BREAKING NEWS

Tuesday, March 4, 2014

TBL YAKABISHI CHUO KIKUU CHA KUMBUKUMBU YA STEFANO MOSHI MAJENGO KWA MKATABA

CHUO Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo) cha mkoani Kilimanjaro, kimekabidhiwa majengo ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa mkataba wa miaka mitano, lengo likiwa ni kuboresha maendeleo ya elimu nchini.
Hafla ya makabidhiano hayo ilishuhudiwa na Meneja wa TBL Kanda ya Kaskazini, Salvatory Rweyemamu na viongozi wengine wa chuo hicho, akiwemo Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Julius Mosi.
Akizungumza baada ya kuingia mkataba huo, Rweyemamu alisema hatua hiyo inatokana na kampuni hiyo kutambua umuhimu wa matumizi wa majengo hayo kwa chuo hicho kwa maendeleo ya elimu nchini.
Alisema TBL imeamua kuingia mkataba moja kwa moja na chuo hicho, ambao vilevile utahusisha punguzo la gharama za ukodishaji.
"Majengo haya tumekuwa tukiyatumia kama stoo ya kuhifadhia bia, hata hivyo kwa kutambua umuhimu wa matumizi ya majengo haya kwa uongozi wa chuo, tunayakabidhi majengo haya tukiwa tumedhamiria kupunguza gharama za ukodishaji pia," alisema Rweyemamu.
Alisema awali majengo hayo, yalikuwa yakimilikiwa na Kampuni ya Kilimanjaro Development Forum (KDF) na kwamba imeamua kuyakabidhi kwa chuo hicho pamoja na kupunguza gharama za kuyakodisha kwa mwezi kutoka Sh milioni 8.4 hadi Sh 100,000 pamoja na kusimamia gharama nyinginezo kama vile kodi ya viwanja.
"Tunafanya hivi kama mchango wetu TBL katika maendeleo ya elimu hapa nchini, lakini pia tunatarajia kusimamia gharama zozote zile, kama vile kodi ya kiwanja," alisema Rweyemamu.
Kwa upande wake, Katibu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Julius Mosi, alisema kitendo kilichooneshwa na TBL ni cha kiungwana, kizalendo na cha kuigwa na makampuni mengine makubwa ambayo yanaingiza faida kubwa kutokana na kodi za wananchi. Mkuu wa Chuo cha SMMUCo, Arnold Temu alisema chuo hicho kina wanafunzi zaidi ya 2,603 .
Alisema kwamba kuongezeka kwa wanafunzi mwaka hadi mwaka tangu chuo kianzishwe mwaka 2008, kumesababisha kuwe na haja ya kuongeza majengo.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates