Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, kimesema mtuhumiwa
Mashusha Matata hadi sasa ameshatoa kete 82 za dawa ya kulevya aina
cocaine zenye thamani Sh83.6 milioni.
Matata alikamatwa Machi 17 mwaka huu, saa 8 mchana
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akitoka
Brazil. Alitua na Ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.
Akizungumza jana, Kamanda wa kitengo hicho, Godfrey Nzowa alisema awali mtuhumiwa alitoa kete 21 kwa njia ya haja kubwa.
Kamanda Nzowa alisema Matata alitoa kete hizo kwa awamu tatu, kwanza kete 30, baadaye 31 na siku iliyofuata alitoa kete 21.
Alisema mtuhumiwa huyo akiwa na hati ya kusafiria
yenye namba AB362172 mali ya Tanzania, alitiliwa shaka na askari polisi
hivyo kumtia nguvuni.
“Aliposhuka uwanja wa ndege tulimshuku huenda
akawa amebeba dawa za kulevya. Tuliamua kumhoji kabla ya kuja kukubali
saa moja baadaye,” alisema Nzowa.
Kamanda Nzowa alisema bado wanaendelea na
upelelezi na kwamba hatua hiyo itakapokamilika, atasomewa mashtaka
Mahakama Kuu kwa vile thamani ya dawa hizo ni kubwa na mtumhumiwa bado
anaendelea kuzitoa.