DC NKURLU - AAGIZA TANESCO NA DAWASA KUFIKISHA HUDUMA MISUGUSUGU IFIKAPO DISEMBA
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Fadhil Nkurlu, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam na Pwani (DAWASA) kuhakikisha huduma za maji na umeme zinawafikia wananchi wa Mtaa wa Saeni na Karabaka, Kata ya Misugusugu, ifikapo Desemba mwaka huu.
Nkurlu ametoa agizo hilo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Misugusugu, ambapo alipokea na kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa eneo hilo.
Amesema kwa kuwa Kibaha ni Manispaa, wananchi hawapaswi kuendelea kukosa huduma muhimu za maji na umeme, hivyo amezitaka taasisi hizo kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi kabla ya mwisho wa Desemba.
Kwa upande wao, wawakilishi wa TANESCO na DAWASA wamemhakikishia Mkuu huyo wa Wilaya kuwa ifikapo Desemba wananchi wataanza kupata huduma hizo, wakieleza kuwa miundombinu tayari imewekwa na kilichobaki ni hatua chache za ukamilishaji, huku fedha za utekelezaji zikiwa zimepatikana.
Katika mkutano huo, wananchi pia wameibua kero ya uchafuzi wa mazingira unaotokana na baadhi ya viwanda, hususan utiririshaji wa maji machafu katika makazi ya watu.
Akijibu hoja hiyo, Nkurlu amesema ofisi yake iko katika hatua za kuwaita wamiliki wa viwanda kwa kikao cha pamoja ili kutafuta suluhisho la kudumu.
Aidha, kuhusu ujenzi wa kituo cha polisi na soko, amewataka wananchi kushirikiana kutafuta maeneo yanayofaa, huku akiahidi kuchangia ujenzi wa kituo cha polisi mara wananchi watakapoanza utekelezaji. Diwani wa Viti Maalum, Sarah Uledi, amemshukuru kwa kufika kusikiliza kero zao, akisema mkutano huo umesaidia kutoa ufafanuzi kuhusu changamoto zilizodumu kwa muda mrefu, hususan maji na umeme.




0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia