Na Woinde Shizza, Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi, ametoa wito mzito kwa wananchi wa mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kulinda amani ya nchi kwa nguvu zote, huku akihimiza mshikamano na upendo miongoni mwa jamii ili kuleta maendeleo ya kweli kwa taifa.
Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wamiliki wa saluni na wafanyakazi wa sekta hiyo jijini Arusha, Kihongosi alisema kuwa amani ndiyo msingi wa kila hatua ya maendeleo, na kwamba haitakiwi kuruhusu mtu au kikundi chochote kuivuruga.
“Wasikubali kabisa kuvunjiwa amani ya nchi yao. Amani hii si ya bahati mbaya, ni urithi wa wazee wetu na tunapaswa kuilinda kwa gharama yoyote,” alisisitiza Kihongosi huku akipongeza mkoa wa Arusha kwa kuwa kitovu cha utalii, hivyo kuhitaji huduma zenye weledi na nidhamu ya hali ya juu.
Aidha, RC Kihongosi alihamasisha wanawake wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo ya mama inayotolewa na serikali kupitia mpango wa kuwawezesha wanawake kiuchumi. Alisema fedha zipo na zinatolewa kwa dhamira ya dhati ya kuinua maisha ya wanawake na familia zao.
“Tusikubali kuona wanawake wanakosa fursa hii. Fedha zipo, na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kuwainua wanawake wa taifa hili,” alisema.
Katika hotuba hiyo, pia alitoa maagizo kwa Maafisa Biashara na watendaji wote kuacha majungu na chuki zisizo na tija, badala yake wajikite katika kazi, kushirikiana na kuwa chachu ya maendeleo kwenye maeneo yao.
“Tuachane na maneno ya chini kwa chini. Badala yake, tuchape kazi kwa moyo mmoja. Huu ndiyo wakati wa kujenga Arusha mpya yenye nidhamu, mshikamano na maendeleo,” alisema kwa msisitizo.
Kadhalika, aliwataka wananchi kujitokeza kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa hivi karibuni, na kuchagua viongozi bora watakaosimamia haki, maendeleo na amani ya kweli.
Kauli za RC Kihongosi zimekuja wakati ambapo taifa linapita kwenye kipindi nyeti cha maandalizi ya uchaguzi, huku changamoto za kijamii na kiuchumi zikionekana kwa baadhi ya maeneo. Hivyo, wito wake umeibua mjadala mpana kuhusu wajibu wa kila Mtanzania katik
a kulinda misingi ya taifa.
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia