Na Woinde Shizza, Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amepokea Mwenge wa Uhuru 2025 kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Gloriana Julias Kimathi, katika hafla iliyofanyika katika uwanja wa Magereza Kisongo, tayari kwa kuukimbiza katika Jiji la Arusha leo
Akizungumza mara baada ya kupokea Mwenge huo, Mkude alisema kuwa Mwenge wa Uhuru katika Jiji la Arusha utakimbizwa umbali wa kilomita 117.8 na utazungukia jumla ya miradi minane ya kisekta yenye thamani ya Sh bilioni 8.6.
Aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa maji wa Moivaro uliogharimu Sh bilioni 3.6, ujenzi wa jengo la utawala Shule ya Msingi Terrat wenye thamani ya Sh milioni 21, na uzinduzi wa mradi wa nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari Korona uliogharimu Sh milioni 21.
Aidha, alisema Mwenge huo utaweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 2.4 katika maeneo ya Kwa Benson, CCM, TCA, Levolosi hadi TRA East Africa, mradi ambao umegharimu Sh bilioni 2.7.
Vilevile, Mwenge wa Uhuru 2025 utazindua huduma ya uchunguzi wa saratani ya matiti katika Kituo cha Afya Kaloleni, mradi unaogharimu Sh milioni 440, na kutembelea mradi wa kiuchumi wa kikundi cha vijana cha Alvena Bees Investment kilichopo kata ya Kaloleni, mradi wenye thamani ya Sh milioni 110.
Pia, Mwenge huo utazindua ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa, matundu 22 ya vyoo na ofisi nne kwa mfumo wa ghorofa katika Shule ya Sekondari Arusha, mradi unaogharimu Sh milioni 694.1, sambamba na kutembelea mradi wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa wa JSM uliopo kata ya Sombetini wenye thamani ya Sh milioni 800.
Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, ameweka jiwe la msingi katika mradi wa jengo la utawala la Shule ya Msingi Terrat, kata ya Muriet, mradi unaogharimu Sh milioni 21, fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Ussi aliipongeza halmashauri hiyo kwa hatua kubwa ya maendeleo na utekelezaji wa agizo la serikali kuhusu matumizi ya nishati safi kwenye taasisi.
Alisema Jiji la Arusha limefikia asilimia 92 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi zenye watu zaidi ya 100, hatua aliyoieleza kuwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Rais wetu amekuwa balozi wa nishati safi Afrika ametafiti, kagundua athari za kuni na mkaa, akaanzisha kampeni ya matumizi ya nishati safi na sasa Tanzania inaongoza ,hili ni jambo la kujivunia kama taifa," alisema Ussi.
Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni: "Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa Amani na Utulivu."
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia