NABII MKUU PROF. GEORDAVIE AAHIDI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KATIKA KILA JAMBO
Na Woinde Shizza, Kisongo - Arusha
Nabii Mkuu Prof. GeorDavie ameahidi kushirikiana na viongozi mbalimbali wa Serikali, huku akitoa ahadi ya kuendelea kushirikiana na Serikali katika kila jambo litakalolenga maendeleo na ustawi wa jamii.
Ahadi hiyo ameitoa leo Jumapili, Novemba 1, 2026, katika Ibada Maalum iliyofanyika katika kanisa la ngurumo ya upako(chuo kikuu cha manabii), Kisongo, Arusha, mbele ya maelfu ya waumini kutoka ndani na nje ya nchi.
Nabii Mkuu ameyasema hayo baada ya kupokea salamu za Rais na pongezi kutoka kwa viongozi wa Serikali waliohudhuria ibada hiyo, amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Rugangira, kwa nidhamu aliyoonyesha kwa watumishi wa Mungu na kumuombea apandishwe cheo zaidi.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Rugangira, ametuma salamu nyingi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kutambua kazi kubwa inayofanywa na Nabii Mkuu ambayo amesema imevuka mipaka hadi kuchangia Sekta ya Utalii.
"Kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, tunatambua kazi kubwa anayofanya Nabii Mkuu, kazi yake imevuka mipaka mpaka kwenye Utalii, maana wageni wengi wanakuja nchini kwa ajili ya ibada zake," alisema Rugangira.
Rugangira pia ametoa wito kwa kanisa kushirikiana na Serikali kusafisha Wilaya ya Arumeru, kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambavyo vimezidi, pamoja na kushirikiana kutangaza AFCON na Utalii.
Kwa upande wake, Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumai, ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kusamehe madeni ya taasisi za dini na kupunguza kodi za mashirika ya dini, hatua iliyoleta faraja kwa wananchi.
"Nampongeza Nabii Mkuu kwa kazi kubwa anayofanya hapa nchini na duniani ,hakuna kitu muhimu kama amani, naomba uendelee kutangaza amani, kuiombea nchi yetu na kumuombea Rais wetu aendelee kuwa na afya njema," alisema Dkt. Lukumai.
Akiongea kwa niaba ya Rais wa Umoja wa Makanisa ya Kitume na Kinabii, Dkt. Pro Joshua, Mchungaji Filipo Msengi, amemuomba Nabii Mkuu kutangaza Novemba 1 ya kila mwaka kuwa siku ya hija kwa watoto wake wote wa kiroho aliowapaka mafuta ambapo watakuwa wakija Kisongo kumsalia Mungu na kutoa sadaka zao.
Ibada hiyo imehudhuriwa na wageni kutoka nchi mbalimbali duniani, zikiwemo Canada, New Zealand, Afrika Kusini, Chile, Bulgaria, Mexico, Marekani (Florida), Poland, Sweden, Denmark, Urusi, Uruguay, Argentina, Korea, Vietnam, Brazil na Uganda.


0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia