Sehemu ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wakati wa Mkutano wa Kilele wa siku moja ambapo Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali walipitisha Tamko kuhusu nini kinatakiwa kutekelezwa katika kulikabili wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji tatizo ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa nchi mbalimbali. mkutano huo ulipitisha Tamko lijulikanalo kama Tamko la New York kuhusu wakimbizi na wahamiaji( New York Declaration for Refugees and Migration. |
Na Mwandishi Maalum, New York
Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali, jana ( jumatatu) wamepitish tamko la kwanza la
aina yake linalolenga pamoja na mambo
mengine kuichagiza jumuiya ya kimataifa
kushirikiana katika kukabili wimbi
kubwa la wakimbizi na wahamiaji.
Kupitia Tamko hilo
ambalo linatambulika kama Tamko la New
York, linazitaka serikali za mataifa
yote, bila kuingilia uhuru wa mambo yao
kama mataifa huru au ukiukwaji wa sheria za kimataifa, kuwapokea,
kuwahifadhi na kuwapatia huduma za kijamii wakimbizi na wahamiaji bila ya kujali hadhi zao.
Ni tamko ambalo
limetokana na majadiliano ya muda mrefu baina ya nchi wanachama wa Umoja
wa Mataifa, Asasi za kiraia na Mashirika
ya Kimataifa, majadiliano ambayo wakati
mwingine ililazimu wajumbe kukubaliana kutokukubaliana katika baadhi ya vipengele vya tamko hilo.
Upitishwaji wa Tamko hilo la New York kuhusu
wakimbizi na wahamiaji umefanyika ikiwa na sehemu ya uliokuwa mkutano wa siku moja
uliojadili changamoto kuhusu wakimbizi
na wahamiaji ambao idadi yao imezidi kuongeza na kubwa kuwahi kutokea.
Kwa mfano, takwimu
zinaoonyesha kwamba, mwaka 2015 idadi ya wakimbizi na wahamiaji ilifikia watu
milioni 224, ongezeko ambalo kasi yake ni kubwa kuliko ongezeko la idadi
ya watu duniani.
Hata hivyo inaelezwa
pia kwamba kuna takribani watu
65 milioni ambao wamelazimishwa kuhama, wakiwamo zaidi ya wakimbizi
milioni 21, milioni tatu wanaotafuta
hifadhi na zaidi ya milioni 40 wakiwa ni wakimbizi wa ndani.
Wakuu wa Nchi na
Serikali pamoja na wakuu wa Mashirika
na Taasisi za Kimataifa,
wanaahidi kupitia tamko hilo la New York , pamoja na mambo mengine,
kulinda haki za binadamu za wakimbizi na wahamiaji wote bila ya kujali hadhi yao.
Ikiwa ni pamoja na haki za wanawake na wasichana pamoja na kukuza fursa yao ya
kushiriki kikamilifu katika kutafuta
suluhu.
Wameahidi pia kuzuia
vitendo vya ukatili wa kingono na
udhalilishaji dhidi ya wanawake. kuhakikisha kwamba watoto wakimbizi na
wahamiaji wanapata elimu mara tu wanapofika nchi ya ugenini.
Vile
vile tamko hilo, linashauri na kupendekeza nchi ambazo zimekuwa ama
zikipokea wakimbizi na kuwahifadhi au zile ambazo ni njia
wanayopitia kwenda nchi nyingine basi zisaidiwe katika ubebaji
wa jukumu hilo.
Tamko hilo pia linataka kukomeshwa kwa tabia ya kuwaweka vizuizini watoto ili kubaini hadhi
yao ya uhamiaji. Linataka pia kutafutiwa makazi wakimbizi wote ambao
wanatambuliwa na Kamisheni ya Umoja wa
Mataifa kuhusu wakimbizi kuwa wanaohitaji makazi, pamoja na kuwatafutia fursa za kuhamia nchi nyingine.
Katika kuhakikisha changamoto
ya wakimbizi na wahamiaji
linashughulikiwa katika ukamilifu wake, Umoja wa Mataifa umeamua katika mkutano
huo wa Jumatatu kuiingiza rasmi Shirika la Kimataifa la Wahamiaji ( IOM) kuwa chini ya mfumo wa Umoja wa Mataifa.
Wakati
huo huo, Rais wa
Marekani, Barack Obama,
ameeitisha siku ya jumatano Mkutano wa Viongozi kuhusu Wakimbizi. (
Leaders’ Summit on Refugees) . Katika mkutano huo viongozi wakuu wa
nchi na serikali
walioalikwa watatarajiwa kutoa ahadi zao kuhusu namna serikali zao
zitakavyo wasaidia wakimbizi.
Tanzania ni kati ya nchi zilizoalikwa kuhudhuria na
kushiriki mkutano huo. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Augustin Mahiga ( Mb)
anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika
Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa. Anatarajiwa kuwasilisha ahadi ya
Tanzania katika Mkutano huo.