KODI YA VINGAMUZI YAFIKIRIWA KUONDOLEWA
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba
Serikali inakusudia kupunguza au kuondoa kabisa kodi katika
ving’amuzi ili kuwezesha Watanzania wengi kumudu kununua vifaa hivyo na
kupata huduma ya matangazo ya runinga.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba alisema jana kuwa kwa sababu Serikali
inatekeleza makubaliano ya kimataifa ya kuhamia mfumo wa dijitali kutoka
analojia, ni vyema kila Mtanzania akawa na uhakika wa kupata huduma ya
matangazo ya runinga na hilo haliwezi kufanikiwa iwapo bei ya ving’amuzi
itaendelea kuwa juu.
Akizungumza kwenye mkutano wa 21 wa Umoja wa
Taasisi za Utangazaji Kusini mwa Afrika (Saba), Makamba alisema hivi
sasa wizara yake inawasiliana na Wizara ya Fedha pamoja na wadau wengine
kuangalia njia bora na sahihi ya kufanikisha lengo hilo.
“Tayari serikali imepunguza viwango vya kodi
kwenye ving’amuzi ili kuwapa nafuu wananchi, lakini tunafikiria
kuipunguza zaidi au kuondoa kabisa kodi ili kuwezesha Watanzania wote
wenye seti za televisheni kupata matangazo ya runinga,” alisema Makamba.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Profesa John Mkoma alisema Tanzania
inajivunia kufanikiwa kutekeleza malengo ya kimataifa ya kuhamia mfumo
wa dijitali kutoka analojia kulinganisha na nchi zingine za SADC.
Alisema matumizi ya king’amuzi imerahisisha
gharama za matangazo ambapo hivi sasa mtu anaweza kurekodi kipindi na
kukipeleka kwenye kituo cha Tv au redio kwa ajili ya kurushwa hewani.
Profesa Mkoma alisema matumizi ya dijitali pia
yameboresha usikivu wa sauti na muonekano wa picha kwenye vituo vya
televisheni nchini.
Tanzania ilianza kuingia kwenye mfumo wa dijitali
kwa kuzima mitambo ya analojia kuanzia mwishoni mwa mwaka jana kwa
kuanzia na mkoa wa Dar es Salaam mpango ulioendelea kwa mikoa mingine ya
Tanzania.
Tayari baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki yameanza kufuata hatua hiyo ya Tanzania.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia