Mojawapo
kati ya vipaumbele muhimu vya Marekani nchini Tanzania ni kukuza
maendeleo ya kiuchumi na kujenga uwezo (empowerment) wa raia wote kwa
ubia na Watanzania kutoka sekta zote. Nchi hii imejaaliwa neema ya kuwa
na maliasili nyingi na utajiri mkubwa, mbali na kuwa na vivutio vingi
vya dunia kama vile Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama za Taifa na
maeneo ya urithi wa Dunia yanayotambuliwa na UNESCO kuanzia Kilwa
Kisiwani hadi Zanzibar. Wakati dunia ikitambua hazina hizi kuwa na
thamani kwa dunia nzima, bado ukweli ni kuwa, kwa njia ya kipekee kabisa
hazina hizi ni za Kitanzania. Pamoja na hali hii, baadhi ya raia
wanajiuliza ni kwa namna gani uchumi wa Tanzania utabadilika na kuwa ule
wenye kuleta ustawi.
Mustakabali
wa maendeleo ya Tanzania utategemea mawazo na maono ya uongozi wa
Watanzania wenyewe. Nimevutiwa sana na jitihada za Watanzania kutoka
serikalini na taasisi huru za kiraia kutafuta njia mpya zenye uwazi,
uwajibikaji na uadilifu zaidi katika kusimamia na kutumia utajiri mkubwa
wa asili ambao nchi hii imejaliwa kwa manufaa ya wote. Mpango wa
Kimataifa wa Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia
zinazohusika na Uvunaji Maliasili (Extractive Industry Transparency
Initiative - EITI) ni nyenzo inayoweza kusaidia katika kufikia azma hii
adhimu na inayostahili kufikiwa kwa haraka .
Yatupasa
tutambue kuwa zaidi ya watu bilioni 3.5, takriban nusu ya watu wote
duniani, wanaishi katika nchi zilizo na utajiri wa asili kwa mfano
mafuta, gesi na madini. Hata hivyo, katika maeneo mengi, utajiri huu
hautumiki katika kusaidia mipango ya maendeleo ya mataifa yao au
kusaidia kuwakwamua raia kutoka katika lindi la umasikini. Mojawapo
kati ya sababu kuu ya hali hii ni kuwa uvunaji wa rasilimali hizi hutoa
changamoto nyingi kwa serikali. Changamoto hizo ni pamoja na ile ya
kuhakikisha kuwa uvunaji huo unasimamiwa kamilifu, kwa uwazi na kwa njia
inayowahusisha kikamilifu wadau wote. Kutokana na hali hii huu ni
wakati mwafaka wa kufikia makubaliano mapana kuhusu viwango vya juu
tunavyopaswa kuvifikia katika usimamizi wa rasilimali hizi.
Tarehe
23 na 24 Mei mwaka huu, wawakilishi wa serikali, sekta binafsi na
jumuiya huru za kiraia kutoka duniani kote walikutana huko Sydney,
Australia kwa ajili ya Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa EITI. EITI ni
mfumo kimataifa ambao serikali kwa hiari yao zenyewe, huahidi kusimamia
kwa uwazi na uwajibikaji shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya
mafuta, gesi na madini katika nchi zao. Ni kwa sababu hiyo, Marekani
inaelekea kuungana na Tanzania na jumuiya ya mataifa mengine zaidi ya 35
kutoka Afrika, Asia, Marekani ya Kusini na Ulaya ambayo yameonyesha
dhamira ya kuwajibika kwa dhati na kwa uwazi kwa watu wao kwa kuwa
wanachama kamili wa EITI.
Kwa
kupitia EITI, nchi wanachama hushirikiana na sekta binafsi na asasi za
kiraia kuchapisha taarifa ya mwaka ambayo, pamoja na mambo mengine,
huonyesha taarifa za mapato ambayo serikali imeyapata pamoja na taarifa
za mapato ya makampuni yanayojihusisha na shughuli za uchimbaji na
biashara ya mafuta, gesi na madini. Mfumo huu huongeza uwazi, huimarisha
uaminifu na kutoa takwimu muhimu zinazohitajika katika kuhakikisha na
kufuatilia uwajibikaji.
Marekani
imekuwa ikiisaidia EITI toka kuanzishwa kwake zaidi ya miaka kumi
iliyopita. Mwezi Desemba 2012, tulifurahishwa na tangazo kwamba
Tanzania imekuwa nchi ya kumi barani Afrika kukidhi viwango vya EITI.
Tunapongeza hatua hii kubwa iliyopigwa na Tanzania katika kukuza uwazi
na uwajibikaji. Jitihada za Tanzania kujiunga na EITI zilianza mwaka
2009 na kufanikiwa kwake kufanya hivyo katika kipindi cha miaka mitatu
tu kunaonyesha jinsi misingi EITI kuhusu uwazi katika mapato ilivyo na
manufaa kwa nchi zote katika kanda zote na viwango vyote vya maendeleo.
Bunge
la Marekani huzitaka baadhi ya kampuni za Kimarekani zinazojihusisha na
shughuli za mafuta, gesi na madini kuwasilisha taarifa zao za kila mwaka
kwa Tume ya Masoko ya Hisa (U.S. Securities and Exchange Commission)
kubainisha malipo mahsusi wanayoyatoa kwa serikali mbalimbali duniani
kwa ajili ya shughuli za mafuta, gesi na madini. Taarifa hizi
zitajumuishwa na zile za EITI kuonyesha malipo yanayopokelewa na
serikali mbalimbali kutokana na maliasili zake, hata kama nchi hizo si
wanachama wa EITI.
Hata
hivyo, uwazi katika mapato pekee hautoshi kuwasaidia raia kuona picha ya
jumla ya jinsi ambavyo serikali zao zinasimamia rasilimali yao ya
mafuta, gesi na madini. Ni lazima twende mbali zaidi. Hivyo wiki hii
mjini Sydney, wanachama watakubaliana kuhusu mabadiliko kadhaa ya
kimkakati katika mpango wa EITI.
Lengo
ni kufanya taarifa za EITI kuwa za kina na zenye kuaminika zaidi na
zilizo rahisi kufanyiwa uchambuzi. Aidha, mabadiliko hayo yatazitaka
serikali kutoa taarifa muhimu kwa raia wake kuhusu sekta za mafuta, gesi
na madini katika nchi zao, ikiwa ni pamoja na taarifa kuhusu leseni
zilizotolewa, makampuni au watu waliopewa leseni hizo, kiasi gani
kinazalishwa na nafasi ya makampuni ya mafuta/madini yanayomilikiwa na
serikali katika sekta husika. Aidha, EITI itazihimiza serikali kwenda
mbali zaidi na kuchapisha kwa hiari yao wenyewe mikataba halisi
iliyoingia na makampuni husika. Utaratibu huu wa uwazi, utakuwa na
manufaa kwa Makampuni ya Kimarekani kwa kuyawezesha kuyaelewa vizuri
mazingira ya kiutendaji na kibiashara ya nchi husika yanapofikiria
kufanya maamuzi kuhusu uwekezaji.
Marekani
inaunga mkono mabadiliko haya yatakayowezesha EITI kuwa chombo che
ufanisi zaidi katika kuwasaidia raia katika nchi zenye utajiri mkubwa wa
maliasili kufaidika kutokana maliasili hizo. Wakiwa na taarifa,
wananchi wataweza kuziwajibisha serikali zao hivyo jamii yote kwa ujumla
kunufaika kutokana na mapato yatokanayo na rasilimali zake. Kwa kuwa na
uwazi na matumizi yenye ufanisi ya maliasili, raia ambao hapo awali
walikuwa katika lindi la ufukara nao pia wataweza kuwa na tumaini la
kuwa na mstakabali mwema wenye ustawi ambapo wataweza kupata huduma bora
za afya, elimu bora na kuweza kutumia uwezo wao kwa kadri ya upeo wao
kuchangia katika maendeleo ya Tanzania.
Alfonso E. Lenhardt
Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia