Chama kipya cha siasa cha Alliance for Change and Transparency
(ACT-Tanzania) kimeanzishwa na kupewa usajili wa muda huku kikitamba
kuwa mbadala wa vyama vyote vilivyopo sasa kwa maelezo kuwa vimekosa
demokrasia ya kweli.
Miongoni mwa viongozi wa muda wa chama hicho ni
Samson Mwigamba aliyetimuliwa uanachama wa Chadema kutokana na
kuhusishwa na waraka uliotaka kumwandaa Zitto Kabwe kuwania uenyekiti wa
chama hicho.
Mwigamba aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, alitimuliwa
pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo, huku
uanachama wa Zitto aliyevuliwa nyadhifa zake zote zikiwamo za Naibu
Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, ukisubiri kesi
aliyofungua mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari , Mwigamba
alisema mchakato wa kuandikisha wanachama mikoani kwa ajili ya kuomba
usajili wa kudumu kwa mujibu wa sheria umeshakamilika.
Alisema kimepata wanachama katika mikoa yote ya
Tanzania Bara na Zanzibar. Hata hivyo, alisema kimechagua mikoa 10
ambayo Msajili wa Vyama vya Siasa atakwenda kuhakiki kama sheria
inavyoeleza kabla ya kupewa usajili wa kudumu.
“Kama tutafanikiwa kupata usajili wa kudumu
mapema, tunatarajia kushiriki kwa nguvu zote katika chaguzi zote ndogo
zitakazojitokeza, uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu
mwakani,” alisema Mwigamba.
Alisema bendera ya chama hicho itakuwa na rangi ya
zambarau inayoashiria haki, heshima na uadilifu na rangi nyeupe
inayonyesha uwazi na usafi.
“Katikati ya bendera inayozungukwa na rangi
zambarau kuna nyota mfano wa chama kinachojitokeza katikati ya vyama
vingi inayokuja kutatua matatizo ya wanyonge yaliyowakabili kwa kipindi
kirefu,” alisema Mwigamba na kuongeza:
“Pembeni mwa bendera hiyo kuna misitari ya rangi
ya dhahabu inayoonyesha rasilimali zetu, rangi nyeusi zinazoashiria sisi
ni Waafirika.”
Alisema hivi sasa hakuna kiingilio katika kujiunga
na chama hicho na kwamba mara baada ya kupatikana kwa katiba, ndipo
suala hilo litakaposhughulikiwa sambamba na kiingilio.
Mwenyekiti wa chama hicho, Kadawi Limbu alisema
ACT - Tanzania kinaamini katika demokrasia jamii na kina shabaha kuu ya
kupigania na kusimamia mabadiliko na uwazi ambayo ni lazima jamii
inufaike nayo.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia