Wananchi wa vijiji vinavyoizunguka hifadhi ya mazingira asili ya Chome
iliyopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro wamekuwa washirika wakubwa
katika uhifadhi baada ya kupatiwa shughuli mbalimbali mbadala rafiki na
mazingira ambazo mbali na kujipatia kipato zimewapunguzia kasi ya
kuingia ndani ya hifadhi na kuvuna rasilimali za misitu zikiwemo
kuni,mbao na uchomaji mkaa kwa ajili ya kujipatoa mahitaji.
Mfuko wa
Uhifadhi wa milima ya Tao la mashariki(EAMCEF)ndio waliowajangea uwezo
wananchi hao baada ya kujiunga kwenye vikundi vya uzalishaji .
Miongoni
mwa vijiji vilivyonufaika na mpango huo ni kijiji cha Ndolwa kilichopo
katika kata ya Vudee ambacho kikundi cha wafugaji nyuki cha Mkombozi
kilipatiwa jumla ya mizinga 60 ya kisasa na vifaa vya kurinia asali
yakiwemo mavazi na mashine ya kucakata asali.
Kwa mujibu
Mwenyekiti wa kikundi hicho Ntarishwa Mnzava kwa kuvuna asali
iliyotokana na mizinga hiyo wamefanikiwa kupanua mradi wao kwa kuuza
asali na kununua mizinga mingine na kwa sasa wana jumla ya mizinga 100.
"pamoja
na kuongeza idadi ya mizinga lakini pia tumekuwa tukigawana fedha
zinazotokana na mapato ya asali ambazo zimekuwa msaada mkubwa sana
kwetu kwenye kuwapeleka watoto shule na mahitaji mengine ya familia
lakini baadhi yetu wameweza kununua mifugo kama kuku na mbuzi ambao
wameongeza mnyororo wa kipato cha familia"alisema Mnzava na kuongeza
kuwa kwa msimu wamekuwa wakivuna asali mpaka zaidi ya lita 400.
Akizungumzia
jitihada hizo zinazofanywa na EAMCEF kuwashirikisha wananchi katika
utunzaji wa mazingira ya hifadhi ya Chome Afisa mtendaji wa kijiji hicho
cha Ndolwa Yassir Ayoub alisema mradi huo wa ufugaji nyuki umesaidia
pia katika urejeshaji wa uoto wa asili vikiwemo vyanzo vya maji
vilivyokuwa vimekauka kutokana na ukataji wa miti lakini mizinga
inayotundikwa msituni imekuwa ni nia mojawapo ya ulinzi,ambapo alieleza
pia kuwa kutokana na kipato wanachopata wanakikundi kimesaida hata kwa
upande wa elimu kwa watoto kupatiwa mahitaji yao ya msingi na kupunguza
utoro.
Kwa upande wa uongozi wa Hifadhi ya Mazingira asili ya Chome mwakilishi wa hifadhi hiyo Samweli Mtaning'ombe anakiri kuwepo kwa mabadiliko chanya ndani ya msitu baada ya wananchi kujengewa uwezo wa kujipatia kipato mbadala na kuimarishwa doria ambapo alieleza kuwa kutoakana na uhaba wa watumishi awali ilikuwa ni ngumu kumudu kudhibiti uhalifu ndani ya hifadhi lakini kwa sasa wananchi wenyewe wamekuwa walinzi baada ya kutambua umuhimu wa hifadhi hiyo kwa uendelevu wa maisha yao.
Afisa miradi wa EAMCEF kanda ya kaskazini Magreth Victor alisema mfuko huo umekuwa ukitoa ruzuku kwa Hifadhi ya mazingira asili ya Chome kila mwaka zaidi ya Shilingi milioni 25 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya hifadhi ikiwemo usafishaji wa mipaka pamoja na kuongeza doria lakini pia kuwajengewa uwezo wananchi kwa kuwapatia shughuli mbadala ili wawe walinzi bora wa msitu kutokana na umuhimu wa milima hiyo ambayo ndiyo chanzo kikuu cha maji yanayotegemewa kwenye matumizi mbalimbali yakiwemo ya nyumbani,umwagiliaji na hata uzalishaji wa umeme katika bwawa la Nyumba ya Mungu.
Mkuu wa wilaya ya Same Rdward Mpogolo aliahidi serikali wilayani humo kuendelea kushirikiana na Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki EAMCEF kwa uhifadhi endelevu wa hifadhi ya mazingira asili ya Chome ambapo alisema wako mbioni kufanya operesheni maalum ya kuwasaka wale wanaokwenda kinyume na sheria za uhifadhi kwa kuendelea kuendesha shughuli za binadamu ndani ya hifadhi.
"wadau wamekuwa wakijitoa kushirikiana na wananchi kuuhifadhi msitu wa chome lakini bado wapo wachache wanaojaribu kuendeleza uhalifu,niwatahadharishe tu kuwa operesheni itakayoanza haitakuwa na msamaha"alisema mpogolo.
Hifadhi ya mazingira asili ya Chome ina eneo lenye ukubwa wa hekta 14,283,ikiwa ndani ya kilele cha milima ya Upare na imesheheni vivutio mbalimbali ikiwemo miti mikubwa,ndege wa aina mbalimbali,maporomoko na maji,maeneo ya asili yaliyokuwa yakitumiwa na wazee wa kabila la Wapare kwa ajili ya mila ambavyo vyote vimekuwa vivutio vikubwa kwa watalii .