MWENYEKITI wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, amesisitiza msimamo wake wa kuwashughulikia wajumbe wa Bunge hilo wenye nia ya kuvunja Muungano uliodumu kwa miaka 50 sasa.
Awali kabla ya kusisitiza msimamo wake, Mjumbe wa Bunge hilo, Mchungaji Christopher Mtikila, alidai kuwa kauli hiyo ilimlenga yeye kumtisha kutokana na msimamo wake wa kupinga Muungano.
Mtikila alibainisha hayo wakati wa kipindi cha maswali katika semina ya uzoefu wa Kenya katika upatikanaji wa Katiba mpya kwenye mada iliyotolewa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya, ambaye sasa ni Seneta wa Busia, Amos Wako.
“Hao watashughulikiwa namna gani?…Muungano ni kikundi cha watu wachache wa CCM ambao ni milioni mbili na si Watanganyika wote milioni 47…watu wanalazimishwa na maslahi lakini saa ya ukombozi imefika sasa, sitabadilisha tutashinda,” alisema Mtikila huku sauti zikisikika ‘imetoshaaaaa kaaa’. Akijibu hoja hiyo, Sitta alisema:
“Mtikila huna haja kuogopa, hii ni nchi ya kidemokrasia na tuliposema tutawashughulikia tunamaanisha kuwa tutawashughulikia kisheria na humu ndani (bungeni) tutawashughulikia kikanuni.”
Kabla ya kusisitiza suala la kuwashughulikia wanaotaka kuvunja Muungano, kwa mara ya kwanza katika Bunge hilo, Sitta alieleza nia hiyo alipokuwa akiwashukuru wajumbe wa Bunge hilo waliomchagua kuwa Mwenyekiti.
“Nawashukuru wajumbe kwa kunichagua, kuna wajumbe wawili au watatu katika maelezo na michango yao wameonyesha dhamira ya kuuvunja Muungano hawa nitashughulika nao kikamilifu,” alisema alipopewa nafasi ya kutoa neno la shukrani kwa kuchaguliwa na wajumbe wa Bunge hilo kwa kura nyingi.
Rais Mbali na suala la kushughulikiwa, Mtikila pia alihoji kauli iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, aliyewataka wabunge kuonesha staha leo wakati Rais Jakaya Kikwete atakapokuwa akihutubia Bunge hilo.
Profesa Mwandosya katika hilo, alisema watu wote leo macho na masikio yao yatakuwa Dodoma kusikiliza Rais anasema nini juu ya mustakabali wa nchi na Muungano.
Alitoa mfano wa Marekani, kwamba Rais Barack Obama anapokwenda kuzungumzia Muungano wa Majimbo ya Marekani, hata askari wa usalama barabarani huwa hawakai barabarani kwa kuwa wote wanakwenda kusikiliza. Kwa Uingereza wakati Malkia akihutubia Bunge, siku hiyo inakuwa ya heshima na kipaumbele sana.
Aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuepusha rabsha yeyote siku hiyo, na kama kuna watu wamepanga kufanya hivyo, wafanye siku nyingine na si siku hiyo. Lakini Mtikila katika hilo alisema:
“Rais (Jakaya Kikwete) anakuja kuzungumza hapa bungeni na kumetolewa mwito na Mwandosya wa kuheshimu viongozi ila wamesahau kwa kina Tony Blair tumeona wakipigwa mayai yaliyooza, nyanya zilizooza.
“Hii ni mbaya na inajenga uoga, tuwe wajasiri, Mungu Amesema onya na kukaripia kwa usahihi tukimkataa Mungu Bunge litakuwa gharika…mtu asimtishe mtu humu tuwe waaminifu kwa aliyeajiriwa na wananchi (Rais); akifanya vizuri tumshauri; lakini akifanya vibaya tumrekebishe,” alisema.
Akifafanua hoja hiyo, Sitta alisema;“Hatutarajii humu mtu aje na mayai viza…Mwandosya amezungumzia staha na hatutarajii mtu aje humu ndani avunje staha, pinga kwa staha.”
Katika hatua nyingine, Seneta Wako aliwashauri wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kutoiga kila kitu kutoka kwenye Katiba za nchi nyingine bali wajifunze na kutunga Katiba inayoendana na mazingira ya Tanzania.
Wako ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya kwa miaka 21 na kustaafu mwaka 2011, ameshauri Bunge hilo kuangalia namna ya kuunda chombo cha kufuatilia utekelezaji wa haraka wa Katiba mpya watakayounda.
Akizungumzia uzoefu wa Kenya katika kuipata katiba mpya, safari iliyoanza mwaka 1991 na kupatikana mwaka 2010, alisema “msiige uzoefu wote wa Kenya ila jifunzeni na mpitie kisha muangalie cha kuchukua isiwe kama Biblia, hakikisheni hamrudii makosa tuliyofanya Kenya.”
Aliwataka wajumbe hao kuangalia namna ya kuunda chombo cha kufuatilia utekelezaji wa haraka wa Katiba mpya na kutolea mfano nchini mwake ambako kumeundwa Tume ya kufuatilia utekezaji wa katiba iliyopewa miaka mitano kufanya kazi ambapo imekuwa ikifuatilia vipengele visivyotekelezwa au kunapokosewa.
“Mfano Rais Mwai Kibaki alipoteuliwa, aliwateua Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu na Mkurugenzi wa Mashitaka lakini Tume ilipinga na uteuzi ukafutwa,” alisema na kuongeza:
“Wananchi pia wanafuatilia Bunge linapofanya kazi na iwapo kuna kipengele hakijatekelezwa, wanahoji na kunaweza kuongezwa mwaka mmoja lakini Mkenya wa kawaida anapoona Bunge halifanyi kazi yake, anaweza kwenda mahakamani na ikaamuliwa Bunge livunjwe,” alisema.
Aliwataka wajumbe wa bunge hilo kubadili fikra zao kwenye utekelezaji wa mambo kadhaa kama walivyozoea zamani na kutolea mfano wa mabadiliko ya Kenya kwa upande wa Jaji Mkuu ambapo duniani kote anateuliwa na Rais, lakini nchini kwake ni nafasi ya kushindaniwa na usaili wake hufanyika kupitia televisheni na kila mtu anaona.HABARILEO