TEKNOLOJIA YA AI KUBAINI MAGONJWA KUPITIA SAUTI YA KIKOHOZI YABUNIWA NA AGA KHAN

Na Mwandishi Wetu
CHUO
Kikuu cha Aga Khan kimekuja na Kikohozi Classifier, teknolojia
inayotumia akili bandia (AI) kuchanganua sauti za kikohozi kwa lengo la
kusaidia kubaini magonjwa ya mfumo wa upumuaji, ikiwamo Kifua Kikuu
(TB), pumu na magonjwa sugu ya mapafu (COPD).
Akizungumza kuhusu
ubunifu huo, Msimamizi wa Mradi na Profesa Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha
Aga Khan, Dkt. Kahabi Isangula, amesema teknolojia hiyo imetengenezwa
nchini Tanzania kwa lengo la kuwezesha uchunguzi wa magonjwa hayo
kufanyika kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu.
Amesema mfumo
huo unalenga kutengeneza kifaa kisichohitaji kuingizwa ndani ya mwili
wa mgonjwa na ambacho kinaweza kutumika katika vituo vya afya vya ngazi
za chini na maeneo ya jamii, hivyo kuongeza fursa ya wananchi kupata
huduma za uchunguzi.

Kwa
mujibu wa Dkt. Isangula, watafiti wanatarajia kukusanya na kurekodi
sauti za kikohozi za watu 30,000 kwa kutumia simu janja na vifaa maalumu
vya kurekodia. Taarifa hizo zitatumika kujenga kanzidata kubwa ya sauti
za kikohozi ambayo itasaidia katika uundaji wa mfumo wa AI.
Amesema
mfumo huo utachanganua sifa mbalimbali zinazopatikana katika sauti ya
kikohozi na kuzihusianisha na viashiria vinavyoweza kuonyesha uwepo wa
TB, pumu au COPD, hatua inayotarajiwa kusaidia wataalamu wa afya katika
mchakato wa uchunguzi.
Utekelezaji unafanyika kwa ushirikiano na
Maabara ya Teknolojia Chipukizi za Afya (Emerging Technologies for
Health) ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)
pamoja na Chuo Kikuu cha Warwick cha Uingereza, kwa ufadhili wa UK
Research and Innovation (UKRI) kupitia Medical Research Council (MRC).
Dkt.
Isangula amesema mpango huo umepitishwa na Wizara ya Afya pamoja na
Programu ya Taifa ya Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, huku shughuli za
utafiti zikifanyika katika maeneo ya Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga,
Iringa na Kilimanjaro.
Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa
utafiti na uchambuzi wa taarifa, hatua inayofuata ni kutengeneza
programu ya simu janja, Kikohozi App, itakayounganishwa na mfumo wa AI
na kufanyiwa majaribio kabla ya kuanza kutumika kwa upana.
Kwa
upande wake, Mtafiti Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan na Shule ya
Uuguzi na Ukunga Kanda ya Afrika Mashariki (SONAM EA), Devotha Kibanga,
amesema ukusanyaji wa sauti unahusisha wagonjwa wapya ambao hawajaanza
kutumia dawa au walioanza matibabu ndani ya kipindi kisichozidi miezi
mitatu.
Amesema wakati wa zoezi hilo, mgonjwa huombwa kukohoa huku sauti ikirekodiwa kwa simu janja.
Taratibu za usalama huzingatiwa, ikiwa ni pamoja na matumizi ya barakoa na usafishaji wa vifaa kwa sanitaiza baada ya zoezi.
Ukusanyaji
wa sauti hizo ulianza Machi mwaka huu na unatarajiwa kuendelea hadi
Septemba 2027, wakati mradi mzima ukitarajiwa kukamilika mwaka 2028.
Katika kipindi hicho, watafiti wataendelea kukusanya na kuchambua
taarifa pamoja na kuendeleza mfumo huo kwa ajili ya matumizi
yanayokusudiwa.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia