Ticker

6/recent/ticker-posts

HUYU NDIE MNYAMA CHUI NA TABIA ZAKE

Karibu katika safu mpya kabisa inayoongelea wanyama wa aina mbalimbali, walio katika mbuga zetu hapa Tanzania, na duniani kwa ujumla. Leo nitamzungumzia mnyama aitwaye chui.

Chui ni mnyama aliye katika kundi la mamalia yaani wanyama wanaonyonyesha, na pia wako katika ukoo wa paka, kwa maana kwamba wana tabia na maumbile yanayofanana na paka. Wanyama wengine walio jamii ya paka ni simba, duma, jaguar, chui milia(hawa wanapatikana sehemu za ulaya na afrika Kusini)
Chui ni mnyama mwindaji anayewinda kimyakimya sana. Anao uwezo wa kuwinda mnyama mkubwa kwa sababu ya fuvu lake kubwa lenye taya zenye nguvu. Urefu wa kichwa na mwili wake ni kati ya sm 125 na 165 na mkia wake unakaribia sm 60 mpaka 110. Urefu wa mabega ni sm 45 mpaka 80. Chui dume ni wakubwa 30% zaidi ukilinganisha na jike, kufikia uzito wa kg 37 mpaka 91 ukilinganisha na jike wenye kg 28 mpaka 60.
Chui wenye miili mikubwa hupatikana kwenye maeneo yaliyojitenga na wanyama wengine wala nyama hasa toka kwa wale jamii ya paka wakubwa waliozoeleka kama vile simba na chui wakubwa wenye milia,"tigers".
Chui mara nyingi huchanganywa na paka wengine wenye madoa, duma na "jaguar". Hata hivyo wana mtindo tofauti wa madoa: duma wana madoa ya kawaida yaliyosambaa mwili wote; jaguar wana madoa madogo ndani ya vijimiraba; wakati chui ana madoa ndani ya miduara midogo kuliko ile ya jaguar. Chui ni mkubwa na mwenye misuli zaidi kuliko duma, lakini mdogo kidogo na mwenye misuli kidogo kuliko jaguar. Madoa ya chui walio Afrika Mashariki ni ya mviringo, na kwa walio kusini mwa Afrika huwa ya mraba. Wanyama aina ya chui wanakadiriwa kuishi umri wa miaka 21.
Chui anao uwezo wa kukwea miti, na huonekana akijipumzisha kwenye matawi ya miti wakati wa mchana, na mara zote hupenda kuburuza mawindo yake mpaka juu ya miti na kuining’iniza huko tayari kwa kujilisha. Ni mara chache chui kula mawindo yake chini ni isipokuwa anapokuwa na watoto. Chui ni mnyama mwenye nguvu za wastani akilinganishwa na wanyama wengine wa jamii yake.
Mnyama huyu anao uwezo wa kukimbia km 58 kwa saa, kuruka mbele zaidi ya mita 6 na kuruka juu kiasi cha kufikia mita 3. Chui kiasili ni miongoni mwa wanyama wanaowinda usiku, japo wamerekodiwa mara kadhaa wakiwinda mchana. Wao hutumia muda wao mwingi kulala, aidha juu ya miti, kwenye miamba au kwenye nyasi. Inasemekana ni mnyama mkali na muoga na ndio sababu hupenda kuishi juu ya miti au katika vichaka vilivyoshonana sana.
Ikumbukwe kwamba chui ni jamii ya viumbe wanaokula nyama. Chakula kikuu cha chui ni wanyama.  Ingawa hupendelea wanyama wa umbo la kati, chui hula wanyama kama vile pofu dume mwenye kg 900, swala, nyumbu n.k. Milo yao hujumuisha sana wanyama wenye kwato na nyani, lakini hula mamba, ndege na samaki. Kwa Afrika, swala wa umbo la kati ndio chakula kikuu cha chui, hasa swala pala. Huko Asia chui hula mbawala, chitali na muntiako na pia aina ya paa wa Asia na Ibex.

Chui akimfuatilia kwa makini mnyama aitwaye Kakakuona

Chui akiwa amemkamata Mamba


Chui akiwa juu ya mti

Post a Comment

0 Comments