Profesa Said A Mohammed |
SEHEMU YA KWANZA
Profesa Said A Mohammed umeandika vitabu vingi.
Ama kweli wewe ni hazina ya fasihi ya Kiswahili ambaye hujapata heshima
inayokustahili. Najua hupendi kusifiwa – lakini lazima tukuthamini ungali hai
maana wewe fahari yetu Waswahili. Hata ukiweka neno “Tanzanian Novelists”,
“Zanzibar Writers”, au “Tanzanian Writers” katika Wikipedia hutajwi. Unadhani
kwanini wengi hasa Tanzania bara na
visiwani hawakufahamu ipasavyo?
Mwandishi : Said A Mohammed
Kama nilivyokueleza katika mkumbo wa
masuali uliyoniuliza mwanzo hapo kitambo, Watanzania na zaidi Wazanzibari
hawana utamaduni wa kusoma vitabu vya fasihi. Kwa hivyo hawajapata ari wala
mwamko wa kujali na kuthamini fasihi yenyewe na waandishi wake. Kweli kuna
wachache ambao wanatangazwa katika vyombo vya mawasiliano, lakini mimi simo
katika orodha ya waandishi hao. Hili ni suala la vyombo vya habari ambavyo mara
nyingi huwatukuza wale ambao wanataka wao watukuzwe. Vilevile kuna wasanii
wanaopenda kujipeleka mbele ili wasikike na hata kuwa na fikra kwamba waandishi
wengine wadidimie. Kwa bahati mbaya au labda kwa bahati nzuri, mimi si mtu wa
kimbele mbele. Naamini sana maneno ya wahenga kwamba Kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza.
Katika dunia ya sasa kujipeleka mbele ili usikike bila umakinifu, ndilo
jambo linaloharibu mambo mengi ikiwemo sanaa ya lugha. Vipawa vinadharauliwa na
sanaa tunazokutana nazo ni sanaa zinazokuzwa tu bila ya kupitiwa kwa kina na
kujadiliwa. Chambilecho, gwiji wetu wa fasihi, Profesa Ebrahim Hussein, hakuna
fasihi tena kwa maana ya fasihi. Hakuna wasomaji wazingatifu. Hakuna uhakiki
kwa maana ya uhakiki. Kuna fikra ya kwamba chochote kile ni sawa. Shairi,
riwaya, hadithi fupi au tamthilia ikiwa ina sura ya tanzu inayohusika, basi ni
fasihi tu kwa maoni ya wengi. Fasihi
haipo. Wasomaji hawapo. Umakinifu wa fasihi haupo. Uhakiki umepotea. Hata wale
ambao tunawatarajia kufanya hivyo hawashughuliki na kusoma, kuandika, kuhakiki
na kuzitangaza kazi za fasihi ya Kiswahili. Sisi waandishi hatuwezi kujitetea.
Wanaojitetea na kuwaponda wenzao ndio katika hao wanaowekwa mstari wa mbele na
wanaojitapa kuwa wanajua hata kuandika kazi za waandishi wenzi wao.
Kuna
dhana inayodai ili mwandishi ajulikane labda aanzie uandishi wa habari, ajenge
jina kihivyo kama walivyofanya baadhi ya waandishi maarufu duniani mfano:
Gabriel Marquez (Colombia) , Ernest Hemingway (Marekani) au afungwe jela kama
Wole Soyinka (wakati wa vita vya Biafra 1967-1970) na Ngugi Wa Thiong’o (Kenya,
1978). Hapa tunatumia neno “kujulikana” si kwa maana mbaya ya kutaka umashuhuri
bali kutathmini wepesi wa wasomaji kuzijua, kuzithamini na kuzipenda kazi za
mtunzi. Mathalan, Watanzania wengi wa kizazi kilichozaliwa baada ya mwaka 1970
wanamfaham marehem Elvis Musiba sana kutokana na tungo zake za mtindo wa
kiupelelezi kuliko marehem Said
Muhammed Said Abdulla aliyemtangulia kwa
mtindo huo huo.
Mwandishi Said A Mohammed:
Suala halina ukweli kamili. Kuna mamilioni ya waandishi ambao hawajui hata
maana ya uandishi habari na wengi katika hao ni waandishi wazuri wanaosifika na
wako wazuri ambao hawajasifika kwa sababu hawajapewa nafasi ya kutangazwa
katika vyombo vya habari. Nao hawapendi kujitokeza kifua mbele kwa kulazimisha
kazi zao kuwa nzuri.
Tukiendelea
na mada hii hii. Waandishi wa vizazi mbalimbali wamefahamika kwa njia tofauti.
Linganisha waandishi wa kizazi cha ukoloni na miaka michache baada ya ukoloni,
mfano Mathias Mnyampala, Shaaban Robert, Muhammed Said Abdullah, Saadan
Kandoro, Faraji Katalambula, nk-
waliothaminiwa kwa kazi zao. Vitabu vyao viliuzwa madukani na hapo hapo
kutumika mashuleni. Linganisha awamu hiyo na ile ya miaka ya 1970 kuendelea:
Mohammed S. Mohammed, Adam Shafi, Euphrase Kezilahabi, Ebrahim Hussein nk,
waliojiingiza ama katika mashindano kwanza (Mohammed Suleiman na “Kiu” -1970),
Adam Shafi (tuzo la Uandishi Bora1998) au kupitia sanaa za maonyesho (Ebrahim
Hussein). Kuanzia hapo mambo yalibadilika kabisa - waandishi wa vizazi vya
miaka 1980 kuendelea walijenga majina
kwa kujitangaza wenyewe kwa kutumia vyombo vya habari, makampuni
waliyounda. Akina Kajubi Mukajanga, Hammie Rajab, marehem Ben Mtobwa, na mwandishi
anayesomwa sana na vijana sasa hivi – E Shigongo – ambaye amewahi kuchapisha
vitabu India-na shirika lake la habari
na blog- Global Publishers. Hawa waliamua kuingia mitaani.
Mwandishi Said Ahmed Mohammed:
Kweli wakati au enzi ya wakati
fulani na mambo yake yanaathiri sio tu fasihi, bali thamani ya fasihi, maudhui
yake, fani yake, waandishi wake na kadhalika. Kwa maoni yangu wakati huu
tulionao ni wakati wa upujufu mkubwa
hasa katika dunia ya tatu. Wasomi hawana tena msimamo seuze watu wa kawaida.
Pesa inatawala, tena inatakikana ipatikane bila ya kutoa jasho. Kila kitu
kinauzwa na watu hawajui kuchagua au kutathmini vitu vyenye hadhi au pengine
wanajua lakini hawana pesa za kununua vitu vyenye hadhi. Kwa hivyo
tunaambukizana upotofu wa mambo na hatimaye hatutambui tunafanya nini.
Kujijengea kampuni na kuuza vitabu vyake mtu ni jambo linawezekana na kwa kweli
tunaliona, lakini mimi nadhani hakuna vipimo vizuri vya mtu anayefanya hivyo.
Yeye mwenyewe aandike, tena avipitie mwenyewe, avihariri mwenyewe, atambue uzuri
na ubaya wa kazi zake yeye mwenyewe na baadaye afyatue vitabu kama matofali,
basi wanaonunua vitabu vyake lazima wawe na mushikeli. Kujitangaza na hata
kutangazwa kwa maana ya kukuzwa tu na watu fulani hakuna maana ya kwamba hakuna
wengineo wanaoandika, tena wanaoandika ambao wana vipawa vikubwa zaidi. Kuepuka
utunzi wa kuuza badala ya kujiuza ndiko kunakopelekea fasihi ya Kiswahili
idharauliwe na ipuuzwe duniani.
Je tunaweza kusema wewe kama mwandishi uliyeamkia
miaka ya mwisho ya Sabini, ulitegemea tu
vitabu vyako kuingia madukani na kusomwa bila kuingia madukani kama Shigongo na
Ben Mtobwa – Mungu amrehemu - waliouza vitabu kama miwa, miswaki, nyama choma
na nyanya?
Mwandishi Said A Mohammed:
Ndiyo, mimi niliandika na mpaka
sasa naandika kwa kutegemea vitabu vyangu kuuzwa madukani, sababu ni kwamba
sitaki vitabu vyangu niviuze kama miwa, miswaki, nyama choma na nyanya. Lengo langu
sio pesa, bali ukweli na umahiri wa kuandika ingawa hata na mimi nathamini na
nazitaka pesa kama wenzangu.
Halafu kuna suala tulilozungumzia mwaka jana la
kupitisha vitabu mashuleni kwanza ndipo visomwe au kuuzwa. Hapa tunaangalia pia
tatizo linalowakumba wachapishaji na soko zima la vitabu vya Kiswahili. Wewe
mwenyewe umeandika vitabu vingi katika medani hii...
Mwandishi Said A Mohammed:
Ingawa mimi nimeandika vitabu vingi mpaka sasa, vichache tu ndivyo
vilivyopata nafasi kuingia mashuleni. Na hivyo vilivyoteuliwa kuingia shule
vilisomwa mwanzo kabla ya kusomwa kwa madhumuni ya elimu shuleni.
Upo usemi
ulioenea kwamba waandishi wa Kiswahili toka enzi za ustaadh Shaaban Robert
mwenyewe hadi leo hawawezi kuuza kazi zao duniani kama wasipoandika lugha za
Kizungu. Hapa tutoe mifano ya William Mkufya (Wicked Walk), Ismail Mbise (Blood
On Our Land), M G Vassanji na Abdul
Razak Gurnah. Profesa Gurnah na Vassanji
(ambao wamehama Afrika Mashariki miaka mingi sana) wameshashinda tuzo kibao za
kimataifa kutokana na kuandika Kiingereza. Je ndiyo suluhisho? Mbona Watanzania
na wasomaji wa Kiswahili hawawafahamu hawa wawili (Vassanji na Gurnah) hasa nao
wamechangia sana kujenga fasihi ya Kiafrika muda mrefu?
Mwandishi Said A Mohammed:
Mimi ni mmojawapo ambaye ninaamini kuandika kwa lugha apendayo na kwa
mtindo auchaguao ni haki ya mwandishi. Sababu za kuchagua lugha inakamatana na
mtu kuandikia watu gani au kwa sababu gani. Wengine wanaandika kwa fahari ya
lugha yao, utamaduni wao na uelevu wa watu wao ambao wangeweza kuisoma kazi
husika na kuitafakari. Wengine wanaandika kwa lugha ya kigeni kwa sababu wanadhani
kuwa lugha ya kigeni ina mvuto mkubwa kwa kazi ya fasihi, tena lugha ka ya
Kiingereza husifiwa na kutoa hadhi kubwa kwa waandishi. Mimi nimo katika kundi
la mwanzo, yaani kuandika kwa maana ya kukitukuza Kiswahili, fasihi na
utamaduni wake. Pia kuwapa fursa wananchi walio wengi na ambao hawakijui
Kiingereza lakini wana nafasi ya kufurahi sanaa yao lugha yao na kubwia fikra
za raia wenzao ambao ni waandishi. Zaidi ya hayo, si kweli kwamba wanaoandika
kwa Kiingereza wanathaminiwa au wanapata pesa nyingi. Inatia moyo kwamba
duniani fasihi haiandikwi kwa Kingereza tu, bali Kichina, Kirusi, Kijerumani,
Kifaransa, Kiholanzi n.k
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia