BREAKING NEWS

Thursday, September 17, 2015

MFA MAJI HAACHI KUTAPATAPA

Na Haji Kombo
Wakati homa ya uchaguzi ikiwa inazidi kupanda nchini Tanzania, huku Khatamu za Uongozi zikiwa zinateleza mikononi mwa Chama Tawala cha Mapinduzi (CCM) kilizokuwa kikizishikilia kwa zaidi ya miaka 50 sasa, viongozi wa chama hicho wamekuwa wakikuna vichwa na kujaribu kuleta fikra mpya za kukinusuru Chama chao kisisambaratike.
Ni wazi kabisa kuwa CCM imo katika pumzi zake za mwisho, na kama methali ya Kiswahili isemavyo, "Mfa maji haachi kutapatapa". Maana ya methali hiyo inaonekana wazi katika muda huu mfupi uliobakia kabla ya Watanzania kuelekea kwenye visanduku vya kupigia kura na kuamua hatima ya nchi yao.
Inavyoelekea ni kuwa CCM wameshakubali kuwa hawawezi kushinda kwa njia za halali, na wananchi wameshashtuka. Kwa hivyo, basi kutokana na ukweli huo, hivi sasa CCM imeelekea mataifa ya nje kujaribu kuyarubuni kwa propaganda ili iwapo mambo yatawaendea vibaya basi mataifa hayo yaiunge mkono kwa hatua watakazo zichukua.
Katika makala yenye kichwa cha khabari: "Tanzania cannot be allowed to be the new front for terrorists" (Tanzania haiwezi kuruhusiwa kuwa uwanja mpya wa magaidi) iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa CCM bwana Abdulrahma Kinana na kuchapishwa kwenye tovuti ya "The Hill" tarehe 10/09/2015, http://thehill.com/blogs/congress-blog/foreign-policy/253142-tanzania-cannot-be-allowed-to-be-the-new-front-for, CCM inadhihirisha wazi jinsi ilivyoishiwa na sera, na sasa inakimbilia propaganda zilizopitwa na wakati.
Nimeifasiri kwa Kiswahili makala hiyo kwa faida ya sote. Tafadhali kuwa mvumilivu kwa makosa yoyote ya kiufasiri au kiutaalamu yatakayojitokeza, na chambua mwenyewe ni ujumbe gani CCM wanautuma kwa nchi za Magharibi? na iwapo nchi hizo zitarubunika kwa propaganda hizo, basi ni jambo la kusubiri na kuona hapo Oktoba 25 mwka huu.
Ifuatayo ndiyo makala yenyewe:
Tanzania Haiwezi Kuruhusiwa Kuwa Uwanja Mpya Wa Magaidi
Magaidi
Mnamo mwaka 2013, walimu wawili wa kujitolea kutoka Uingereza, Kate Gee na Kristie Trup - wote wawili wakiwa wasichana wadogo wakati huo - walikumbwa na mashambulizi mabaya wakati wakiwa Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Tanzania, Afrika Mashariki,wakati watu wawili wakiwa wanaendesha mapikipiki walipowamwagia tindikali nyusoni mwao. Baada ya kusafirishwa kwa ndege na kurejeshwa jijini London, madaktari waliondoa asilimia 30 ya ngozi iliyokuwa imeharibika kutoka mwili wa Kate Gee ambaye ndiye aliyeathirika vibaya zaidi. Mwaka mmoja baadaye, bado alikuwa anahitajika kuvaa kizibo cha plastiki ili kupunguza athari za makovu yaliyokuwa yamegubika uso wake.
Zikisaidiwa na Wapelelezi kutoka Uingereza na Polisi ya Kimataifa (Interpol), hatimaye mamlaka husika nchini Tanzania ziliwatia mbaroni wanachama wa lenye makundi la kigaidi la Kiislam la UAMSHO mafungamano na Boko Haram. Watu hao tayari wameshafunguliwa mashataka Mahkamani. Uamsho imekuwa na historia ya kuwashambilia wageni na hata viongozi wa Kidini wa Kiislamu na wa Kikristo ambao hawakubaliani na lengo lao la kuusambaratisha Muungano wa Tanzania kwa njia za Ugaidi, na baadaye kuigeuza Zanzibar kuwa Dola yenye misimamo mikali.
Hata baada ya mashambukizi dhidi ya Gee na Trup ambao walikuweko Zanzibar si kwa lengo jengine lolote zaidi ya kuwasaidia watu wengine, na ambao hawakuwa na lengo la kumdhuru mtu yoyote, basi kama tulivyosikia katika wiki chache za kampeni za uchaguzi nchini Tanzania, mgombea wa upinzani Edrward Lowassa amedhihirisha wazi uungaji wake mkono wa malengo ya watu hawa wenye misimamo mikali. Kwa miaka kadhaa, swala la hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano wa Tanzania limekuwa ni swali muhimu kwa wananchi wa kisiwa hicho. Ni idadi ndogo mno ya watu wanaohubiri kutaka kujitenga na Bara ambayo iliungana nayo mwaka huo huo ilipoing'oa madarakani serikali ya Kiarabu. Hakuna ubaya wowote kuendeleza mijadala yenye uhalali kamili kisiasa maadam inaendeshwa kwa njia za amani na kidemokrasia.
Lakini swali linabakia kuwa, ni kwa muda gani itawezeakana kwa mjadala kama huo kuendelea kuwa wa amani iwapo upinzani utafanikiwa katika uchaguzi mkuu ujao nchini Tanzania? Lowasssa ambaye ambaye baada ya kuwa Waziri Mkuu kwa miezi 18 tu alilazimishwa na Bunge kujiuzulu wadhifa wake huo kutokana na kashfa za ufisadi, ameahidi kuwaachia huru watu hao waliofanya mashambulzi ya tindikali. Kuwaruhusu watuhumiwa hao wa ugadi 'kupiga miswere" wakiwa huru, na bila shaka yoyote kuanza tena harakati zao za matumizi ya nguvu, kutahatarisha usalama wa raia wa kawaida wa Zanzibar, wa Tanzania Bara - ambao wengi wao wana misimamo ya wastani wakiwa wafuasi wa dini ya Kiislamu au Kikristo - na wageni kutoka nje, ambao wengi wao ni kutoka Uingereza.
Lowassa anapendekeza hili kama jaribio lake la kufa na kupona la ulafi wake wa kuupata Uraisi. Mara tu baada ya jaribio lake la kupata ridhaa ya kugombea Uraisi kwa tiketi ya Chama tawala cha Mapinduzi (CCM) kukataliwa na wapiga kura, alikihama chama hicho na kujiunga na upinzani, ambao ulimfanya kuwa mgombea wake. Viongozi wa Upinzani wenye misimamo ya wastani kama vile Profesa Ibrahim Lipumba aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) chenye ushawishi mkubwa Zanzibar, walijiuzulu kulalamikia dhidi ya hatua hiyo, na kama hatua ya kuiunga mkono Serikali. Tunaweza kudhani tu kuwa hatua ya Lowassa ya kujiunga na makundi haya yenye misimamo mikali ni majibu ya mtu aliyesalimu amri mbele ya ukweli kuwa Wazanzibari wengi katika ngome hiyo ya muda mrefu ya upinzani, wamekuwa wakikataa kuunga mkono juhudi zake za kuwania Uraisi.
Lakini kwa kiasi cha kushangaza, hali siyo kama hivyo.Hatua hii imewakasirisha viongozi wengi wa Kikristo ambao wameitolea wito serikali wa kuitaka kuwafungulia mashtaka mara moja watu wenye misimamo mikali ambao kwa kiasi kikubwa inaaminika kuwa walichoma Makanisa na kuendesha matendo ya utumiaji nguvu yaliyowalenga Wakristo yakiwemo mashambulizi ya tindikali. Ni wazi kabisa kuwa Lowassa hana hamu ya kuwasaidai Watanzania, bali hamu yake ni kujisaidia mwenyewe kuingia madarakani na ngawira ambazo anaamini zinamsubiri huko. Mwisho wa yote, tabia za Lowassa zinajulikana vizuri siyo tu na Watanzania, bali pia na nchi za Magharibi. Katika moja kati ya mawasiliano mengi ya Kidiplomasia ya Marekani yenye kumzungumzia Lowassa uliyoyaweka hadharani, Mtandao wa Udukuzi wa Wikileak umefichua wazi jinsi Wamarekani wanavyomuona Lowassa, pale Balozi wa zamani wa Marekani nchini Tanzania Bwana Mark Green aliposema: "Kwa miaka mingi sasa, harakati za ufisadi za Lowassa zimekuwa si siri tena Tanzania nzima".
Si Tanzania wala nchi za Magharibi amabzo zinaweza kuthubutu kuiona Tanzania ikigeuka kuwa uwanja mpya wa harakati za kigaidi Barani Afrika kwa kupitia maamuzi ya Lowassa. Licha ya mashambulizi ya kutisha yaliyoyafanya katika miaka iliyopita, hata hivyo bado hayajadhihirisha kuwa yana nguvu kama makundi mengine ya Kijihadi kama vile Al-Shabab au Boko Haram. Bila shaka ikilinganishwa na majirani zetu kama vile Kenya, tunashukuru kuwa Tanzania imekuwa na amani na imesalimika na matendo ya utumiaji nguvu.
Wakati swali la ni nani anayeongoza Tanzania ni raia wa nchi yangu pekee wenye haki ya kulijibu, basi Uingereza na washirika wake katika vita vya mapambano dhidi ya ugaidi wa Kiislamu zina haki ya kuwa na wasiwasi mkubwa iwapo Lowassa atashinda na hatua alizoahidi kuzichukua dhidi ya watu wenye misimamo mikali. Wakati Al-Shabab waliposhambulia jengo la Biashara la West Gate mjini Nairobi mwaka 2013, serikali za Uingereza na Marekani zilitoa tahadhari ya kusafiri kwa raia zao zikiwataka kutotembelea maeneo mengi ya Kenya. Hatua hii iliathiri vibaya sekta yao muhimu ya Utalii: bila shaka yoyote ile, kushamiri kwa harakati za kigaidi Zanzibar, kutaiangamiza sekta ya Utalii Tanzania, khususan ile ya Zanzibar ambayo kisiwa hicho kinaitegemea mno.
Kwa hivyo, chaguo ambalo Tanzania inakabiliana nalo katika uchaguzi ujao lina athari ndani na nje ya mipaka yake. Iwapo Lowassa na waungaji wake mkono wa upinzani watashinda, ingawaje uwezekano huo ni mdogo kwa mujibu hali ilivyo hivi sasa, basi nchi iko katika hatari ya kuwa uwanja mpya wa magaidi, katika wakati ambao magaidi wanaendelea kushindwa katika nchi nyengine Barani Afrika.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates