TBN yashukuru serikali kwa mafunzo ya mabloga kuelekea uchaguzi mkuu
Na mwandishi wetu ,Dar es Salaam
CHAMA cha Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) kimesema kimeridhishwa na juhudi za serikali kuwapatia wanachama wake mafunzo maalumu yatakayoongeza weledi, uzalendo na uwezo wa kupambana na taarifa potofu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema mafunzo hayo yatahusisha mabloga zaidi ya 200 wakiwemo wale wanaoishi nje ya nchi, ambapo mazungumzo kati ya TBN na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) tayari yamefikia hatua za mwisho za utekelezaji.
“Tumekuwa tukishirikiana kwa karibu na TCRA ambao wametuthibitishia kuwa wako katika hatua ya mwisho ya kutekeleza maagizo ya serikali kuhusu mafunzo haya muhimu,” alisema Msimbe.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwajengea mabloga uwezo wa kutambua na kupambana na habari feki, kuimarisha uzalendo, na kusambaza taarifa sahihi zitakazosaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi wakati wa uchaguzi.
Msimbe aliongeza kuwa baadhi ya mabloga wanaoshiriki ni mara yao ya kwanza kushiriki uchaguzi mkuu, hivyo ni muhimu kujengewa msingi wa kimaadili, uelewa wa katiba, na nafasi ya vyombo vya habari katika kulinda amani na demokrasia.
“Uamuzi huu wa serikali wa kutupatia mafunzo ni hatua muhimu kwa taifa letu. Tunahitaji kujifunza, kukumbuka misingi ya taifa, na kuelimika kuhusu nafasi yetu kama wachangiaji wa amani na demokrasia,” alisema.
Kwa mujibu wa TBN, zaidi ya wanachama 150 walioko mikoa mbalimbali watahusika moja kwa moja na mafunzo hayo, na tayari uongozi wa chama hicho umeanza mchakato wa kusajili taarifa sahihi za wanachama kupitia Mratibu wa TBN, Bw. Gadiola Emanuel.
Aidha, Msimbe alitoa wito kwa mabloga ambao bado hawajajiunga na TBN kuchangamkia fursa hiyo ili wawe sehemu ya wanufaika wa mafunzo, huku akieleza kuwa chama hicho kinajumuisha watengeneza maudhui kutoka sekta mbalimbali kama michezo, siasa, afya, uchumi, na jamii kwa ujumla.
Kwa hatua hiyo, serikali inaweka msingi wa kuwajengea mabloga uwezo wa kutoa taarifa za kweli zenye kulinda misingi ya uwajibikaji, uwazi, na haki kuelekea uchaguzi huru na wa haki.
.jpg)
0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia