Rais Jakaya Kikwete. DODOMA. RAIS Jakaya Kikwete LEO ataambatana na
ujumbe mzito wa marais wastaafu wa pande zote za Muungano, wake wa
waasisi wa taifa na mawaziri wakuu wastaafu atakapokwenda kuzindua Bunge
Maalumu la Katiba. Hatua ya Rais
kuambatana na ujumbe huo imepongezwa na viongozi wa vyama vikuu vya
upinzani nchini, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na mwenzake
wa Chadema, Freeman Mbowe. Mbali na viongozi hao, Rais
Kikwete pia ataambatana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar, Seif Sharif Hamad. Wanaotarajiwa kuwamo katika
msafara huo ni Rais wa pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa
tatu, Benjamin Mkapa na marais wastaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour na
Amani Abeid Karume, Mama Maria Nyerere na Mama Fatma Karume. Miongoni
mwa mawaziri wakuu wastaafu wanaotarajiwa kuwamo ni pamoja na Jaji
Joseph Warioba, ambaye juzi aliwasilisha bungeni hapo Rasimu ya Katiba
kwa kutoa hotuba iliyoliteka Bunge kwa jinsi alivyofafanua mambo mengi
yenye utata kuhusu muundo wa Muungano. Mawaziri wakuu
wengine ni Cleopa Msuya, John Malecela, Dk Salim Ahmed Salim, Frederick
Sumaye pamoja na Edward Lowassa na Mizengo Pinda ambao ni wajumbe wa
bunge hilo. Wengine walioalikwa ni mabalozi wa nchi
mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, viongozi wa dini,
vyama vya wafanyakazi, vyama vya siasa, wafugaji, wakulima, wavuvi na
wawakilishi wa sekta binafsi. Katibu wa Bunge Maalumu la
Katiba, Yahaya Khamis Hamad aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa
Rais Kikwete atahutubia Bunge hilo kwa mujibu wa Kanuni ya 75 (1). Rais
Kikwete atapokewa katika Viwanja vya Bunge na Mwenyekiti wa Bunge
Maalumu la Katiba, Samuel Sitta na baadaye kukagua gwaride maalumu kabla
ya kuhutubia Bunge kuanzia saa 10:00 jioni. Kwa mujibu wa
ratiba iliyotolewa jana, baada ya Rais kuhutubia saa 11:35 jioni,
aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa bunge hilo, Pandu Ameir Kificho atatoa
neno la shukurani kabla ya Rais kupiga picha za kumbukumbu na wajumbe wa
Bunge hilo. Suala la hotuba ya Rais Kikwete limekuwa sehemu
ya mjadala katika Bunge hilo kutokana na baadhi ya wajumbe kuhoji
sababu za Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu kabla ya Rais kuzindua Bunge
kwa mujibu wa kanuni. Mjadala huo uliwafanya baadhi ya
wajumbe kumzuia Jaji Warioba Jumatatu iliyopita kuwasilisha rasimu hiyo
kama ilivyokuwa imepangwa hadi kilipofanyika kikao cha maridhiano siku
hiyohiyo usiku na kufikia mwafaka kwamba Mwenyekiti huyo wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba awasilishe Rasimu juzi na Rais ahutubie LEO.
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia