Zitto, Filikunjombe wadai waziri alitaka kuiba ripoti. |
Viongozi
wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na Deo Filikunjombe
wamemtuhumu Waziri William Lukuvi kuwa alitaka kuiba ripoti ya kamati
yao kuhusu uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Sakata hilo lilihitimishwa Jumamosi wakati Bunge lilipoazimia kuwajibishwa kwa watu wote waliohusika kwenye uchotwaji wa fedha hizo, ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa taasisi za fedha zilizoruhusu kufanyika kwa miamala mikubwa kinyume na taratibu za kibenki.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao wawili kutoka Chadema na CCM walilieleza gazeti hili kuwa jaribio hilo lilishindikana baada ya wao na mjumbe mwalikwa, Luhanga Mpina (CCM) kuamua kukesha wakiilinda ripoti hiyo tangu ilipokuwa ikichapwa hadi ilipowasilishwa bungeni.
Hata hivyo, Lukuvi alikanusha vikali tuhuma hizo akisema kuwa aliipata ripoti hiyo siku iliposomwa na kwamba kama angehusika, asingekubaliwa kuwa mjumbe wa kamati ya maridhiano iliyoundwa mwishoni mwa kikao kupendekeza maazimio ya Bunge.
“Si kweli,” alisema waziri huyo wa nchi anayehusika na sera, utaratibu na Bunge.
“Unajua PAC walikuwa wanafanya kazi chini ya hazina. Hata Spika wa Bunge hakuiona hiyo ripoti, aliisikia tu ikisomwa bungeni. Kwanza kamati ilikuwa ikidurufu hiyo taarifa yake eneo la mbali na ili uipate ilikuwa ni lazima umrubuni Zitto.”
Aliongeza kusema: “Kama kweli nilikuwa nataka kuiba taarifa yao nisingekubali kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya maridhiano, iliyokutana kupitia upya mapendekezo ya PAC baada ya yale ya awali kuzua mvutano bungeni.”
Hata hivyo, Filikunjombe, ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa walilazimika kumwondoa eneo la kuchapishia ripoti hiyo. “Waziri Lukuvi alitumwa saa 9:00 usiku kuiba taarifa yetu wakati tunaichapa. Taarifa ilikuwa katika ‘flash’ na tulipogundua hilo tulimfukuza. Sisi tuliamua kuilinda ripoti ili isiibwe,” alisema Filikunjombe ambaye ni mbunge wa Ludewa kwa tiketi ya CCM.
“Ile taarifa tuliichapa usiku wa kuamkia Jumatano ambayo ilikuwa siku ya kuiwasilisha bungeni. Na hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kikao cha Bunge kuahirishwa mara tu baada ya PAC kuwasilisha taarifa yake, ili Serikali ikajipange,” aliongeza.
Mbali na kauli yake ya jana, Filikunjombe aligusia suala hilo la ulinzi wakati akishukuru wabunge kwa kushikamana katika kufikia maazimio manane ya kuwawajibisha wote waliohusika.
Katika shukrani hizo, Filikunjombe alisema walilazimika kukesha usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita kuilinda ripoti yao isiibiwe na hivyo kuwashukuru watendaji wa Bunge kwa kazi nzuri.
Hata hivyo, kabla ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo kulienea taarifa kuna watu waliiiba na kunyofoa kurasa zilizokuwa na nyaraka za vielelezo na baadaye kuanza kuzisambaza. Polisi ilidai baadaye kuwa ilimkamata mtu aliyekuwa akisambaza vitabu hivyo vya ripoti, lakini hadi leo hajafikishwa mahakamani wala hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na polisi kuhusu maendeleo ya mtuhumiwa huyo.
Katika sakata hilo kubwa la aina yake, Bunge limtia hatiani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Mwanasheria Mkuu Jaji Fredrick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Eliachim Maswi na wakurugenzi wa Shirika la Umeme kwa kuhusika kwa makusudi au kwa uzembe katika kufanikisha miamala haramu kutoka kwenye akaunti hiyo.
Bunge pia lilitaka hatua za kisheria zishughulikie watu wote waliohusika kwenye sakata hilo, wakiwemo wanasiasa waliopokea fedha za mgao, taasisi za kifedha zilizohusika kufanikisha miamala haramu na wafanyabiashara waliohusika.
Vikwazo
Akizungumzia vikwazo walivyokumbana navyo wakati wa kutekeleza majukumu yake, Filikunjombe alisema kamati hiyo, iliyokuwa na wajumbe 24, watatu wakiwa waalikwa, kati yao 19 kutoka CCM na watano kutoka upinzani, walipata vikwazo vingi ikiwa ni pamoja na jaribio la kurubuniwa.
Filikunjombe alisema wajumbe wa PAC waliamua kuwa kitu kimoja na kuweka itikadi zao pembeni licha ya watu mbalimbali kutumia fedha kutaka kuwagawa ili wasisimamie ukweli. “Unajua sakata la Escrow linawagusa watu wenye fedha ambao walianza kuuaminisha umma kuwa wajumbe wa PAC na sisi tumekula fedha hizo. CCM ilitakiwa kuuchukulia wizi huu kama ajenda yake kuu,” alisema.
Alisema hakupendezwa na ushauri uliotolewa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge kuhusu adhabu wanazotakiwa kupewa watuhumiwa wa wizi wa fedha hizo, wakati na yeye akiwa miongoni mwa watuhumiwa kutokana na kudaiwa kupewa Sh1.6 bilioni.
Kuhusu suala la watuhumiwa kujiuzulu, Filikunjombe alisema siku zote Serikali haipendi kusimamiwa na Bunge, bali inapenda kushauriwa na kwamba hiyo ndiyo sababu ya Serikali kukataa pendekezo la PAC la wahusika kujiuzulu bila kuziomba mamlaka za uteuzi kutekeleza hilo.
“Ukitizama suala la (mkataba wa ufuaji umeme) Richmond si kama fedha zilichotwa wazi, lakini hili la escrow fedha zimechotwa na waliochota wanajulikana, sasa iweje tushikwe na kigugumizi kutaka wajiuzulu. Tena fedha hizo ni mara tatu ya zile za Richmond,” alisema.
Zitto ataja vitisho
Kwa upande wake Zitto alisema: “Vitisho vilikuwa vingi, lakini siyo kutoka serikalini bali kutoka kwa watu binafsi ambao wanahusika na uchotwaji huu wa fedha.
“Mfano kupigiwa simu kuambiwa niachane na jambo hili ama sivyo nitakufa au hata kutishiwa kuchafuliwa. Vipeperushi vya matusi dhidi yangu vilisambazwa kwenye nyumba za wabunge ili kuniondolea heshima na uhalali wa kuongoza vikao.”
Akieleza sababu za kuilinda ripoti, Zitto alisema: “Kwa sababu Serikali ilikuwa inataka kuipata mapema ili kuichakachua, hatukulala siku hiyo mpaka taarifa yetu ilipokuwa taarifa rasmi ya Bunge. Mimi, Deo na Luhaga ndio tuliopewa jukumu hilo.”
Alisema hawakupata usumbufu kutoka serikalini, isipokuwa pale zilipoanza kujengwa hoja kuwa mahakama imezuia mjadala.
Alipoulizwa kama watuhumiwa wa sakata hilo waliwahi kumfuata kwa namna yoyote ile alisema: “(Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen) Masele peke yake ndiye alikuwa akiomba msaada. Maswi alinipigia simu siku moja tu kuomba msaada, lakini sikumjibu kitu. PAC tunaamini kuwa tumetenda haki kwa wananchi.”
Maswi alipopigiwa simu jana alipokea na mwandishi alipojitambulisha, alikata simu na alipopigiwa tena kwa simu tofauti alipokea na alipoulizwa swali hilo aliikata tena simu. Ripoti ya PAC ilisomwa na kujadiliwa bungeni na kusababisha mtikisiko mkubwa kutokana na mapendekezo yake kuwagusa watu wazito ndani ya Serikali.
Watu wengine waliotajwa kwenye ripoti hiyo ni wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na kuwavua nyadhifa zao wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge., Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Andrew Chenge (Kamati ya Bajeti).
Mapendekezo hayo yanataka Mwambalaswa, Ngeleja na Chenge wavuliwe nyadhifa zao, sambamba na wote waliohusika katika muamala wa Akaunti ya Escrow kuchukuliwa hatua baada ya uchunguzi.MWANANCHI