni janga kubwa miongoni mwa jamii nyingi barani Afrika.

0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia