CCM KUONDOA KODI ZA HOVYO ,YASEMA ELIMU ITAKUWA BURE HADI KIDATO CHA IV
Na Joachim Mushi, Mbulu
MGOMBEA mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Samia
Suluhu amesema chama hicho kikichaguliwa na Watanzania kuunda Serikali tena
kitahakikisha kinaweka utaratibu mzuri utakaomfanya mwananchi
mfanyabiashara kupenda kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo. Samia ametoa
ahadi hiyo Mjini Mbulu alipokuwa akiwahutubia wananchi na wanaCCM katika
mkutano wa hadhara wa kampeni za chama hicho.
Alisema watahakikisha wanaondoa kodi za hovyo hovyo ambazo zimekuwa
zikitozwa hivi sasa katika maeneo anuai. "...Tutaweka utaratibu mzuri ambao
utamfanya mwananchi apende kulipa kodi, ila kodi za hovyo hovyo
tutaziondoa...," alisema mgombea huyo mwenza wa urais akiilani ilani ya CCM
na kumuombea kura mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Pombe Magufuli.
Akihutubia mkutano mwingine Jimbo la Babati Mjini Bi. Suluhu alisema
serikali itakayoundwa na Chama Cha Mapinduzi ili kuboresha sekta ya elimu
itahakikisha inatoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne
jambo ambalo pia litawapunguzia mzigo familia na kutoa fursa sawa ya elimu
ngazi ya msingi na sekondari (kidato cha nne).
Aidha alisema serikali itakayoundwa na CCM pia itahakikisha inafanya
maboresho makubwa katika sekta ya afya, umeme, huduma za maji safi na
salama pamoja na kuwawezesha wananchi hasa makundi ya vijana na akinamama.
Alisema katika maeneo ya wafugaji watahakikisha wanashirikiana na
halmashauri kupima na kuweka mipaka ya ardhi katika vijiji ili kuondoa
mvutano wa wakulima na wafugaji.
Kuwasaidia wafugaji kujenga majosho ya nifugo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
viwanda vya kuchakata bidhaa za mifugo kuziongezea thamani. Hata hivyo
aliwahakikishia wanavijiji ambao wamekumbwa na ukame kuwa Serikali
imejipanga kuwasaidia hivyo hakuna mwanakijiji atakaye kufa kwa njaa.
Pamoja na hayo alisema Serikali ijayo ya CCM ili kuongeza kasi ya
uwajibikaji imepanga kuunda kitengo maalumu cha kupokea na kushughulikia
kero na malalamikoa ya wananchi, jambo ambalo litaweka bayana nani hataki
kuwajibika kazini.
0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia