NDEJEMBI: TEKNOLOJIA ITUMIKE KUONGEZA UFANISI WA UKUSANYAJI WA MAPATO
Na Mwandishi Wetu, Arusha
MAKAMU
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John
Ndejembi, amesema teknolojia inapaswa kuwa nyenzo muhimu katika kuongeza
ufanisi na usawa wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili nchi ziweze
kufadhili shughuli na vipaumbele vya maendeleo kupitia rasilimali zake.
Makamu
wa Rais ameyasema hayo leo, Oktoba 6, 2026, wakati akimwakilisha Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,
katika ufunguzi wa Mkutano wa 46 wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa
Jumuiya ya Madola (CATA), unaofanyika katika Ukumbi wa Gran Melia,
jijini Arusha.
Amesema mfumo mzuri wa kodi unapaswa kuwa wa
uhakika, kuwezesha biashara halali, kuhimiza uwekezaji na urasimishaji
wa shughuli za kiuchumi, sambamba na kuwezesha sekta binafsi kutumia
nafasi yake katika kuchagiza mabadiliko ya kiuchumi kama ilivyokusudiwa
chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
“Ukusanyaji wa kodi haupaswi kuzuia shughuli za kiuchumi zenye tija, bali unapaswa kuunga mkono shughuli hizo,” amesema.
Makamu
wa Rais amesema ukuaji endelevu wa mapato unapaswa kutokana na ukuaji
wa uchumi, urasimishaji wa shughuli za kiuchumi, kuongeza wigo wa walipa
kodi, kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari, matumizi bora ya data na
teknolojia, pamoja na kuwa na mfumo wa kodi unaokua sambamba na uchumi.
Aidha,
amesema ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi unapaswa kutoa
matokeo ya vitendo, huku akieleza kuwa mabaraza kama CATA yanapaswa
kusaidia katika kupima utendaji, kubadilishana taarifa, kuimarisha
usaidizi wa kiutawala, kujifunza kutoka kwenye mifumo inayofanya vizuri
na kutafsiri uzoefu wa kimataifa kuwa mageuzi ya ndani yanayoweza
kupimika.
Amesema Tanzania inatambua umuhimu wa ushirikiano wa
kikodi baina ya mataifa na inaendelea kuimarisha ushiriki wake katika
mifumo ya kimataifa, ikiwemo kubadilishana taarifa za kodi na usaidizi
wa masuala ya kiutawala baina ya nchi.
Kwa mujibu wa Makamu wa
Rais, Julai 2026, Tanzania ilitajwa kimataifa kuwa inatimiza vigezo vya
kimataifa katika ulipaji kodi pamoja na viwango vya uwazi na
ubadilishanaji wa taarifa pale zinapohitajika.
Amesema hatua hiyo
ni faraja ya maendeleo, lakini pia ni ukumbusho kwamba viwango vya
kimataifa vinaendelea kubadilika, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea
kuboresha mifumo ya kisheria na uwezo wa kitaasisi.
Makamu wa
Rais amesema Rais Samia amekuwa akisisitiza matumizi ya teknolojia,
usawa, ushiriki wa walipa kodi na utoaji wa huduma bora katika usimamizi
wa mapato.
Amesema matarajio ya Serikali ni kuwa na mifumo ya
kisasa itakayopunguza mwingiliano usio wa lazima, kuongeza uwazi,
kusaidia utekelezaji unaozingatia hatari na kuwawezesha walipa kodi
wanaofuata sheria kutimiza wajibu wao kwa urahisi.
Akizungumzia
kaulimbiu ya mkutano huo, “Kutumia Teknolojia kwa Ukusanyaji Bora wa
Mapato” (Leveraging Technology for Efficient Revenue Collection), Makamu
wa Rais amesema teknolojia inapaswa kuwezesha Serikali kurahisisha
ulipaji kodi kwa hiari, kuwatambua wale wasiokidhi wajibu wao wa kodi,
kupunguza gharama za kiutawala, kuboresha huduma kwa walipa kodi na
kuwezesha biashara halali.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA), Dkt. Abu Tariq Jamaluddin, amesema CATA ni jumuiya ya viongozi na wataalamu wa masuala ya kodi wanaojifunza kutoka kwa kila mmoja na kukua pamoja.
Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, CATA imeendelea kuimarisha jumuiya hiyo kupitia programu za uongozi, mipango na teknolojia, pamoja na mijadala inayofanyika kwa njia ya mtandao kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu.
Awali, Kiongozi mwenyeji wa mkutano huo ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), CPA Yusuph Mwenda, amemshukuru Rais Samia kwa uongozi wake katika kuimarisha mabadiliko ya kidijitali yanayowezesha ukusanyaji wa kodi kwa urahisi na ufanisi.
Amesema Serikali imewekeza katika mifumo kadhaa ya kisasa, ikiwemo Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya Ndani (IDRAS), wenye jumla ya moduli 17.
Amesema miongoni mwa moduli hizo ni mfumo wa utoaji ankara za kielektroniki, ambao sasa unawawezesha walipa kodi kutoa ankara hizo bila kulazimika kutumia mashine halisi.
Mkutano huo unawakutanisha zaidi ya wataalamu na viongozi 400 kutoka nchi 48 za Jumuiya ya Madola, ukiwa na lengo la kubadilishana maarifa na uzoefu katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa kodi kwa kutumia teknolojia za kisasa.


.jpeg)







0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia