WANACHAMA WA CCM WAKAMATWA ARUSHA

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU)mkoani Arusha inawashikilia wanachama watatu wa CCM akiwemo aliyekuwa mgombea wa nafasi ya ubunge katika jimbo la uchaguzi la Arumeru,mashariki Elirehema Kaaya ambaye ni katibu mwenezi wilaya ya Nyamagana , baada ya kuwakuta wakigawa fedha za rushwa ili kuwashawishi wajumbe wamchague  mgombea wa nafasi ya uteuzi wa ubunge Siyoi Sumari.

Kwa mujibu wa mkuu wa Takukuru mkoa wa Arusha Mbengwa Kasomambutu alisema hadi jana walikuwa wamemtia mbaroni mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite na diwani wa kata ya Mbughuni Thomas Mollel maarufu kwa jina la “Askofu” akiwa katika  kikao kilichodaiwa ni mkakati wa kugawa fedha kwa wajumbe wa mkutano walioshiriki uteuzi wa awali wa nafasi ya  ubunge kwa tiketi ya ccm.

Kasomambutu alisema askofu Mollel alikabidhiwa fungu la fedha kwa ajili ya kushawishi kundi la madiwani wa jimbo la Arumeru Mashariki ili wampigie kura Siyoi Sumari ambapo juzi alikutana na baadhi yao katika kikao ambacho hakikua rasmi wala halali kwa wakati huu.

Alimtaja mwanachama mwingine wa ccm aliyekamatwa kuwa ni,Joseph Mollel ambaye ni katibu wa umoja wa vijana wilayani Monduli, wajumbe wa kikao hicho ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini alisema kikao hicho hakikumalizika vizuri kutokana na wajumbe hao kugomea ushawishi huo wakidai kiasi chafedha kinachotolewa ni kiduchu.

“askofu alifika pale na kudai kuwa yeye ni mjumbe tu na mjumbe hauwawi ila ameombwa awashawishi wajumbe hao wakubali kufanya ujanja wowote ili kijana huyu apite halafu mtaona mambo yenu yatakavyonyooka maana Mzee hayupo yupo Ujerumani jamani”alisema Mjumbe huyo.

Kasumambutu alifafanua kuwa, mtuhumiwa mwingine aliyekamatwa jana na kuhojiwa ni aliyekua mgombea wa nafasi ya utezi ndani ya CCM kabla ya uchaguzi huo kurudiwa leo Elirehema Kaaya(katibu mwenezi CCM Nyamagana) ambae alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo.

Alisema mtuhumiwa huyo ambaye baada ya kuhojiwa amekutwa na tuhuma za kupewa jukumu la kuwashawishi kwa rushwa wajumbe wote waliompigia kura katika uchaguzi wa awali wapatao 205 ili wahamishie kura zao kwa mgombea Siyoi ili kumuwezesha kushinda.

Mmoja wa wajumbe waliokuwa wakishawishiwa na mtuhumiwa huyo ambae hakutaka jina lake litajwe gazetini alidai kuwa Elirehema alitumwa na mtoto wa kigogo mmoja aliyekutana nae Dar es Salaam kuja kushawishi kundi hilo kwaajili ya kumuwezesha Siyoi kushinda.

Alisema kwa sasa taasisi yake bado inaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine zaidi ya watatu waliokimbia katika tukio la jana na kutelekeza pikipiki walizokuwa wakitumia baada ya kukurupushwa na wenzao kukamatwa, katika kikoa haramu katika baa iitwayo Levis iliyoko kata ya Maji ya Chai wilayani Arumeru.

Pamoja na hili alisema taasisi yake inazishikilia pikipiki mbili zilizokutwa katika eneo hilo mojawapo ikidaiwa ni ya katibu hamasa wa UVCCM Arumeru John Nyiti ambae anahisiwa alikuwepo katika kikao hicho na kukimbia.

Kufuatia kukamatwa kwa watuhumiwa hao Askofu Mollel katika kikao chake na waandishi wa habari alimtupia lawama mkuu wa mkoa wa Arusha Magessa Mulongo kuwa ndiye aliyehusika kuwatuma takukuru kuwakamata.

Akijibu tuhuma hizo Mulongo alisema Takukuru ni taasisi inayojitegemea hivyo hana mamlaka ya kuwaagiza kufanya kazi na kuwataka wale wote waliokamatwa kwa tuhuma hizo wajibu tuhuma zao kwa mamlaka hiyo badala ya kuanza kutafuta mchawi.

Alisema taasisi hiyo iko kwaajili ya kila mtu bila kujali kuwa yeye ni nani hivyo mtu hapaswi kuanza kuzua madai yasiyo na msingi kwa kumtuhumu mtu kuwa anahusika na wao kukamatwa kwakua chama kilionya masuala yote ya rushwa katika uchaguzi huo.

“mimi nasema askofu na wenzake wajibu tuhuma zao kama umekutwa ugoni na mke wa mtu usiseme hapa lazima Fulani anahusika kunitaja bali jibu tuhuma za kukutwa ugoni na mke wa mtu usitafute mchawi takukuru sisi wote ni wateja wao”alisema Mulongo.
 
     

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post