Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) yajivunia Mafanikio


Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imesema imepokea zaidi ya mashauri 350 yanayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, huku takribani mashauri 200 yakiwa tayari yamefanyiwa maamuzi.

Mafanikio hayo yametajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa haki na ulinzi wa haki za msingi za wananchi katika bara la Afrika, licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili taasisi hiyo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo ya miaka 20 Jijini Arusha, Rais mstaafu wa mahakama hiyo, Jaji Imani Aboud, amesema taasisi hiyo imeendelea kupiga hatua katika kupokea na kushughulikia mashauri yanayowasilishwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika, hali inayoonesha umuhimu wake katika mifumo ya utoaji haki barani humo.

Amesema “Mahakama hii ilipoanza kazi ilikuwa na nchi 12 zilizokubali kutambua mamlaka yake kupitia matamko maalumu yaliyowezesha wananchi na taasisi zisizo za kiserikali kuwasilisha mashauri moja kwa moja mahakamani hapo”.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi nne za Afrika zilizoondoa utaratibu huo, nyingine zikiwa Rwanda, Tunisia na Ivory Coast, hatua inayopunguza fursa za wananchi kutumia mahakama hiyo kutafuta haki katika ngazi ya bara.

Kwa upande wake Wakili Bahame Tom Nyanduga kutoka Tanzania, amesema changamoto za upungufu wa rasilimali watu na fedha ni miongoni mwa vikwazo vinavyoweza kudhoofisha uwezo wa mahakama hiyo kutekeleza majukumu yake ya kulinda haki za binadamu barani Afrika.

Nyanduga amesema licha ya taasisi hiyo kufanikiwa kuwepo kwa kipindi hicho, bado inahitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa nchi wanachama ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano hadi kumi ya mwanzo wa uendeshaji wa mahakama hiyo, kati ya nchi 34 zilizokuwa zimeridhia mkataba wake, ni nchi 10 pekee zilizokuwa zimekubali wananchi wake kuwasilisha mashauri moja kwa moja mahakamani hapo.

Ameongeza kuwa hali hiyo ilikuwa changamoto kubwa ikizingatiwa kuwa bara la Afrika lina nchi 55, hivyo ushiriki mdogo wa nchi wanachama katika kuruhusu wananchi kutumia mahakama hiyo uliathiri wigo wa upatikanaji wa haki.

“Msingi wa kuanzishwa kwa mahakama hii ulikuwa ni kuhakikisha wananchi wa Afrika wanapata fursa ya kutafuta haki katika ngazi ya bara pale wanaposhindwa kupata suluhisho kupitia mifumo ya mahakama za ndani ya nchi zao” amesema.

Akifungua maadhimisho hayo, Rais wa mahakama hiyo, Jaji Blaise Tchikaya, amesema anaamini taasisi hiyo itaendelea kukua na kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio katika miaka ijayo.

“Ni dhahiri kuwa kongamano hili ni fursa kwa majaji, wataalamu wa sheria, viongozi wa taasisi na wadau wengine kutathmini mafanikio yaliyopatikana, kujadili changamoto na kuweka mikakati mipya ya kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu barani Afrika” amesema Jaji Tchikaya.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia