Tume ya Uchaguzi yawanoa wasimamizi kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025


Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Zakia Abubakary, amesema kuwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ni ya kitaifa na yanahitaji watendaji wenye weledi, uadilifu na uzingatiaji wa sheria, kanuni na Katiba.


Zakia alitoa kauli hiyo leo Julai 21, 2025 jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa waratibu, wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi,Mafunzo hayo yamepangwa kufanyika hadi Julai 23, yakilenga kuwawezesha watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.


Alieleza kuwa watendaji hao wamepewa dhamana kubwa ya kusimamia mchakato wa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa upande wa Tanzania Bara, hivyo ni muhimu kwao kulinda siri, kutokuwa wanachama wa chama chochote cha siasa, na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu.


"Nawasihi msimamie viapo vyenu vya kutunza siri na kutojihusisha na vyama vya siasa, Uchaguzi huu ni wa Taifa, na nyie ndio mnaoubeba," alisema Zakia.


Aliwataka watendaji hao kuanza mapema utambuzi wa vituo vya kupigia kura ili kubaini mahitaji maalum, pamoja na kuhakikisha kuna mpangilio mzuri utakaowezesha uchaguzi kufanyika kwa amani na utulivu.


Kadhalika, Zakia aliwataka kusoma kwa makini Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na tume ili kujiepusha na malalamiko kutoka kwa wadau wa uchaguzi.


"Maelekezo na miongozo ni nguzo kuu katika utekelezaji wa kazi zenu. Wahakikishe mnazingatia ipasavyo kila kinachotolewa na Tume," aliongeza.

Aidha, Zakia alifafanua kuwa mafunzo kama hayo yanaendelea pia katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Shinyanga, Rukwa na Kusini Pemba, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu.


Kwa mujibu wa tume, uteuzi wa maafisa uchaguzi na maafisa ununuzi umetolewa kwa kuzingatia masharti ya kisheria yaliyoainishwa katika Kifungu cha 6(1), (2), 5 na Kifungu cha 8(1) na (2) vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.




About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia