WATENDAJI UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2025 WAFUNDWA
Na. Mwandishi wetu.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewaasa watendaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume.
Hayo yamesemwa mkoani Morogoro na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele wakati akifungua mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba mwaka huu kwa tarehe itakayotangazwa na Tume.
Jitahidini na mjiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi. Hakikisheni mnazingatia ipasavyo Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume, amesema Jaji Mwambegele.
Amewataka watendaji hao kuvishirikisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika hatua zote kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, sheria, kanuni na maelekezo ya Tume.
Amewasisitiza pia juu ya umuhimu wa kuwashirikisha wadau wa uchaguzi kwenye maeneo wanayopaswa kushirikishwa kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo ya Tume.
Amewakumbusha kuhusu wajibu wao wa kuhakikisha wanavitambua vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika na kuhakikisha kunakuwa na mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
“Ajira za watendaji wa vituo zizingatie kuajiri watendaji wenye weledi, wanaojitambua, wazalendo, waadilifu na wachapakazi na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi, amesema Jaji Mwambegele.
Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk akifungua mafunzo hayo Unguja leo na amewasisitiza watendaji hao kuhakikisha vifaa vya uchaguzi wanavyopokea kutoka Tume, wanavihakiki, kuvikagua na kuhakikisha vinasambazwa kwenye vituo vyote na kila mkuu wa kituo anapata vifaa vyote vya uchaguzi vinavyohitajika mapema
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia