KIHONGOSI ASISITIZA ELIMU YA KITAALAMU KWA VIJANA KATIKA TAMASHA LA SAMIA CONNECT
Na Woinde Shizza, Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Laban Kihongosi, aliwataka vijana hususani walioko katika sekta ya utalii kuzingatia elimu ya kitaalamu na kuepuka mambo yasiyoendana na taaluma.
Kihongosi aliyasema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari alipotembelea Banda la chuo cha taifa cha utalii lililopo Katika tamasha la tatu la Samia connect linalofanyika jijini hapa ambapo alisema kuwa elimu ya kitaalamu ni msingi wa kutoa huduma bora kwa wageni wa kimataifa, jambo linaloongeza hadhi ya mkoa wa Arusha kama kisiwa cha utalii.
“Vijana wanapaswa kuwa na ujuzi wa kisasa katika utalii, iwe ni hotel, mahoteli madogo, au huduma za ziada kama usafirishaji na mwongozo wa watalii, Ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba kila mteja anapata huduma bora zinazokidhi viwango vya kimataifa,” alisema Kihongosi, akisisitiza kuwa ajira zinazoibuliwa na sekta ya utalii zinapaswa kuwa na tija na ufanisi.
Aidha, Kihongosi aliongeza kuwa tamasha la Samia Connect ni fursa kwa wananchi wa mkoa wa Arusha kuonyesha vipaji vyao na kujiendeleza kielimu.
Aidha alisema kuwa serikali inashirikiana na taasisi mbalimbali za elimu na mashirika ya kiraia ili kuhakikisha vijana wanapata mafunzo yanayowawezesha kutoa huduma bora kwa wageni.
“Ni muhimu pia wakazi wa Arusha kushiriki katika mafunzo ya kitaalamu yanayotolewa na vyuo vya utalii ili kuongeza ujuzi na kupata ajira ,hii si tu inawawezesha kiuchumi, bali pia inasaidia mkoa wetu kuwa kitovu cha utalii cha kiwango cha juu,” alisema Kihongosi.
Aidha, tamasha hilo limeambatana na mazoezi ya asubuhi (jogging) yaliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa, ambapo wananchi walianza siku yao kwa afya na mshikamano wa kijamii.
Kwa upande wake Afisa Masoko wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Eugen Malley, alisema chuo chake kimeamua kushiriki tamasha hili kuunga mkono jitihada za Rais na kutoa fursa kwa wananchi kupata mafunzo ya kitaalamu.
“Chuo chetu kinazalisha wapishi, waongoza watalii, na kutoa mafunzo kuanzia cheti hadi diploma, Utalii unachangia pakubwa kuongeza pato la taifa,” alisema Malley.
Aidha alisema Tamasha la Samia Connect limeonyesha wazi jinsi uwekezaji katika sekta ya utalii unavyoongeza ajira na mapato kwa wananchi wa kawaida, huku likisisitiza umuhimu wa elimu ya kitaalamu na ubora wa huduma.
Alisema Serikali inasisitiza kwamba sekta ya utalii ni nyenzo muhimu ya kuongeza mapato ya taifa na kuboresha maisha ya wananchi, huku ikihamasisha vijana kuzingatia elimu ya kitaalamu ili kutoa huduma bora kwa wageni wa kimataifa.
Wakazi wa mkoa wa Arusha wamejitokeza kwa wingi kushiriki tamasha la Samia Connect, jambo lililojaza viwanja vya Mgambo Uzunguni kwa shangwe na mshikamano wa kijamii, kuonyesha kuwa wananchi wanathamini fursa zinazotolewa na serikali kupitia jitihada za maendeleo.








0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia