MWELEKEO wa upelelezi wa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow umebadilika na sasa tukio hilo linahusishwa na kisasi cha mapenzi na tayari mtu mmoja anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi Mwalimu Dorothy Moses kutiwa mbaroni na polisi.Awali, ilidaiwa kwamba Kamanda Barlow ambaye aliuawa kwa risasi usiku wa kuamkia Jumamosi muda mfupi baada ya kumfikisha mwalimu huyo nyumbani kwake, alivamiwa na majambazi.
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI, Robert Manumba
alithibitisha jana kukamatwa kwa mtu huyo (jina tulihifadhi) akisema: “Ni kweli
mtu mmoja amekamatwa, lakini kwa sasa siwezi kuzungumzia kwa kina kuhusu suala
hilo kwa sababu bado tunamhoji na
tunaendelea na uchunguzi. Tutakapokamilisha, tutatoa taarifa.”
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola pia
alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo. Hata hivyo, alisema amesikia habari
hizo kwa kuwa yuko safarini kwenda mkoani Kilimanjaro kwenye mazishi ya kamanda
huyo... “Hayo nimesikia, lakini kwa sasa sipo Mwanza hivyo siwezi kuzungumzia
lolote.”
Habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi,
zinaeleza kwamba upelelezi wa mauaji hayo umefanikiwa kwa hatua kubwa na kwamba
mtu huyo alikamatwa Dar es Salaam baada ya kuwekewa mtego na makachero waliopo
katika timu ya uchunguzi na alisafirishwa hadi Mwanza ambako anashikiliwa na
jeshi hilo.
Ilielezwa kuwa mtu huyo alikamatwa kutokana na kuwapo kwa
taarifa za siri za kiitelejensia kutoka kwa watu mbalimbali.
“Kuna hali imefunguka na imesaidia sana. Inaonyesha kwamba
Dorothy alikuwa na uhusiano na mtu huyu ambaye alikuwa akifika nyumbani kwake,
kama mumewe na watu wanajua jambo hili,” alieleza mmoja wa askari polisi ambaye
hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Alisema kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba uamuzi
wa mwalimu huyo kusitisha uhusiano wa mapenzi na mtu huyo huenda ndicho chanzo
cha mauaji hayo lengo likiwa ni kumshawishi Dorothy kurejesha uhusiano.
“Mimi natambua kwamba huyu jamaa na Dorothy walikuwa na
uhusiano na inajulikana mjini kuwa hata mke wa mtuhumiwa anatambua jambo hilo
kwani walishagombana siku moja mjini na hata katika msiba nyumbani kwao na
mtuhumiwa,” alisema mama mmoja (jina tunalo), aliyejitambulisha kama mmoja wa
marafiki wa karibu wa Dorothy.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitangiri (jina tunalo),
anasema amekuwa akimfahamu mtuhumiwa aliyekamatwa kama baba mwenye nyumba hiyo
na kila mara amekuwa akimkuta hapo nyumbani wakati wa kujisomea na wanafunzi
wenzake.
“Mimi ninamfahamu kama baba wa rafiki yangu na nimewahi
kumkuta wakati wa kujisomea hapo nyumbani na watoto wa nyumba hiyo.”
Dorothy ambaye ametajwa kuwa mjane, ni Mwalimu katika Shule
ya Msingi Nyamagana na tangu kufariki kwa mumewe Ofisa wa zamani wa TRA, Modest
Lyimo mwaka 1997.
“Watu wote wanajua kwamba mtuhumiwa alikuwa akitembea na
huyo mwalimu, wameonekana mara nyingi wakiwa muziki,” alieleza mmoja wa ndugu wa
karibu wa mke wa mtuhumiwa.
Hili ni tukio la tatu mkoani Mwanza kutokea kwa ofisa wa
polisi kuuawa. Katika tukio la awali lililotokea mwaka 1987, askari
aliyetambulika kwa jina la Inspekta Gamba aliuawa kwa risasi na watu
wanaosadikiwa kuwa ni majambazi eneo la Nyakato na katika tukio la pili mwaka
1997, aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Kati ASP Mahende aliuawa kwa kupigwa risasi
eneo la Bugando saa nne usiku alipokuwa akifuatilia majambazi waliokuwa
wakijitayarisha kuvamia.
Dar wamuaga Kamanda Barlow
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal aliongoza
waombolezaji waliofika kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Barlow
nyumbani kwake, Ukonga Dar es Salaam jana.
Mwili wa Kamanda Barlow ambao unasafirishwa leo kwenda
mkoani Kilimanjaro kwa mazishi, uliwasili
nyumbani kwake saa 6.45 kabla ya kupelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Agustino, Ukonga kwa ajili ya
ibada na kutoa heshima za mwisho.
Akitoa salamu za Serikali, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Pereira Silima alisema kifo cha Kamanda Barlow ni pengo kwa taifa...
“Tutahakikisha watuhumiwa wanapatikana kwa mikono yote miwili na hatua za
kisheria zinachukuliwa dhidi yao.”
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema alisema juhudi za
kuwasaka watuhumiwa zinaendelea kwa ushirikianao wa wananchi.
“Kifo cha Kamanda Barlow kimeacha pengo kwani hivi sasa
askari mmoja analinda watu 1,300 hivyo kwa kifo chake unaweza kuona ni pengo la
aina gani na ukilinganisha yeye alikuwa kamanda wa mkoa mzima,” alisema IGP
Mwema.
Alisema jeshi lake litaendelea kulinda amani ya wananchi na
kifo cha Kamanda Barlow kinalifanya liongeze nguvu.
Akitoa mahubiri, Padri Veri Urio alisema kila jambo hutokea
kwa wakati na kifo cha Kamanda Barlow kimesababishwa na watu. Alisema mwenye
mamlaka ya kuondoa uhai wa mtu ni Mungu pekee hivyo waliosababisha kifo chake
siku ikifika, watajibu kwa nini walifanya hivyo.
IGP Mstaafu, Omary Mahita alisema atamkumbuka Kamanda
Barlow kwa uchapaji wake kazi tangu akiwa polisi Interpol (polisi kimataifa)alifanya kazi kwa
weledi uliotukuka.
“Daima nitamkumbuka kwani nimefanya naye kazi sehemu
tofauti na askari waliobaki waige mfano wake wa uwajibikaji” alisema
Mahita.
Mbali ya Dk Bilal, viongozi wengine walioshiriki katika
ibada hiyo jana ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, makamanda wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), makamanda wa polisi, viongozi wa Serikali na vyama vya siasa na
wananchi.
Imeandikwa na Frederick Katulanda, Mwanza na Ibrahim
Yamola, Dar.
CHANZO CHA HABARI HII NI "GAZETI LA MWANANCHI".
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia