Kutokana na juhudi za kiwanda hicho, Serikali inapaswa
kukipatia ruzuku. Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha vikombe kati ya
1,500 mpaka 2,000 kwa siku.
Kama unatabia ya kupenda kukagua bidhaa kwa lengo
la kujua zinatengenezwa wapi, basi ni rahisi kwa kuwa vikombe vingi
vinavyotumika kunywea chai, vimetengenezwa China.
Ukifika wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro utakuta
kiwanda cha kutengenezea bidhaa hizo zinazotumika kunywea chai pamoja
na matumizi mengine.
Tununue bidhaa zetu
Kiwanda cha Kilimanjaro Industries Development
Trust (KIDT) ambacho ni tawi la Kiwanda kikuu kilichopo Moshi kimekuwapo
wilayani hapo kwa takribani miaka 30, kikizalisha vikombe, sahani,
bakuli, birika, majagi na vifaa vya kuwekea maua.
Bidhaa hizo zinazozalishwa kutokana na malighafi
zinazopatikana wilayani humo, wilaya jirani ya Mwanga na malighafi
nyingine kutoka Pugu Dar es Salaam.
Msimamizi wa Kiwanda hicho, Loveness Mhina anasema
vikombe hivyo vya udongo na bidhaa nyingine wanazotengeneza wanatumia
mawe wanayoyatoa eneo la Kavambughu, nje kidogo ya wilaya hiyo, udongo
maalum wanaochimba eneo la Kifula wilayani Mwanga na Kaolini
inayopatikana Pugu Dar es Salaam. Mhina anasema kiwanda hicho kwa siku
kina uwezo wa kuzalisha vikombe kati ya 1,500 hadi 2,000 kwa siku.
Mbali na kutengeneza vyombo hivyo vya mezani pia
kiwanda hicho kinatengeneza vifaa visivyopitisha umeme (insulators),
vinavyotumiwa na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) ambavyo navyo
hutengenezwa kwa malighafi hizo.
Miaka 30 kiwanda kimefanya nini?
Meneja Mkuu wa KIDT, Mhandisi Frank Elisa, anasema
kiwanda hicho kilipaoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1980,
hakikuanzishwa kwa lengo la biashara.
“Wajapan ndiyo walioanzisha viwanda hivi na lengo
lao lilikuwa kuanzisha viwanda vidovidogo kwa kutumia raslimali
zinazopatikana maeneo husika.Kwa mfano, malighafi za kiwanda hiki,
nyingi zinatoka Same,” anasema.
Anasema fursa za biashara zipo nyingi, lakini changamoto kubwa inayowakabili ni mtaji wa kukipanua kiwanda hicho.