TANZANIA YAGEUKA KITOVU CHA HUDUMA ZA KIBINGWA ZA AFYA KWA MATAIFA JIRANI
Na Woinde Shizza,Arusha
Tanzania imeendelea kupiga hatua katika sekta ya afya, hali inayoiwezesha nchi kutoa huduma mbalimbali za kibingwa na kuvutia wagonjwa kutoka mataifa jirani wanaofika nchini kwa ajili ya matibabu.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 100 ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, yaliyofanyika jijini Arusha, akieleza kuwa maendeleo hayo yanaashiria mabadiliko makubwa katika uwezo wa nchi kutoa huduma za afya.
Amesema kuwa tofauti na miaka ya nyuma ambapo Tanzania ililazimika kutegemea madaktari kutoka nje ya nchi kutoa baadhi ya huduma za kibingwa, kwa sasa nchi imejenga uwezo wa kutoa huduma hizo ndani ya mipaka yake na hata kuhudumia wagonjwa kutoka mataifa jirani.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na juhudi za Serikali katika kuimarisha mifumo ya afya, ikiwemo Bohari ya Dawa (MSD), inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa dawa pamoja na kuimarisha udhibiti wa ubora na usalama wa bidhaa za afya.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za awali barani Afrika kufikia Kiwango cha Ukomavu wa Tatu (Maturity Level 3) katika mfumo wa udhibiti wa dawa, kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA). Hatua hiyo imeiwezesha nchi kutoa uzoefu na mwongozo kwa mataifa mengine yanayolenga kufikia kiwango hicho.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika huduma za kibingwa na mafunzo ya madaktari bingwa nchini, hatua inayosaidia kupunguza gharama na ulazima wa wagonjwa kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.
Ametaja huduma za upasuaji wa moyo zinazotolewa jijini Dar es Salaam na upandikizaji wa figo unaofanyika Dodoma kuwa ni miongoni mwa huduma zilizokuwa zikiwafanya wagonjwa wengi kutafuta matibabu nje ya nchi, hususan India, lakini sasa zinapatikana ndani ya Tanzania.
Akizungumzia msingi wa maendeleo ya sekta ya afya nchini, Mchengerwa amekumbusha misingi ya Azimio la Arusha la mwaka 1967, akisisitiza umuhimu wa kumuweka mwananchi katika kiini cha mipango ya maendeleo ya taifa.
Pia, amerejea kampeni ya “Mtu ni Afya” ya mwaka 1973 iliyolenga kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa afya ya mazingira, matumizi ya vyoo bora na kuchemsha maji ya kunywa ili kujikinga na magonjwa.
Amesisitiza kuwa ujenzi na uimarishaji wa hospitali ni sehemu ya kutambua thamani ya maisha ya kila mwananchi bila kujali hali yake ya kiuchumi, akibainisha kuwa kila Mtanzania ana haki ya kuishi na kupata huduma za afya.
Katika kuhitimisha, Mchengerwa amehimiza Watanzania kuendelea kuthamini na kutumia huduma za afya zinazopatikana nchini, huku akisisitiza umuhimu wa kuunga mkono juhudi za kuimarisha sekta hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.















0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia