Mkutano wa 16 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utafanyika Tarehe 30 Novemba, 2014 Nairobi, Kenya.
Kwa mujibu wa Mkakaba Mkutano huu utatanguliwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri la
Jumuiya
ya Afrika Mashariki utakaofanyika Tarehe 20 – 27 Novemba, 2014 katika
ngazi ya Wataalam, Makatibu Wakuu na Mawaziri. Aidha, katika Mkutano wa
Wakuu wa Nchi, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kukabidhiwa
uwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha mwaka mmoja na
Jamhuri ya Kenya inayomaliza kipindi chake, Ikiwa ni utekelezaji wa
Ibara ya 12 (2) ya Mkataba wa Uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumzia
Tanzania kuchukua Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Katibu Mkuu
wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Joyce Mapunjo alisema,
“Katika kipindi cha uenyekiti wake, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
itaendeleza mafanikio yaliyopatikana wakati wa kipindi cha uenyekiti wa
Jamhuri ya Kenya. Aidha, mkazo utawekwa katika kuhakikisha mtangamano wa
Afrika Mashariki unaendelezwa kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba wa
Uanzishwaji wa Jumuiya pamoja na Kanuni na Taratibu za Jumuiya. Aidha,
mkazo utawekwa katika kuhakikisha Sekta binafsi na Wadau wengine
wanashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa mtangamani wa Afrika
Mashariki ikiwa ni pamoja na kuzitumia fursa zitokanazo na Jumuiya ya
Afrika Mashariki,”
Mkutano
wa 16 wa Wakuu wa Nchi utatanguliwa na Mkutano wa tatu wa Kazi wa Wakuu
wa Nchi kuhusu uendelezaji wa miundombinu katika Jumuiya. Mkutano hu
utapokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo waliyoyatoa katika mkutano wa
pili uliofanyika mwezi Novemba, 2012 na kuidhinisha miradi 72 ya
miundombinu ya kipaumbele ya barabara, reli, nishati na bandari. Kwa
upande wa utekelezaji miradi 16 imekamilika, 39 utekelezaji unaendelea
na 17 ipo katika hatua za awali za kutafutiwa fedha kwa ajili ya
utekelezaji wake.
Kwa
upande wa Tanzania miradi nine imekamilika ambayo ni kuupatia mji wa
Kibondo umeme, mradi wa barabara ya Mbezi-Shule-Tangibovu-Makutano ya
Nelson Mandela na barabara ya Tabata. Barabara nyingine iliyokamilika ni
Nyangunge – Musoma-Airari. Shemu ya Simiyu-Musoma inayounganisha Kenya
na Tanzania ujenzi unaendelea.
Kwa
mujibu wa Agenda, Wakuu wa Nchi watapokea taarifa ya Baraza la Mawaziri
la Jumuiya kuhusu utekelezaji wa mtangamano wa Afrika Mashariki kwa
kipindi cha Novemba, 2013 – Novemba, 2014. Aidha, Wakuu wa Nchi
watajadili hatua iliyofikiwa katika majadiliano ya Sudan Kusini kujiunga
na Jumuiya ya Afrika Mashariki, maombi ya Jamhuri ya Somalia kujiunga
na Jumuiya ya Afrika Mashariki, suala la uchangiaji katika bajeti ya
Jumuiya na mapitio ya mfumo wa Kitaasisi wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Wakuu
wa Nchi watajadili pia hatua iliyofikiwa katika majadiliano ya
uanzishaji wa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki Ikiwa ni pamoja
na maandalizi ya Mpangokazi wa kuelekea katika Shirikisho pamoja na
mchakato wa kuiongezea mamlaka Mahakama ya Afrika Mashariki ili iweze
kushughulikia mashauri yanayohusu biashara, uwekezaji na utekelezaji wa
Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki.
