RAIS SAMIA AWATAKA WANA- ARUSHA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UTALII WA MIKUTANO NA AFCON 2027

 



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa Arusha kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na utalii wa mikutano pamoja na maandalizi ya Michuano ya Soka ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, itakayofanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda.


Akizungumza na wananchi wa Ngaramtoni, Wilaya ya Arumeru, Mkoani Arusha leo Novemba 19, 2026, mara baada ya kuwasili nchini akitokea Uganda, Rais Samia amesema Arusha imeendelea kuwa kitovu cha mikutano na utalii, hali inayoweka fursa kubwa kwa wananchi kujipanga kunufaika na wageni watakaofika mkoani humo.


Amesema ujio wa wageni kutokana na mikutano ya kimataifa pamoja na AFCON 2027 utachochea shughuli za kiuchumi, zikiwemo biashara, huduma za hoteli, usafiri, uongozaji watalii na sekta nyingine, akiwataka wananchi kutumia fursa hizo kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.





Aidha Rais Samia amesisitiza umuhimu wa wananchi kulinda amani na utulivu, akieleza kuwa usalama wa nchi na maeneo husika ni msingi wa kuvutia wageni, huku akiwataka pia wananchi na viongozi kuhakikisha miji inakuwa safi ili wageni wanaotembelea Tanzania waondoke na taswira nzuri ya nchi.


Aidha, Rais Samia amewaahidi wananchi kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo itakayowanufaisha wananchi na wageni, huku akieleza kuwa Serikali imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 500 kwa ajili ya miradi ya maji na kuagiza mamlaka za maji kuhakikisha wananchi wanaoishi maeneo yenye vyanzo vya maji wanapewa kipaumbele katika upatikanaji wa huduma hiyo.


Rais Samia kadhalika amewashukuru wananchi wa Arusha kwa upendo na mapokezi makubwa waliyompa, akieleza kuwa amewasili mkoani hapa kwa ajili ya kufungua Mkutano wa Mwaka wa Jeshi la Polisi Tanzania utakaofanyika Moshi, Kilimanjaro, pamoja na kutunuku Kamisheni kwa Maafisa wanafunzi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Chuo cha Kijeshi Monduli, Mkoani Arusha, Jumamosi.




About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia