Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) |
MJADALA
mkali uliibuka bungeni jana baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe (Chadema) kuwalipua baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali
akitaka wachunguzwe kwa makosa ya kuficha mabilioni ya fedha nje ya
nchi.
Zitto
alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akiwasilisha hoja yake binafsi
kuhusu kulitaka Bunge kuchunguza na kuielekeza Serikali kuchukua hatua
dhidi ya raia wa Tanzania walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.
Bila
ya kuwataja kwa majina, mbunge huyo aliwataja watu hao kwa nyadhifa
kuwa ni watu wote walioshika nyadhifa za uwaziri mkuu katika kipindi cha
2003 hadi 2010, walioshika nyadhifa za uwaziri wa nishati na madini
katika kipindi hicho na waliokuwa makatibu wakuu Wizara ya Nishati na
Madini.
Wengine
ni mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara ya Ulinzi, wakuu wa majeshi,
wanasheria wa Serikali, makamishna wa nishati, walioshika wadhifa wa
Ukurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),
Uenyekiti na Ujumbe wa Bodi wa TPDC katika kipindi cha mwaka 2003 hadi
2010.
Kutokana
na hilo, Zitto aliitaka Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria
bungeni wakati wa Mkutano wa 11 wa Bunge wa Aprili mwakani.
“Mbali
na hilo napendekeza kuwa iwe ni marufuku kwa kiongozi yeyote wa umma au
mume au mke wake au mtoto wake kuwa na akaunti nje ya nchi isipokuwa
kwa sababu maalumu na kwa kibali rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano,” alisema Zitto.
Pia
Zitto alitaka Serikali kuwasiliana na Benki ya Dunia kupitia kitengo
cha ‘Assets Recovery Unit’ ili mabilioni ya fedha na mali ambazo
zimetoroshwa nje ya nchi kwenda Uswisi, Dubai, Mauritus na maeneo
mengine ziweze kurejeshwa.
Aliwataka
Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya nchi waeleze wamezipata
wapi na Takukuru wachukue hatua za kisheria dhidi ya watu wote
wanaomiliki fedha hizo kinyume cha sheria.
Zitto
alisema katika mkutano wa Bunge la 11 na baada ya taarifa ya Kamati
Teule ya Bunge kuhusu raia wa Tanzania wenye kumiliki fedha za kigeni
kwenye benki na mali nje ya Tanzania ilete taarifa ya hatua ilizochukua
ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha nje ya nchi.
Alipendekeza
kwamba Serikali katika bajeti ya mwaka 2013/14 ianzishe kodi maalumu ya
asilimia 0.5 ya thamani ya fedha zilizotoroshwa ili kuweka rekodi za
uhakiki fedha za ndani na zinazotoka nje.
Mbunge
huyo alisema mazungumzo yake na wachunguzi wake binafsi kiwango cha
fedha kinachomilikiwa na Watanzania Uswisi peke yake ni takriban mara 20
ya kiwango kilichotangazwa na benki ya taifa ya nchi hiyo.
Alisema fedha hizo ni sehemu tu ya fedha ambazo Watanzania wamezificha katika benki mbalimbali za nje.
Alitoa
mfano wa Benki ya UBS peke yake iliyopo katika nchi hiyo ina maofisa
240 ambao wanashughulikia wateja wa Tanzania na kila ofisa mmoja
husimamia mteja mmoja mwenye kiwango kisichopungua dola za Marekani 10
milioni.
Zitto
alisema Benki Kuu ya Uswisi ilitangaza kuwa jumla ya dola za Marekani
196 milioni zilikuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti za benki za nchi hiyo.
Alisema
kuwa pamoja na Mkurugenzi wa Takukuru kukaririwa akisema kuwa
ataiandikia Serikali ya Uswisi barua kuomba kurejeshwa kwa fedha hizo ,
lakini mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.
Majibu ya AG
Akichangia hoja hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema alisema Serikali imeanza kuzifanyia uchunguzi tuhuma hizo.
Alisema
kwamba siyo kwamba Serikali imelala bali inaendelea na uchunguzi na
kwamba vyombo vya usalama na Takukuru wanalifanyia kazi suala hilo.
Mbunge
wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka alisema hata kama ni Rais
aliyeko madarakani au waziri mkuu ama kiongozi yeyote atajwe bungeni ili
Bunge limwondolee kinga aburutwe mahakamani.
Alimtaka Zitto kuwataja kwa majina watu hao ili wachukuliwe hatua.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliwataja
marehemu Daudi Balali, Andrew Chenge na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya
Fedha, Gray Mgonja kwamba walihusika na tuhuma za ufisadi wa Tan Gold
hivyo Bunge linapaswa kuchukua hatua. “Si fahari kwa Serikali kuwa na
watendaji ambao siyo waaminifu,” alisema.
Aliwataka wabunge kuwa pamoja na hasa upande wa CCM kwa kuwa ni wengi waunge mkono hoja ya Zitto ili dhambi isije ikawadondokea.
Alisema mapendekezo ya Jaji Werema ni ya kuua hoja na si kuiboresha.
Naye Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina alitaka watu walioficha fedha nje ya nchi watajwe kwa majina ili wananchi wawafahamu.
Mpina
ambaye aliwahi kuwasilisha hoja nyingine ya kuwapo mabilioni
yaliyofichwa nje ya nchi na baadhi ya Watanzania, alisema yeye haogopi
kitu chochote na kwamba waliochota fedha wachukuliwe hatua.
Mbunge
wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema wapo Watanzania wanaotoa fedha
nyingi kwenye uchaguzi na kutoa misaada mbalimbali kiasi cha kuiharibu
nchi, hao peke yake wanatosha kudhihirisha kwamba ni mafisadi walioficha
fedha nje.
Alisema
Bunge lisigawanyike kama ilivyotokea katika Bunge la Tisa kwenye
masuala ya Dowans , Richmond na Epa ambapo kila wabunge wakisimama
viongozi wa Serikali wanatoa vikwazo kuzuia juhudi zao na akaapa katika
mabilioni ya Uswisi hawatalala.
Wiki
iliyopita wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kuhusu
mabilioni ya fedha yaliyofichwa nje ya nchi, Freeman Mbowe, Waziri Mkuu
Mizengo Pinda alisema Serikali imeanza kulifanyia uchunguzi wa kina
suala hilo ili kujua ukweli wake na hatua za kuchukua.
Waziri Mkuu alisema mara baada ya uchunguzi huo kukamilika Serikali itatoa taarifa kamili.
Taarifa
kutoka Benki Kuu ya Uswisi inaonyesha kuwa baadhi ya fedha hizo
zimewekwa katika akaunti za vigogo hao na kampuni za mafuta na gesi
zilizopo nchini.
Zitto
akihutubia mkutano wa hadhara Rombo mkoani Kilimanjaro Oktoba 26 mwaka
huu, alimlipua Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah akidai kuwa
bosi huyo ameandika barua Uswisi, akieleza kwamba Tanzania haina
masilahi na mabilioni ya fedha yaliyofichwa katika benki za nchi hiyo.
Hata hivyo, Dk Hoseah alikanusha akisema kuwa tuhuma hizo hazina ukweli wowote.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia