Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus
Makunga amewataka viongozi kuanzia ngazi za vijiji,kata,tarafa mpaka wilayani pamoja na
wataalamu wakiwemo maofisa ugani kuhakikisha wanatumia mwezi huu wa mwanzo wa
mvua za masika kuwaelimisha wananchi kuhusiana na mbinu za kukabiliana na
ugonjwa mpya na hatari wa mahindi.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa agizo
hilo wakati anafungua kikao cha dharura cha kuweka mikakati ya kukabiliana na
ugonjwa huo kilichowashirikisha watalamu
wa kilimo kutoka vituo vya utafiti nchini pamoja na wadau,viongozi wa ngazi
mbalimbali,maofisa ugani wa vijiji,viongozi wa dini pamoja na viongozi wa siasa
wakiwemo madiwani.
Makunga ameeleza baada ya kikao
hicho viongozi wa ngazi ya vijiji wanatakiwa kuitisha mikutano ya vijiji na
wale wa kata kukaa katika vikao vya maendeleo ya kata ndani ya wiki mbili ili
kuweka mkakati wa kuelimisha wananchi jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huo
hatari wa mahindi unaofahamika kama Lethal Necrosis Disease.
Aidha amewaagiza wataalamu wa ugani
kutumia muda wa siku saba kufanya tathimini ya maeneo yao endapo kuna ugonjwa
huo na kuwashilisha taarifa hizo katika vikao vya Halmashauri za vijiji na
Kamati za maendeleo za kata na baadaye mwisho wa mwezi katika halmashauri ya
wilaya ya Hai.
Ameonya kuwa endapo kila mdau
atazembea katika kuhakikisha anatimiza wajibu wake kuwepo kwa ugonjwa huo
litakuwa janga kubwa kutokana na idadi kubwa ya wananchi katika wilaya hiyo
kutegemea zaidi mahindi kwa matumizi ya family,kipato pamoja na malisho ya
mifugo.
Makunga pia ameitaka halmashauri ya
wilaya kuhakikisha inasambaza kwa wingi vipeperushi vinavyohusiana na ugonjwa
huo ili elimu iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi badala ya kuendelea kubaki
navyo katika maofisi.
Awali mtaalamu mtafiti kutoka kituo
cha utafiti wa kilimo cha Selian cha Arusha Dk Peter Matowo ameeleza kuwa
madhara makubwa ya ugonjwa huo ni pamoja na uharibifu shambani unaoweza kufikia
asilimia mia moja kwa mimea kufa na kukosa mavuno,magunzi na punje zilizoathirika
kuwa na sumu ya magonjwa hatari ya ukungu kwa binadamu na kutofaa kwa malisho
ya mifugo.
Ameeleza kuwa ugonjwa huo unaenezwa
na virusi na kwamba hauna tiba wala mbegu kinzani na hivyo njia pekee ya
kudhibiti ni kwa wakulima kuzingatia kanuni zinazoshauriwa zikiwemo za kung’oa
mara moja mimea iliyoathirika,kupiga dawa za kuua wadudu aina ya
thrips,beetles,leafhoppers na aphids waenezao ugonjwa huo,kupanda mazao mara tu
mvua zinyeshapo pamoja na kilimo cha mzunguko wa mazao.
Ugojwa huo ulianza nchini Marekani
mwaka 1976 na kuingia katika nchi za Kenya mwaka 2011 na Tanzania mwaka 2012 na
kuenea katika wilaya za mkoa wa Kilimanjaro,Arusha na Mwanza
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia