DC Monduli Amsimamisha Mwenyekiti wa Kijiji Kupisha Uchunguzi.

Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Gloriana Kimath, Novemba 18, 2026, amemsimamisha kazi Mwenyekiti wa Kijiji cha Mti mmoja, Ibrahim Leiyo, kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazohusiana na uongozi wake. Hatua hiyo imetangazwa katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero na changamoto za wananchi uliofanyika katika Kijiji cha Mti Mmoja, Kata ya Sepeko, Wilaya ya Monduli.


Katika mkutano huo, wananchi waliibua changamoto za migogoro ya ardhi na kutokuwa na imani na mwenyekiti wa kijiji, wakidai kuwa amekuwa chanzo cha migogoro hiyo kwa kutoshirikisha Serikali ya Kijiji katika maamuzi muhimu, kukwepa vikao na kufanya maamuzi kuhusu ardhi bila kufuata utaratibu unaotakiwa. Baadhi ya wananchi walisisitiza kuwa wanahitaji ardhi yao irejeshwe na kuwepo kwa uwazi katika usimamizi wake. Kufuatia kusimamishwa kwa Ibrahim Leiyo, Moitiko Jamaamabye ni mwenyekiti wa Kitongoji cha Sepeko ameteuliwa kukaimu nafasi ya mwenyekiti wa kijiji wakati taratibu za uchunguzi zikiendelea.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mgogoro wa ardhi, Afisa Ardhi Mteule, Waziri Juma, alisema Serikali inaendelea kupitia uhalali wa hati za ardhi zinazolalamikiwa na kuchukua hatua za kisheria zinazohitajika ili kuhakikisha ardhi hiyo inarejeshwa kwa wananchi endapo itathibitika kuwa kuna ukiukwaji wa taratibu. Alibainisha kuwa baadhi ya mashauri bado yanaendelea katika vyombo vya sheria, ikiwemo Baraza la Ardhi na Nyumba pamoja na Mahakama Kuu.

Kwa upande wa changamoto ya wanyamapori, wananchi walieleza hofu yao kutokana na tembo kuvamia maeneo yao na kuhatarisha usalama wao. Akijibu hoja hiyo, Afisa Wanyamapori, Natashoo Msuya, alisema gari litapatikana kuambatana na vijana na wananchi kwenda maeneo yenye changamoto ya tembo kwa ajili ya kuratibu hatua za kuwafukuza. Pia aliwataka wananchi kutoa taarifa za uwepo wa wanyamapori kwa Mtendaji wa Kijiji ili hatua zichukuliwe kwa haraka.

Kuhusu eneo la jeshi linalotumika kwa malisho ya mifugo, Mhe. Kimath alisema wananchi wataendelea kunufaika na eneo hilo kwa ajili ya malisho, isipokuwa wakati wa mazoezi ya kijeshi ambapo wanapaswa kuheshimu na kufuata utaratibu wa jeshi na si vinginevyo.

Katika mkutano huo, wananchi pia walieleza masuala mengine yanayohusu matumizi ya ardhi ya kijiji na mashauri yanayoendelea dhidi ya baadhi ya familia katika Baraza la Ardhi na Nyumba. Mkuu wa Wilaya aliwataka wananchi kutumia vikao na njia za kisheria kutatua tofauti zao badala ya kuendeleza migogoro isiyo na tija. Aidha, alielekeza Halmashauri kuhakikisha usafi wa mazingira unafanyika angalau mara moja kila mwezi kwa kushirikiana na wananchi ili kuzuia magonjwa ya mlipuko.

. Kimath alihitimisha kwa kuwataka wananchi wa mti mmoja na Sepeko kwa ujumla, kudumisha amani, umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa changamoto zilizopo zinapaswa kutatuliwa kwa kufuata sheria na taratibu za Serikali. Alieleza umuhimu wa wananchi na viongozi kushirikiana katika kujenga mazingira bora ya maendeleo na kuhakikisha migogoro haizuii utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya jamii.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia