RC Arusha Atoa Siku Tatu kwa Madereva Toyo Kutii Maagizo ya Usalama


Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenan Kihongosi akiongea na waendesha boda boda pamoja na bajaji Katika uwanja wa kumbukumbu ya sheikh Amri Abeid jioni Arusha 

Na Woinde Shizza,Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenan Kihongosi, amefanya kikao maalumu na madereva wa vyombo vya usafiri mdogo ikiwemo toyo na bajaji, kwa lengo la kujitambulisha rasmi na kutoa maelekezo ya usalama na utaratibu wa uendeshaji katika jiji hilo la kitalii.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jijini Arusha Katika viwanja sheikh Amri Abeid ,  Kihongosi aliwapa madereva hao siku tatu kuhakikisha kuwa wanatoa milio inayofanana na mabomu waliyoiweka kwenye pikipiki zao maarufu kama "toyo", akisisitiza kuwa baada ya muda huo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.



"Milio hiyo si salama, inatisha wananchi na kuharibu taswira ya mji wetu wa utalii, tutaifuatilia na kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka agizo hili," alisema Kihongosi kwa msisitizo.



Aidha, aliwataka madereva hao kuhakikisha wanavaa kofia ngumu (helmet) wakati wote wanapoendesha vyombo vyao kwa ajili ya usalama wao binafsi, akisema miili yao ni mali ya serikali na lazima ilindwe.


Katika kuimarisha nidhamu barabarani,  aliwasihi madereva kutokimbia polisi wanaposimamishwa, bali washirikiane kwa amani na kufuata sheria zote za usalama barabarani.


"Kazi yenu ni ajira kama kazi nyingine jukumu lenu ni kubwa kwa jamii, hivyo msikubali kugawanywa na mtu yeyote, wakiwemo wanasiasa," alisema.

Kihongosi aliwahimiza pia kuwa chanzo cha taarifa kwa vyombo vya dola, kwani wao hupokea abiria wengi na wanaweza kusikia mazungumzo ya kihalifu, huku akiwataka wawe mstari wa mbele kutoa taarifa za uhalifu zitakazosaidia kulinda usalama wa mkoa wa Arusha.

Katika hatua nyingine, RC alitoa onyo kali kwa vibaka, wezi na tatu mzuka, akisema kwamba hawana nafasi katika mkoa wa Arusha na kwamba biashara hizo ni hatari na zisizo na tija.


"Nawaambia wazi, kazi hiyo si salama, mkoa huu hautakuwa sehemu ya watu wanaoamua kufanya uhalifu na kuharibu amani, hatuwezi kukuza utalii kama mgeni anakuja na kuibiwa," alisema.

Alihitimisha kwa kumtaka Kamanda wa Polisi Wilaya (OCD) kutowavumilia watu wanaovunja sheria kwa makusudi, huku akisisitiza kuwa Arusha lazima ibaki kuwa mahali salama kwa raia na wageni.

Aidha madereva hao waiomba mkuu wa mkoa kusaidia upya kuangalia sehemu ambazo wanapaki pamoja na kuwasaidia kurudishiwa njia za kupita na vituo vya bajaji kwani kuna sehemu ambazo wamezuiwa kubeba abiria na kupaki  Hali inayowapelekea kazi yao kuwa ngumu.



Kwa upande WA swala hilo mkuu wa mkoa aliwahaidi kulifanyia kazi na  kukutana nao tena kabla ya mwezi wa tisa kuwapa majibu.

Post a Comment

0 Comments