UN YASIFU AMANI TANZANIA, YASISITIZA UWEKEZAJI KTK UTALII, DIRA 2050
MRATIBU Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania, Susan Namondo, amesema amani ya Tanzania kwa miaka mingi imekuwa msingi muhimu wa maendeleo ya sekta ya utalii, akisema nchi inapaswa kuendelea kuilinda ili dunia iweze kunufaika na vivutio na hazina za asili zilizopo nchini.
Namondo amesema utalii una mchango mkubwa kwa uchumi wa Tanzania, lakini pia unaiwezesha dunia kunufaika na vivutio na rasilimali za kipekee zilizopo nchini.
Amesema serikali imeendelea kuweka mkazo katika maendeleo ya utalii, jambo linaloonekana kutokana na hatua iliyofikiwa na sekta hiyo, huku akieleza kuwa juhudi hizo zinaendana na ajenda pana ya maendeleo ya Tanzania.
Amepongeza pia msisitizo wa Serikali katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisema ni nyaraka muhimu inayoweka msingi wa mwelekeo wa maendeleo ya nchi kwa miaka ijayo.
Kwa mujibu wa Namondo, miongoni mwa changamoto kubwa zinazopaswa kupewa kipaumbele ni kuwawezesha vijana kupata fursa za kiuchumi, kuongeza tija katika kilimo na kuhakikisha vijana wanashiriki kikamilifu katika sekta hiyo pamoja na huduma za kijamii.
Amesema Umoja wa Mataifa na washirika wengine wa maendeleo wako tayari kuendelea kuunga mkono jitihada za Tanzania katika kutekeleza Dira ya Taifa 2050 na ajenda zake za maendeleo.
Akizungumzia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Namondo amesema kiwango cha utekelezaji duniani bado hakiridhishi, akibainisha kuwa kwa sasa ni takribani asilimia 36 tu ya malengo hayo yaliyo katika mwelekeo wa kufikiwa.
Amesema changamoto hiyo imechangiwa na matukio mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo mlipuko wa UVIKO-19, vita vya Ukraine na migogoro mingine inayoendelea duniani ambayo imeathiri uchumi na maendeleo ya nchi nyingi.
Hata hivyo, amesema changamoto hizo hazipaswi kuwa sababu ya kupunguza juhudi, kwa kuwa wananchi bado wanahitaji huduma bora na fursa za kiuchumi, hivyo serikali na wadau wa maendeleo wanapaswa kuongeza juhudi ili kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa.


0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia