KENYATA AWATAJA WALIOHUSIKA NA ULIPUAJI

Askari wa Kenya wakiwa juu ya jengo la Westgate jana kuwasaka magaidi walioteka watu tangu Jumamosi. Picha ya AFP

Nairobi. Wakati jengo la ghorofa tatu lililovamiwa na magaidi likiripotiwa kuanguka jana na kuua watu sita, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema mwanamke mmoja raia wa Uingereza na Wamarekani wawili au watatu wanashukiwa kuongoza shambulizi la kigaidi lililofanywa katika jengo la biashara eneo la Westgate, Nairobi, Jumamosi iliyopita.
Akilihutubia taifa la Kenya jana, Rais Kenyatta alisema hakuna ushahidi wa kuwahusisha watu hao na tukio hilo moja kwa moja  lakini uchunguzi unaendelea.
“Wataalamu wa mambo ya upelelezi wanaendelea kuchunguza juu ya ushiriki wa watu hawa na wakiwabaini, basi tutachukua hatua kali,” alisema Rais Kenyatta.
Tangu kutokea kwa shambulizi hilo, vyombo mbalimbali vya habari vilimtaja mwanamke wa Uingereza, Samantha Lewthwaite kuwa ndiye aliyeongoza shambulizi hilo.
Pia jina lake lilitajwa na Kundi la Al-Shabaab kupitia katika mtandao wa mawasiliano wa kijamii wa Twitter.
Hata hivyo, maelezo ya Rais Kenyatta yanapingana na ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi hiyo, Joseph ole Lenku ambaye alikaririwa na vyombo vya habari jana akidai kuwa hakukuwa na mwanamke miongoni mwa magaidi hao, bali baadhi yao walivaa nguo za kike.
Rais Kenyatta alisema magaidi watano walikuwa wameuawa katika operesheni hiyo ya kulikomboa jengo hilo.
Pia alibainisha kuwa watu kumi na moja walikuwa wanashikiliwa na polisi wakishukiwa kushiriki katika shambulio hilo.
Magaidi wanaoaminika kuwa wafuasi wa Kundi la Al-Shabaab walivamia jengo hilo na kufanya shambulizi lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 60 na 175 kujeruhiwa, Jumamosi iliyopita.
Rais Kenyatta aliapa kuwa Serikali yake imepania kuwashinda magaidi na kuhakikisha inawafikisha kwenye mikono ya sheria.
Ghorofa kuanguka
Pia Rais Kenyatta alitangaza kuwa maofisa sita wa usalama walifariki dunia jana jioni baada ya kuangukiwa na ukuta baada ya kudondoka kwa ghorofa tatu za jengo ambalo magaidi wamejichimbia.
CHANZO mwananchi

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post