Kumekuwepo
na mafanikio kupitia ushiriki wa Tanzani katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Tangu kuanza kwa Umoja wa Forofha wa Afrika Mashariki, mauzo
ya Tanzania katika Jumuiya ya Afrika yameongezeka kutoka Dola za
Marekani Milioni 142 mwaka 2005 hada kufikia Dola za Marekani Milioni
1,120 mwaka 2013. Bidhaa ambazo zimekuwa zikiuzwa kwa wingi ni pamoja na
nafaka, karatasi, mbole, vifaa vya umeme, mashine, bidhaa za mafuta na
vimiminika, vyandarua, bidhaa za plastiki, chai, na bidhaa za karatasi.
Bidhaa nyingine ni saruji, matunda, chuma, samaki, ngano, sukari na
nguo.
Kwa
upande wa uwekezaji, miradi iliyowekezwa hapa Nchini kutoka nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki imeongezeka kutoka miradi 35
yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 39.65 mwaka 2005 na kufikia
Miradi 244 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 676.45 mwaka 2013.
Miradi hii imezalisha jumla ya ajira 15,721 katika kipindi husika.
Katika
kuimarisha biashara na fursa za masoko ndani ya Jumuiya, Tanzania
imeanza utekelezaji wa mfumo wa Himaya ya Forodha ulioanza 1 Julai,
2014. Katika mfumo huu, uthamini wa bidhaa na ukusanyaji wa kodi
unafanyika katika Nchi mwanachama iliyoagiza bidhaa na baada ya
kuthibitisha kwamba kodi imelipwa bidhaa zinaondolewa kutoka bandari ya
Dar es salaam na kusafirishwa kwenda nchi husika mwanachama chini ya
usimamizi wa Mamlaka ya Forodha kwa kutumia mfumo wa Kieletroniki wa
Ufuatiliaji wa bidhaa. Aidha, bidhaa zilizolipiwa kodi katika Nchi
husika husafirishwa hazihitaji kuwekewa dhamana na hivyo kupunguza
gharama za kufanya biashara.
Kwa
upande wa uendelezaji wa Miundombinu Jumuiya imeandaa Mipango Kabambe ya
uendelezaji wa barabara na reli zinazounganisha Nchi Wanachama.
Utekelezaji wa mipango hiyo unaendelea na kwa upande wa Tanzania
umehusisha ujenzi wa barabara ya Arusha- Namanga-Athi river,
Arusha-Holili-Voi-Mwatate na Malindi-Lingalinga lunga/Tanga-Bagamoyo
zote zikiunganisha Tanzania na Kenya. Kwa upande wa mtandao
unaounganisha Tanzania, Burundi, Rwanda na Uganda ujenzi wa barabara
zinazoanzia Tunduma-Iringa/Sumbawanga na kuelekea nchi hizo jirani
umekamilika.
Ibara
ya 124 ya Mkataba inatambua kuwa amani na usalama ndiyo msingi wa
maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Nchi Wanachama zimeidhinisha na kutekeleza Mkakati wa kikanda wa Amani
na Usalama tangu mwaka 2006.
Katika
kukabiliana na changamoto za kiusalama katika Jumuiya Mkakata huu
umefanyiwa mapitio na kuongeza masuala ya Kukabiliana na Uharamia,
Kupambana na uhalifu wa kimtandao, Biashara Haramu ya Usafirishaji wa
Binadamu, Mauaji ya Kimbari na Usafishaji wa fedha haramu ambazo ndizo
zimekuwa zikitumika kufadhili uhalifu.
Aidha,
ili kushirikisha wadau zaidi katika kuimarisha usalama, Jumuiya
iliandaa kongamano la viongozi hao katika kuzuia kusambaza kwa waumini
wa itikadi kali za kidini na pia kuwashirikisha katika kufundisha
umuhimu wa imani yao ya dini na amani kwa waumini wao. Katika
kuhakikisha wanachi wanashirikishwa utaratibu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya
kukutana na Sekta binafsi, Asasi za kiraia na wadau wengine kwa ajili ya
mashauriano na kupata maoni yao juu ya uendeshaji wa Jumuiya.
Imetolewa na
Katibu Mkuu
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia