MADIWANI SIMANJIRO KUFUATILIA MAPATO YA MADINI

 Na Mwandishi Wetu, Simanjiro


MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, wameazimia kufuatilia kwa karibu mapato yatokanayo na shughuli za uchimbaji wa madini ili kuhakikisha yanachangia ipasavyo maendeleo ya wilaya hiyo.

Azimio hilo limefikiwa katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika makao makuu ya wilaya hiyo, yaliyopo Orkesumet.

Katika kikao hicho, madiwani wamemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuiwezesha Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kukutana na Afisa Madini Mkazi wa Mirerani (RMO), George Kaseza, kwa lengo la kupata taarifa sahihi kuhusu mapato yatokanayo na madini ya graphite na madini mengine.

Diwani wa Kata ya Ngorika, Albert Msole, amesema kuwa mbali na kufuatilia mapato hayo, madiwani wanataka kuhakikisha kampuni za uchimbaji madini zinatimiza wajibu wao wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) kwa kuchangia shughuli za maendeleo katika wilaya hiyo.

Msole amesisitiza kuwa kampuni zinazoshindwa kutekeleza wajibu huo zinapaswa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazotawala sekta ya madini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Kaleya Melita Mollel, amesema suala la uwajibikaji kwa jamii kwa kampuni za uchimbaji madini linapaswa kupewa kipaumbele ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zilizopo katika maeneo yao.

"Tutakwenda kwa RMO Mirerani na kupatiwa taarifa sahihi za mapato yatokanayo na graphite na madini mengine ili kufuatilia uwajibikaji kwa jamii kwa wachimbaji," amesema Mollel.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia