TANAPA YABAINISHA MIKAKATI YA KUIMARISHA UHIFADHI NA KUKUZA UTALII NCHINI
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, kuongeza idadi ya watalii na kukuza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa taifa, huku likipanua fursa za kiuchumi kwa wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka hifadhi.
Akizungumza Novemba 10, 2026, katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamishna Mwishawa alisema maboresho ya miundombinu ya usafiri, ikiwemo ujenzi wa viwanja vinne vya ndege katika hifadhi za Nyerere, Mikumi na Ruaha, pamoja na uwekezaji katika reli ya kisasa ya SGR na barabara, yameongeza urahisi wa kufikika kwa hifadhi na kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi.
Alisema TANAPA pia imeimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika shughuli za doria, ufuatiliaji wa wanyamapori na kudhibiti ujangili. Aidha, wananchi wamepewa nafasi ya kushiriki katika ulinzi wa rasilimali hizo kwa kutoa taarifa za matukio yanayohusisha wanyamapori wakali na waharibifu kupitia namba maalumu za mawasiliano zilizowekwa katika kanda mbalimbali za shirika hilo.
Katika kuhakikisha jamii zinazozunguka hifadhi zinanufaika na uhifadhi, TANAPA inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayojumuisha ujenzi wa shule, mabweni, zahanati na vituo vya polisi, pamoja na uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa ya maji.
Miradi mingine ni pamoja na kuanzisha viwanda vidogo vya kukamua mafuta ya alizeti na kusindika asali, pamoja na kuwawezesha wananchi kupitia benki za jamii (COCOBA) zinazowapatia mikopo kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Kamishna huyo, uwezeshaji huo unalenga kuongeza ajira, kipato na fursa za biashara kwa wananchi, hatua inayochangia kuimarisha ushiriki wa jamii katika shughuli za uhifadhi.
Katika kupanua wigo wa utalii, TANAPA imewekeza pia katika uwanja wa gofu uliopo Fort Ikoma, pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ukiwa na lengo la kuunganisha utalii wa wanyamapori na michezo. Uwekezaji huo unatarajiwa kuvutia watalii na wapenzi wa mchezo wa gofu kutoka masoko ya kimataifa, kuongeza fursa za uwekezaji na kuitangaza Tanzania katika utalii wa michezo.
Sambamba na hilo, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kuweka mkazo katika kukuza utalii Kusini na Magharibi mwa Tanzania kwa kuvutia uwekezaji katika hifadhi za Nyerere, Ruaha, Kitulo, Katavi, Gombe, Milima ya Mahale, Udzungwa na Rubondo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Aidha, TANAPA kwa kushirikiana na wadau wa utalii imepanga kuandaa vifurushi maalumu vya utalii vinavyohusishwa na mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), vitakavyowawezesha mashabiki wa soka wanaotembelea Tanzania kupata fursa ya kutembelea hifadhi za Serengeti, Nyerere, Saadani, Mikumi, Tarangire, Arusha na Manyara.
Mkakati huo unalenga kuwapa mashabiki hao fursa ya kutembelea vivutio vya utalii katika siku ambazo hawatakuwa wakishuhudia mechi, huku ukitarajiwa kuongeza idadi ya watalii na mapato ya taifa.
Mikakati mingine iliyotajwa ni ujenzi wa barabara ya kilomita 6.69 kwa kiwango cha lami kutoka lango kuu la Hifadhi ya Taifa ya Manyara hadi Minjingu, pamoja na kuanzisha utalii wa majini katika Ziwa Victoria utakaounganisha maeneo ya Ghuba ya Speke ndani ya Serengeti, Kisiwa cha Saanane, Kisiwa cha Rubondo na Burigi-Chato.
Akizungumzia mwenendo wa utalii katika mwaka wa fedha 2025/2026, Kamishna Mwishawa alisema TANAPA imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha ushindani wa hifadhi za taifa katika soko la kimataifa, kukuza utalii wa ndani, kuboresha huduma na kupanua wigo wa uwekezaji.
Alisema hatua hizo zinalenga kuongeza mapato ya taifa na mchango wa sekta ya utalii katika upatikanaji wa fedha za kigeni.
Aidha, amewataka wahariri na waandishi wa habari kuwa washirika muhimu katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi na mchango wake katika maendeleo ya taifa, huku akiwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali za hifadhi, kutoa taarifa za vitendo vinavyohatarisha maliasili na kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na utalii kujiongezea kipato.



0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia