"Utafiti: Kuzimwa kwa Mitandao Duniani Kote Kumeathiri Mamilioni, Haki za Binadamu Zikihatarishwa"


Ripoti za utafiti mpya zinaonyesha kuwa kuzimwa kwa mitandao ya intaneti kumeathiri mamilioni ya watu duniani kwa njia mbalimbali, huku athari hizo zikionekana kuenea katika sekta zote za maisha.

 Kwa mujibu wa ripoti hiyo, serikali zinatumia mbinu ya kuzima mitandao kama njia ya kudhibiti mawasiliano, hasa wakati wa machafuko ya kisiasa, maandamano, au katika mazingira ya kutaka kuzuia habari fulani zisisambae haraka.



Kwa kawaida, serikali huagiza watoa huduma za mitandao kufunga au kupunguza kasi ya huduma za intaneti katika baadhi ya maeneo, hali inayowazuia wananchi kuwasiliana kwa njia ya mtandao. Katika visa vingine, serikali hufungia baadhi ya huduma za tovuti kama vile mitandao ya kijamii au majukwaa ya mawasiliano ya moja kwa moja. 

Hali hii imeonekana mara nyingi hivi karibuni, ikiwemo kufungiwa kwa mitandao maarufu kama X (zamani Twitter) na Telegram katika nchi mbalimbali kwa sababu za kisiasa.


Athari za kuzimwa kwa mitandao haziishii kwenye kutatiza mawasiliano ya kibinafsi pekee. 

Kwa mujibu wa Shirika la Human Rights Watch, hatua hiyo imewazuia watu kupata huduma muhimu za kijamii, kiuchumi, na hata zile zinazohusiana na afya. 

“Kuzimwa kwa mitandao ni mbinu ya serikali za kiimla kujaribu kukandamiza maoni ya wananchi wao, jambo linalokandamiza haki za kibinadamu,” inasema ripoti hiyo.


Kwa upande wa makundi ya haki za binadamu, kuzimwa kwa mitandao ni ukiukwaji mkubwa wa haki za msingi za watu.

 Wanaona kuwa intaneti ni nyenzo muhimu ya kupata habari, kuwasiliana, na hata kujieleza.

 Katika karne hii ya teknolojia, intaneti imekuwa haki ya msingi kama vile huduma nyingine muhimu kama maji na umeme.

 Kupitia kampeni ya #KeepItOn, mashirika yanayopigania haki za dijitali, kama vile Zaina Foundation, yamekuwa yakiendeleza juhudi za kuhamasisha jamii na serikali kutetea uhuru wa mawasiliano.

 Kampeni hii inalenga kuhakikisha kuwa kila mtu duniani ana haki ya kutumia intaneti bila vizuizi vyovyote, hata katika hali za machafuko au maandamano.


Utafiti huo umebainisha kuwa mamilioni ya watu wanaathirika moja kwa moja kutokana na kuzimwa kwa intaneti, hasa wale wanaotegemea mitandao kufanya kazi, kama vile wafanyabiashara wadogo wadogo, wanaharakati, na wanahabari. 

Athari za kiuchumi kutokana na kuzimwa kwa mitandao ni kubwa, huku ripoti zikionyesha kuwa mataifa yanapoteza mabilioni ya dola kila mwaka kutokana na hatua hiyo.


Serikali, hata hivyo, mara nyingi zinajitetea kuwa hatua ya kuzima mitandao inachukuliwa kwa sababu za kiusalama wa kitaifa au kuzuia uchochezi wa vurugu ,Hata hivyo, wataalamu wa haki za kibinadamu wanasema kuwa kuna njia mbadala za kushughulikia changamoto hizi bila ya kukiuka haki za msingi za wananchi.


Kampeni za #KeepItOn zinaendelea kuchukua nafasi muhimu ulimwenguni, zikisisitiza umuhimu wa kulinda uhuru wa mtandao ili kuhakikisha jamii zinapata fursa ya kuwasiliana, kujifunza, na kushirikiana.

 Viongozi wa kimataifa wanahimizwa kuweka mikakati madhubuti ya kisheria inayozuia serikali kutumia mbinu ya kuzima mitandao kama njia ya kudhibiti wananchi wao

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post