JESHI
la polisi mkoani Kilimanjaro, kikosi cha kutuliza ghasia (FFU)kimefanikiwa
kuzima maandamano makubwa ya Wanafuzni ya Shule ya Sekondari Lyamungo, iliyoko
wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, uliokuwa ukielekea kwa Mkuu wa mkoa huo,
Leonidas Gama.
Maandamano
hayo yaliyotokana na kile kilichodaiwa kuwa ni baadhi ya wanafunzi kutoridhishwa
na ratiba ya chakula shuleni hapo, yalilenga kufikisha ujumbe katika ofisi ya
mkuu wa Mkoa, zilizoko mjini Moshi, kilomita zaidi ya 21 kutoka shuleni hapo.
Taarifa
zilizothibitishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani hapo, Robert Boaz zinasema
kuwa wanafunzi hao walianza chokochoko hizo juzi jioni baada ya ratiba ya
chakula iliyokuwa ikionesha kuwa walitakiwa kula wali kubadilishwa ghafla na
uongozi wa Shule bila ya kutoa taariofa kwa serikali ya wanafunzi.
Kamanda
Boaz amesema wakiwa wameshafika eneo la njia panda Umbwe, maandamano hayo
yalizuiwa na kikosi cha kukabiliana na ghasia (FFU) lakini akaendelea
kusisitiza kuwa taarifa zilizotapakaa mitaani kuwa kulikuwa na hali ya
kushambuliana kati ya FFU na Wanafunzi hao sio za kweli.
“Hakuna
makabiliano, jeshi la polisi kikosiu cha FFU hakijafanya mashambulizi yoyote
kama inavyodaiawa, kilichotokea pale ni kwamba baada ya kufika njia panda Umbwe,
tulifanikiwa kuwahi na kuwazuia, hatuwezi kuruhusu watu kuandamana bila kufuata
taratibu,” alisema Boaz.
Kamanda
Boaz alisema kuwa taarifa kamili zitatolewa baadae ambapo ameongeza kuwa tayari
uongozi wa wilaya, wakiwemo Afisa elimu sekondari na Mkurugenzi wa Halmashauri
wameshafika shuleni hapo kuzungumza na Wanafunbzi hao kujua kiini cha
maandamano hayo ni nini.
Kwa
upande wake Mkuu wa wilaya ya Hai, Novatus Makunga, amesema kuwa lengo la
maandamano yanawezekana hayakuwa mabaya lakinii utaratibu uliotumika sio sahihi.
“Ni
kweli kulikuwa na maandamano ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Lyamungo,
inawezekana walikuwa na nia njema tu, lakini naendelea kusisitiza kuwa
utaratibu waliouchukua sio sahihi kisheria, hapa tunavyoongea hakuna taarifa au
malalamiko yoyote yaliyofikishwa ofisini kwangu,” alisema Makunga.
Taarifa
zilizopatikana na kuthibitishwa na uongozi wa wilaya ya hai kuwa hiyo sio mara
ya kwanza kuwepo kwa tatizo kama hilo kwani Aprili mwaka huu wanafunzi
waliripotiwa kugoma baada ya kutokukubaliana na mabadiliko ya ratiba ya chakula
shuleni hapo.